Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana katika mataifa mengi ya bara Afrika sio jambo geni, na wengi wao hupitia wakati mgumu ili kuweza kujikimu kila siku. Nchini Kenya katika muda wa chini ya miaka 10, kuna kijana aliweza kujiendeleza kutoka kuwa ombaomba na sasa anaendesha biashara kubwa.
Kijana Joel Muroki kwa sasa ni moja kati ya wafanyabiashara wazuru katika mji wa Isinya katika kaunti ya Kajiado. Kijana huyo anasema baada ya kuondoka nyumbani kwao kutokana na kukosa karo ya shule, aliwaaga wazazi wake kuwa anakwenda kutafuta ajira Nairobi. Lakini huko maisha yalikuwa magumu, na akajikuta anakuwa ombaomba. Kijana huyo anasema anakumbuka hata kuna wakati alilazimika kulala bila hata kula.
Lakini baadaye alianza kazi ya kung'arisha viatu, aliyofanya kwa muda wa miaka kadhaa na kuweka akiba ya kutosha na kufungua duka ndogo, lakini alilazimika kulifunga muda mfupi baada ya kusumbuliwa na maofisa wa mamlaka ya jiji, na kuajiriwa kwenye duka lingine la jumla. Baada ya hapo ndipo alihamia katika mji wa Isinya na kufungua kioski kidogo.
Hata hivyo kazi hii pia ilikumbwa na changamoto. Baada ya miaka miwili kisoski chake kilivamiwa na wezi na kuibiwa karibu kila kitu. Hata hivyo alijitahidi na kuweza kujaza tena kioski chake na kuendelea na biashara.
Bw James Majira ni mmoja wa wafanyakazi walioanza kazi na Bw Muroki na anaeleza kuwa ameona biashara hiyo ikikua na kufikia ilipo, duka hili lilianza kwenye kibanda kidogo, baadaye walihamia kwenye nyumba nyingine, na wana duka kubwa zaidi, na wanaweza kufungua tawi lingine ambalo pia ni kubwa zaidi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |