Andre Ayew aendelea kuwaziba midomo Waghana kwa kujitahidi kufanya vizuri
(GMT+08:00) 2015-02-10 15:34:46
Nyota wa Ghana, Andre Ayew ana kibarua kipevu cha kufuta hisia za Waghana wengi kwamba amepata nafasi ya kucheza timu ya taifa ya nchi hiyo kwa sababu tu ya baba yake mzazi, Abedi 'Pele' Ayew. Wakati alipocheza fainali za kwanza za Afcon mwaka 2008, mashabiki wengi wa soka nchini Ghana waliponda uteuzi wake kwenye kikosi wakisema ulifanyika kwa sababu tu ya umaarufu wa baba yake. Hata hivyo, Andre Ayew aliwaziba midomo mashabiki hao kwa kuisaidia Ghana ilipobeba ubingwa wa Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2009, na pia alikuwa kwenye kikosi kilichofika fainali ya Afcon 2010 katika fainali zilizofanyika Angola. Andre mwenye umri wa miaka 25, anayecheza kikosi cha Marseille, pia amecheza fainali mbili za Kombe la Dunia kitu ambacho baba yake mzazi hajawahi kukifanya, huku juzi Jumapili akiibeba Ghana kwenye fainali ya Afcon dhidi ya Ivory Coast, ingawa ushindi ukaenda kwa Ivory Coast. Kwenye fainali hizo za Guinea ya Ikweta, Andrew ameng'ara na kufunga mabao matatu ikiwamo ya ushindi dhidi ya Afrika Kusini pia alifunga kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Guinea ya Ikweta katika nusu fainali.