Kocha wa Bordeaux Willy Sagnol akosolewa kwa matamshi ya ubaguzi
(GMT+08:00) 2014-11-18 09:44:10
Kocha wa klabu ya soka Bordeaux iliyopo nchini Ufaransa Willy Sagnol amekosolewa vikali kufuatia matamshi yake kuwa wanasoka kutoka Afrika wana nguvu lakini hawana maarifa wala nidhamu. Kwenye mahojiano na gazeti moja Sagnol mwenye miaka 37 alisema umuhimu wa wanasoka kutoka Afrika ni kwamba wao ni rahisi na wako tayari kupambana, na kusisitiza kuwa mchezo wa soka hauhitaji vitu hivyo tu bali unahitaji mbinu, maarifa na nidhamu. Rais wa klabu ya Bordeaux Jean-Louis Triaud amemtetea kocha huyo akisema matamshi yake yametafsiriwa vibaya, kwani yeye sio mbaguzi. Mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa Lilian Thuram ameyakashifu matamshi ya kocha huyo huku chama kinachopambana na ubaguzi wa rangi kikitaka kocha huyo kuchukuliwa hatua. Matamshi hayo ya Sagnol yamekuja siku ambayo rais wa Shirikisho la Soka la Italia Carlo Tavecchio kuzuiwa na FIFA kushika wadhifa wowote kwa miezi 6 kutokana na kutoa matamshi ya kibaguzi. Uefa imempiga marufuku Tavecchio kwa miezi 6 kuanzia Oktoba 7 baada ya kutolea mfano "kula ndizi" wakati anajadili wimbi la wachezaji kutoka nje kwenye soka ya Italia.