Hali Barcelona yazidi kuwa tete, baadhi ya wachezaji kutaka kuihama
(GMT+08:00) 2015-01-07 14:12:16
Mabingwa wa zamani wa Hispania na Ulaya, FC Barcelona wako kwenye mgogoro mzito ambao unatishia kupotea kwa amani ndani ya klabu hiyo. Hali ndani ya Nou Camp imekuwa mbaya kufuatia matokeo mabaya ambayo klabu hiyo imeyapata hivi karibuni hasa kwenye mchezo wao wa kwanza kwa mwaka 2015 ambao walijikuta wakifungwa na vijana wa David Moyes, Real Sociedad. Makamu wa Rais wa Barcelona, Josep MarĂa Bartomeu amejikuta akiwa hana la kufanya kutatua mgogoro uliojitokeza hivi karibuni huku shinikizo juu yake kuwajibika likizidi kuongezeka siku hadi siku. Katika kipindi cha saa 24 zilizopita Barcelona imemfukuza kazi Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Andoni Zubizaretta huku dakika chache baada ya kufukuzwa kwake msaidizi wake kwenye nafasi hiyo, Carles Puyol naye akiamua kuachia ngazi. Zubizaretta amelaumiwa kwa kusajili wachezaji ambao wameshindwa kuonyesha kiwango cha juu hadi sasa akiwemo Luis Suarez. Matokeo mabaya yamefanya nafasi ya kocha Luis Enrique kuwa hatarini huku akipewa mechi mbili za kuhakikisha anashinda au kufukuzwa kazi. uongozi wa klabu hiyo unajuta kutokana na kutambua kuwa ulifanya makosa kumuajiri Luis Enrique ambaye ameonekana kukosa uzoefu wa kuwaongoza wachezaji nyota huku akilaumiwa kwa kitendo cha kuwaanzisha kwenye benchi nyota wawili wa timu hiyo Lionel Messi na Neymar. Mgogoro huo kwa sasa umezua tetesi nyingine kuhusiana na baadhi ya wachezaji ambao wanaweza kuihama klabu hiyo ambapo inadaiwa kuwa Hali ya Messi kutoelewana na kocha wake imepelekea kufikira kuihama Barcelona japo hakujawa na taarifa rasmi toka kwake au wawakilishi wake kuthibitisha habari hizi.