• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maonesho ya vitu vya kale ya China na Tanzania yahimiza mawasiliano ya kiutamaduni kati ya nchi hizo

    (GMT+08:00) 2014-12-16 18:40:03

    Maonyesho ya vitu vya kale ya China na Tanzania kuhusu historia ya Njia ya Hariri Baharini inayounganisha China na Afrika yamefunguliwa Dar es Salaam, Tanzania. Hii ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania. Lengo la maonesho hayo ni kupitia historia ya mawasiliano ya kirafiki yaliyodumu kwa miaka elfu kadhaa kati ya China na Afrika, na kuonesha mbinu ya usafiri baharini katika siku za kale za China na nia ya watu ya kuchunguza dunia isiyofahamika.

    Vitu 41 vya kale vilivyotolewa na Jumba la Makumbusho la historia ya usafiri nje ya nchi la Quanzhou na vitu 24 vya Jumla la Makumbusho la Tanzania vinaoneshwa kwenye maonesho hayo yatakayodumu kwa mwezi mmoja. Akieleza maana ya historia ya Njia ya Hariri Baharini, mkuu wa Jumba la taifa la Makumbusho la Tanzania Dkt. Aujax Mabula anasema,

    "Hariri na kauri za China vilifika Afrika Mashariki kupitia Njia ya Hariri Baharini, na kuleta mawasiliano ya kiutamaduni, kimawazo na kidini kati ya pande hizo mbili. Kupitia njia hiyo, China imetoa mchango mkubwa katika sekta ya utamaduni kwa Afrika Mashariki na hata sehemu nyingine duniani."

    Kama alivyosema Dkt Mabula, Njia ya Hariri Baharini iliyounganisha China na Afrika ilihimiza mawasiliano kati ya Asia na Afrika katika sekta za utamaduni, usanii na teknolojia. Kufanyika maonesho hayo ya historia ya Njia ya Hariri Baharini kati ya China na Tanzania pia kunatokana na ushirikiano mkubwa kati ya nchi hizo mbili. Ili kuandaa maonesho hayo, wataalamu wa mambo ya kale wa China na Tanzania walikutana kwa mara nyingine. Kwa mujibu wa kaimu balozi wa China nchini Tanzania Li Xuhang, vitu vya kale vinavyooneshwa kwenye maonesho hayo vinatolewa kwa pamoja na China na Tanzania, hali ambayo ni ya kwanza kutokea barani Afrika.

    Imefahamika kuwa vitu vya kale vya kichina vilivyotolewa na Tanzania katika maonesho hayo vyote viligunduliwa nchini humo, na vingi kati ya hivyo havijawahi kuoneshwa kwa umma, hivyo wataalamu wa mambo ya kale wa Tanzania pia wana matarajio makubwa na maonesho hayo.

    Profesa Qin Dashu, ambaye ni mwalimu wa idara ya akiolojia katika Chuo Kikuu cha Beijing aliwahi kuongoza timu ya wataalamu wa mambo ya kale ya China kufanya utafiti katika pwani ya Kenya. Prof. Qin amesema maonesho hayo yameonesha ukubwa na sifa ya biashara ya China ya zamani katika Afrika Mashariki, na maingiliano ya China na Afrika kabla ya msafara wa Zhenghe kufika kwenye eneo hilo. Anasema, 

    "Maonesho hayo yameondoa ufahamu mbaya kuwa biashara kati ya China na Afrika Mashariki ilianza wakati msafara wa Zhenghe ulipofika kwenye eneo hilo. Lakini biashara hiyo ilianza katika zamani wakati wa enzi ya Song ya Kusini, na ilifikia kilele chake ifikapo enzi ya Ming. Na kiuhalisia vyombo vya kauri vya kichina viligunduliwa katika sehemu za pwani za nchi nyingi za Afrika Mashariki zikiwemo Somalia, Kenya, Tanzania na hata Msumbiji."

    Konsela wa utamaduni wa China nchini Tanzania Liu Dong amefafanua kuwa maonesho hayo yamefungua ukurasa mpya kwa mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na Tanzania, na pia ni mwanzo na fursa ya kufanya ushirikiano kati ya watafiti wa mambo ya kale wa nchi hizo mbili. Anasema,

    "Kuonesha vitu vya kale vya kichina nchini Tanzania kunaweza kuhimiza mawasiliano ya kiutamaduni kati ya nchi hizo mbili. Hivi sasa, tunazungumza na Mamlaka ya vitu vya kale ya taifa ya China kuhusu kufanya ushirikiano na Tanzania katika kuandaa maonesho ya vitu vya kale, kwani Tanzania ina udhaifu katika sekta ya jumba la makumbusho, na tunatarajia kutoa msaada kwa Tanzania kupitia maonesho hayo."

    Katika miaka ya hivi karibuni, mbali na kuendeleza mambo ya kisiasa na kibiashara, China na Tanzania zimefanya ushirikiano katika utamaduni na elimu na kupata mafanikio. Madarasa mawili ya taasisi ya Confucius yameanzishwa katika vyuo vikuu viwili nchini Tanzania, tamthiliya za Kichina ikiwemo Mao Doudou na Mama Wakwe Zake toleo la Kiswahili zimeoneshwa nchini Tanzania, idadi ya wanafunzi wa Tanzania wanaoweza kupata udhamini wa masomo kutoka China pia inaongezeka mwaka hadi mwaka.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako