• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nini mustakbali wa Burkina Faso baada ya kupata rais wa mpito?

    (GMT+08:00) 2014-11-28 20:17:54

    Wakati hali ya Burkina Faso ikiekelea kutulia baada ya rais wa muda Bw Michel Kafando kuapishwa, matukio yaliyotokea nchini Burkina Faso katika muda wa wiki chache zilizopita yanafanya watu wajiulize ni nini kinaendelea kwenye demokrasia ya nchi za Afrika. Tarehe 31 Oktoba, baada ya shinikizo kutoka kwa waandamanaji, Rais wa Burkina Faso Bw Blaisse Compaore aliamua kujiuzulu na kukimbilia Ivory Coast. Kitendo hicho kinaonekana kwa baadhi ya watu kama ni mwendelezo ya kulichotokea Tunisia, Libya na Misri, lakini hali ya jumla ya utulivu na uvumilivu iliyooneshwa na watu na taasisi mbalimbali za Burkina Faso, imewafanya baadhi ya watu wajiulize ni nini kinaendelea katika nchi hiyo.

    Moja linalotakiwa kutajwa, ni kuonekana kwa ukomavu wa kisiasa kwa wananchi wa kawaida wa Burkina Faso hasa kuamua kutoa sauti ya kulinda katiba ya nchi kwa maandamano ya amani. Pili ni utulivu na usikivu uliooneshwa na pande mbalimbali, likiwemo jeshi la nchi hiyo. Baada ya Rais Blaisse Compaore kukimbilia Ivory Coast, jeshi lilitangaza kutwaa madaraka lakini baada ya mawasiliano na nchi jirani na jumuiya za kikanda, pande hizo zimeonesha utulivu na usikivu, na kufanya mpito wa nchi hiyo uendelee salama. Katika miaka ya nyuma kila tukio la kuondolewa madarakani kwa Rais wa nchi, lilifuatiwa na vurugu kubwa na hata mauaji, wakati mwingine majeshi yalitumia nguvu kubwa kurudisha utulivu kwa nguvu na hata kung'ang'ania madaraka. Uwajibikaji uliooneshwa na jeshi la Burkina Faso na pande nyingine ni wa kihistoria ambao unaonekana kuweka mfano kwa nchi nyingine za Afrika.

    Inatakiwa kukumbukwa pia kuwa katika siku za nyuma nchi za Afrika zenyewe hazikuwa na sauti kubwa kushughulikia matukio kama hilo, sauti kubwa iliyokuwa inasikika baada ya kutokea kwa matukio kama hiyo ni kutoka nchi za magharibi, (hasa kwa nchi zilizokuwa watawala wa nchi zinazokumbwa na matukio hayo) lakini safari hii tumeona Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, Rais Mack Sall wa Senegal, na Rais John Mahama wa Ghana ambaye pia ni mwenyekiti wa ECOWAS, pamoja na maofisa wa Umoja wa Afrika wakiwa mstari wa mbele katika kuhakikisha suala hilo linatulizwa. Matukio haya pamoja na waandamanaji kutosukumwa na nguvu kutoka nje, vinaleta sura ambayo kwa kiasi fulani inatia moyo.

    Hata hivyo kuna baadhi ya mambo ambayo yanayotakiwa kufuatiliwa, ambayo huenda yakafanya hali ya baadaye ya Burkina Faso iwe ya utatanishi zaidi. Kwanza, baada ya kuingia madarakani, Rais wa mpito Bw Michel Kafando alisema ataruhusu uchunguzi ufanyike kuhusu mauaji ya aliyekuwa rais wa Burkina Faso Captain Thomas Sankara, ambaye aliuawa katika mapinduzi yaliyoongozwa na Bw Blaisse Compaore. Zaidi ya miaka 27 iliyopita tangu Kapteni Thomas Sankara auawe, mazingira ya kifo chake bado hayako wazi. Mke wake Bibi Mariam Sankara amekuwa akiomba kila mara uchunguzi wa DNA ufanyike kuhusu yanayodaiwa kuwa ni mabaki ya mwili wake. Haijulikani ni kwanini Bibi Mariam anadai sana uchunguzi huo ufanyike, na matokeo ya uchunguzi huo yatakuwa na maana gani kwa utulivu na mshikamano wa waburkinabe. Jumatatu wiki hii pia maandamano ya kupinga uteuzi wa Bw Adama Sagnon kuwa waziri, kwa madai kuwa alificha habari kuhusu mauaji ya mwandishi mmoja wa nchi hiyo Norbert Zongo mwaka 1998, yanafanya hali ya baadaye isijulikane.

    Pili, ni wachache wanaoamini kuwa kwa sasa kuna mazingira yanayoonesha kuwa hali ya kijamii na kiuchumi ya waburkinabe inaweza kubadilika ndani ya muda mfupi. Maandamano yaliyomuondoa Rais Compaore madarakani, pamoja na kuwa yalionekana ni hatua ya kulinda katiba ya nchi, ndani yake kulikuwa na alama za malalamiko ya hali ya kiuchumi na kijamii inayowasumbua watu wengi wa Burkina Faso. Kwa hiyo bado ni mapema kusema bila shaka kuwa mwelekeo wa Burkina Faso katika siku zijazo utakuwa wa utulivu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako