Dereva Lewis Hamilton atwaa ubingwa wa pili kwenye mashindano ya Fomula One
(GMT+08:00) 2014-11-24 15:05:57
Dereva wa Uingereza Lewis Hamilton jioni ya jana amefanikiwa kutwaa ubingwa wa msimu huu kwenye mashindano ya mbio za magari yaendayo kwa kasi maarufu kama Formula one ya Abu Dhabi Grand Prix. Dereva huyo wa Mercedes aliyefanikiwa kutwaa ubingwa wake baada ya kumaliza mbele ya Felipe Massa toka Brazil na Valteri Boltas wa Finland amesema ushindi huu wa mara ya pili anahisi ni muhimu zaidi kuliko wa awali alioshinda akiwa na McLaren mwaka 2008. Hamilton anamaliza kwenye msimamo wa madereva akiwa amejikusanyia jumla ya pointi 384 akiwa amemzidi mwenzie toka timu ya Mercedes Mjerumani Nico Rosberg kwa pointi 67. Hamilton na Rosberg wamekuwa na upinzani mkubwa tangu kuanza kwa msimu huu ambapo wamegawana mara ambazo kila mmoja ameongoza msimamo wa madereva huku kwa karibu msimu mzima ukiongozwa na madereva hao toka Mercedes. Bingwa mtetezi kabla ya kutwaa kwa Lewis Hamilton Mjerumani Sebastian Vettel ambaye juzi alitangazwa rasmi kuwa dereva mpya wa timu ya Ferarri alikuwa na msimu mbaya ambapo amemaliza kwenye nafasi ya tano katika msimu ambao hakufanikiwa kushinda mbio hata moja. Ushindi huu unamfanya Hamilton kuweka Historia ya kuwa dereva wa nne toka Uingereza kushinda ubingwa wa Formula one kushinda mataji mawili ya dunia, na kuwa kiwango kimoja na Jim Vlark pamoja na Graham Hill ambapo sasa yupo nyuma ya Sir Jackie Stewart. Hamilton pia ameendelea kuweka rekodi nyingine kama Muingereza aliyeshinda mbio nyingi ndani ya msimu mmoja kwa kushinda jumla ya mbio kumi na moja. Hadi sasa Michael Schumacher ndiye anayeshikilia rikodi kwa kushinda mataji saba.