Hicham el Amrani apongeza michuano ya Guinea ya Ikweta
(GMT+08:00) 2015-02-11 14:06:31
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu, barani Afrika, Hicham el Amrani amesifu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Equatorial Guinea. Amesema licha ya ghasia na huduma duni, yalikuwa mashindano yenye mafanikio. Amesisitiza kuwa wanafuraha juu ya maandalizi yote kwa ujumla, kwa muda waliokuwa nao na raslimali walizokuwa nazo, na kusema waliweza kuwa na michuano ambayo imemalizika vizuri. Hata hivyo, mashindano hayo yaliyomalizika Jumapili kwa Ivory Coast kuishinda Ghana kwa mikwaju ya penalti baada ya kutofungana dakika 120 za mchezo na kunyakua kombe, yatakumbukwa kuwa mashindano yenye utata na magumu. Na miongoni mwa utatahuo ni pamoja na penalti iliyopewa Equatorial Guinea dhidi ya Tunisia katika hatua ya robo fainali, ambapo wachezaji wa Tunisia walitakiwa kujizuia na ghasia walipomkimbiza mwamuzi wa mchezo huo Rajindraparsad Seechurn mwishoni mwa mchezo.