Eto'o huenda akatimuliwa na Sampdoria iliyomsaini wiki moja iliyopita
(GMT+08:00) 2015-02-05 14:35:46
Ikiwa imepita wiki moja tu tangu asajiliwe na klabu ya Italia ya Sampdoria, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Cameroon Samuel Eto'o ameripotiwa kutaka kutimuliwa klabuni hapo baada ya kutoelewana na kocha wake. Eto'o aliingia matatizoni na kocha Sinisa Mihaijlovic baada ya kocha huyo kumtaka afanye mazoezi ya ziada kufuatia mchezo ambao Sampdoria ilifungwa 5-1 na timu ya Torino katika muendelezo wa ligi ya Italia maarufu kama Serie A. Kwenye mechi hiyo Eto'o aliichezea klabu yake mpya kwa mara ya kwanza baada ya kuingia akitokea benchi kwenye dakika ya 71 japo uwepo wake haukuweza kuiokoa timu yake. Eto'o na kocha wake walifanya kikao cha dharura kuzungumzia. Inasemekana kuwa uhusiano kati ya Eto'o na kocha wake umefikia hatua mbaya kiasi cha klabu hiyo kuwa na wazo la kuvunja mkataba wake wa miaka miwili baada ya kusaini ndani ya wiki moja tu akitokea Everton. Viongozi wa klabu hiyo ya Sampdoria wamekataa kuzungumzia tukio hilo wakisisitiza kuwa eto'o alikosa mazoezi kwa sababu zake binafasi lakini kocha anasema 'Klub ndio itajua nini cha kufanya ila kwake yeye mchezaji anapofanya kitu kama hiki ni sawa na kumkosea heshima na kumdharau yeye na wafanyakazi wengine.