Kombe la Afcon latimua vumbi nchini Equatorial Guinea
(GMT+08:00) 2015-01-19 14:05:15
Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika ilianza rasmi Jumamosi kwa michezo miwili ya kundi A ikizihusisha timu mwenyeji Equatorial Guinea na Congo Brazzaville pamoja na mchezo mwingine kati ya Gabon na Burkina Faso. Katika mchezo wa kwanza Wenyeji Equatorial Guinea na Congo Brazzavile walitoka sare ya 1-1 katika mchezo uliokuwa mkali na wa kusisimua ambapo timu hizi zilishambuliana kwa karibu dakika zote za mchezo. Katika mechi nyingine ya Kundi A Gabon walianza kufunga kwenye dakika ya 19 mfungaji akiwa mshambuliaji na nahodha wa timu hiyo Pierre Emerrick Aubameyang. Katika kipindi cha pili Gabon waliongeza bao la pili kwenye dakika ya 72 lililofungwa na Malick Evouna. Matokeo haya yanamaanisha kuwa Gabon wanaongoza kundi A baada ya michezo ya kwanza wakiwa na pointi tatu huku Equatorial Guinea na Congo Brazzavil wakifuatia wakiwa na pointi moja kwa kila timu na Burkina Faso wanashika mkia wakiwa hawana pointi yoyote. Na katika mechi za jana Jumapili kwa upande wa kundi B uliowakutanisha Zambia na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo matokeo yalikuwa 1 – 1 huku mchezo kati ya Tunisia na Cape Verde matokeo pia yakiwa suluhu ya 1-1. Mechi nyingine za kundi C zitachezwa leo.