Wanariadha wa Kenya Viola Chelangat Kimetto na Joyce Jemutai Kiplimo wamepigwa marufuku kwa miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa haramu za kusisimua misuli. Taarifa kutoka kwa shirikisho la riadha nchini Kenya imesema wanariadha hao wawili wa kike walipatikana na hatia ya kutumia dawa aina ya Norandrosterone. Kimetto alipatikana na hatia Disemba mwaka jana huku Kiplimo akipatikana na kosa hilo baada ya kushiriki mbio za masafa marefu mjini Yangzhou China Aprili mwaka huu.
Shirikisho la riadha la Kenya limesema linachunguza wanariadha wengine watano wanaoshukiwa kutumia dawa hizo haramu. Aidha shirikisho hilo limewataka wanariadha hao kufika kwenye makao yake makuu siku ya Alhamisi kujadili masuala kadhaa kuhusiana na utumiaji wa dawa hizo zilizopigwa marufuku.