Timu zitakazoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa jana zilifahamu wapinzani wake katika michuano hiyo kwa msimu wa mwaka 2014/2015 baada ya ratiba ya michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika na kombe la shirikisho kupangwa huko Cairo. Ratiba hiyo inaonyesha kuwa mabingwa Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2013/14, Azam FC wamepangwa kucheza na Timu ya El Merreikh ya Sudan. Mechi hiyo ya Ligi wa Mabingwa Afrika itakuwa ya kwanza kwa Azam FC katika kampeni zao za kuwania na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Huku Hii ikiwa ni mara ya kwanza timu hiyo kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Taarifa ya Caf ni kwamba Azam FC itaanzia nyumbani Dar es Salaam na kumalizia ugenini mechi ya pili mjini Kharthoum. Wawakilishi toka Zanzibar KMKM nao watacheza na timu nyingine toka Sudan ya Al Hilal. Wakati huo huo Timu ya Yanga itaanza kampeni yake ya Kombe la Shirikisho kwa kuivaa BDF IX ya Botswana inayomilikiwa na Jeshi la nchi hiyo. Yanga itaanzia nyumbani na kumalizia ugenini dhidi ya Waswana hao waliowahi kung'olewa na Timu ya Simba.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |