Makamu wa Rais wa shirikisho la soka duniani, Mwanamfalme Ali Bin Al Hussein wa Jordan, amesema kuwa atamenyana na Sepp Blatter kuwania urais wa shirikisho hilo katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Mei 29. Sepp Blatter anawania urais wa shirikisho hilo kwa muhula wa tano. Ali Bin Hussein, huenda akaungwa mkono na mashirikisho la soka Ulaya ingawa haijabainika kama shirikisho lenye nguvu sana la soka ya Bara Asia litakuwa mingoni mwao. Mwanamfalme huyo, amesema wakati umefika wa kubadilisha mambo katika shirikisho hilo hasa kutokana na kashfa nyingi ambazo zimeikumba soka duniani akimaanisha madai ya rushwa ambayo amehusishwa nayo, bwana Blatter na kutikisa uongozi wake wa shirikisho hilo kwa miaka 17 iliyopita. Naye Mwanadiplomasia wa zamani wa Ufaransa Jerome Champagne, pia ataendelea kuwania uongozi huo dhidi ya wawili hao. Champagne alitangaza nia yake Januari mwaka 2014 na sasa amemtaka mwanamfalme aeleze mipango yake. Hadi kufikia Januari 29 Wagombea wanapaswa wawe wameshaeleza malengo yao ya kuwania urais. Ali hivi sasa ni miongoni mwa makamu wa rais saba wanaofanya kazi chini ya Blatter.