Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon imeendelea nchini Equatorial Guinea, ambapo timu za kundi C zilipambana kusaka pointi tatu muhimu katika kuendelea na kinyang'anyiro cha taji la michuano hiyo. Timu ya Algeria, walionyesha ubora wao katika kusakata kabumbu, pale walipowachakaza Afrika Kusini mabao 3-1. Afrika Kusini ndiyo iliyoanza kuliona lango la Algeria katika dakika ya 51 likifungwa na Phala. Algeria ilisawazisha bao hilo kwa mpira aliojifunga Thulani Hlatshwayo katika dakika ya 67, huku Ghoulam na Sliman wakifunga katika dakika ya 72 na 83. Na katika mchezo wa mwanzo, ulizikutanisha timu za Ghana na Senegal, ambapo Senegal iliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Ghana ilikuwa ya kwanza kuona lango la Senegal kwa mkwaju wa penalti uliofungwa na Andre Ayew dakika ya 14. Hadi mapumziko Ghana ilikuwa mbele kwa bao hilo. Senegal ilibadilika na kuweza kusawazisha dakika ya 58 kupitia mchezaji wake Mame Diouf. Mpambano huo ukionekana kumalizika kwa sare ya 1-1, mchezaji Sow alibadili matokeo kwa kufunga bao katika dakika ya 90 na kuiwezesha Senegal kuibuka mshindi wa mechi hiyo. Katika kundi C, Algeria na Senegal zina pointi tatu kila moja, huku Ghana na Afrika Kusini zikibakia bila pointi. Leo ni mpambano kwa kundi D lenye timu za Ivory Coast, Mali, Cameroon na Guinea.