Vinara wa Ligi ya Uingereza Chelsea sasa wafikiwa kwa pointi na Manchester City
(GMT+08:00) 2015-01-02 09:48:45
Ligi kuu ya soka nchini England iliendelea jana kwa michezo kumi iliyosakatwa kwenye viwanja kadhaa nchini humo. Ukiachana na mchezo wa Manchester United uliofanyika mapema ambapo mashetani hao wekundu walishikwa shati na Stoke City kwa kutoka sare ya 1-1, mwanzo wa mwaka haukuwa mzuri kwa timu kubwa baada ya timu mbili za London ambazo ni Chelsea na Arsenal kufungwa kwenye michezo yake. Chelsea wakiwa wageni wa Tottenham Hotspurs huko White Hart Lane walipoteza mchezo wao kwa kufungwa 5-3 katika mchezo ambao ulijaa magoli tangu mwanzo. Mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania Diego Costa alikuwa wa kwanza kuifungia timu yake mapema kwenye dakika 18. Mabao mengine ya Chelsea yalifungwa na Eden Hazard na John Terry. Nayo Spurs ilifanya kufuru ya mwaka baadaya wachezaji wake kusawazisha bao la kwanza na kuendelea kumimina mvua ya magoli iliyosababisha mafuriko makubwa hapo kiwanjani. Walioitoa kidedea Spurs ni pamoja na Harry Kane, Danny Rose na winger Andros Townsend. Spurs walipata bao la nne kupitia kwa Harry Kane kabla ya kumalizia karamu kwa bao safi la Nacer Chadli. Mara ya mwisho kwa Chelsea kufungwa idadi kubwa ya mabao kwenye ligi kuu ya England ilikuwa mwaka 1991 ambapo walifungwa na Nottingham Forest 7-0. Arsenal wakiwa kwenye uwanja wa St Mary's walikubali kipigo cha 2-0 mbele ya Southampton huku mabao yote mawili yakifungwa kutokana na makosa ya kizembe ya kipa Wojciech Szczesny. Wafungaji wa Saints kwenye mchezo huo walikuwa Sadio Mane na Dusan Tadic. Katika michezo mingine Manchester City walishinda mchezo wao dhidi ya Sunderland kwa 3-2, Liverpool na Leicester City wakitoka sare ya 2-2 , Newcastle na Burnley nao walifunga 3-3 huku West Ham United na West Brom wakiendeleza mfululizo wa sare baada ya kufungana 1-1. Matokeo haya yamewafanya Chelsea kupunguzwa kasi baada ya Manchester City kuwafikia kwa kutimiza pointi 46 huku Southampton wakiwapumulia Manchester United baada ya kupunguza tofauti ya pointi moja tu baina ya timu hizo.