Kiungo mshambuliaji wa Borrusia Dortmund Marco Reus huenda akashindwa kutimiza ndoto yake ya kujiunga na Fc Barcelona baada ya klabu hiyo kushindwa kwenye rufaa yake ya kupinga adhabu ya kuzuiwa kufanya usajili katika madirisha mawili yajayo ya usajili. Dortmund italazimika kumuuza nyota huyo ambaye ana kipengele kinachomruhusu kuondoka endapo timu yoyote itakuja na dau la euro milioni 25, kipengele ambacho kitaweza kutumika baada ya kumalizika kwa msimu huu. Reus ambaye inafahamika wazi kuwa ataondoka Dortmund msimu ujao aliwahi kuiahidi Barcelona kuwa atajiunga na klabu hiyo baada ya kumalizika kwa msimu huu lakini ahadi hiyo huenda ikashindwa kutimia kwani Barcelona wako chini ya adhabu ya Fifa ya kutosajili mchezaji yoyote kwa vipindi viwili vya usajili baada ya kukutwa na hatia ya kukiuka kanuni za usajili kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 18. Kitendo cha mahakama ya rufaa za michezo ya CAS iliyoko nchini Uswisi kuitupilia mbali rufaa ya Barcelona huenda kikaipa Real Madrid faida ya kuingia na kumsajili mchezaji huyo huku wakifahamu kuwa Barcelona hawataweza kuhusika kwenye usajili wake.