Welbeck hakutakiwa kuondoka Man United, Rooney awanyamazisha Arsenal
(GMT+08:00) 2014-11-24 15:06:46
Nahodha wa zamani wa Manchester United, Paul Ince anaamini kuwa klabu yake hiyo ya zamani haikutakiwa kumruhusu Danny Welbeck kuondoka na kusema kuwa alipoondoka kwenye klabu hiyo wachezaji walipatwa na mshituko. Ameongeza kuwa Welbeck alikuwa na uwezo wa kucheza nyuma na mshambuliaji nayetengeneza nafasi kwa wengine kufunga. Welbeck, ambaye sasa ana miaka 23, aliyekuwa Old Trafford akiwa na miaka minane, alijiunga na Arsenal kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 16. Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alipangwa kuivaa timu yake ya zamani katika mchezo wa juzi usiku wa Ligi Kuu England kwenye Uwanja wa Emirates. Katika mchezo huo Manchester United ikapata ushindi wa kwanza ugenini msimu huu baada ya kuifunga Arsenal 2-1 kwenye uwanja wao wa Emirates, jijini London. Kieran Gibbs alianza kwa kujifunga kabla ya nahodha wa England na Manchester United Wayne Rooney kufunga goli la pili na la ushindi kwa timu yake. Goli hilo limemfanya Wayne Rooney kuwa ndio mchezaji aliyeifunga magoli mengi zaidi klabu ya Arsenal kwa kukusanya jumla ya magoli 11. Kwa maana hiyo Rooney amempita mshambuliaji wa zamani wa Liverpool na England Robbie Fowler ambaye ndio alikuwa anaongoza kwa kuifunga Gunners kwa magoli 10. Rooney alianza kuifunga Arsenal katika mechi yake ya kwanza kabisa ya ligi kuu ya England, wakati akiwa na miaka 16 alipokuwa akiichezea klabu ya Everton. Goli la Rooney limeifanya Arsenal kupoteza mechi yao ya kwanza kwenye uwanja wao wa Emirates kwenye msimu huu.