Kibarua cha Gus Poyet chaota mbawa baada ya Sunderland kufanya vibaya
(GMT+08:00) 2015-03-17 14:07:17
Klabu ya ligi kuu ya Uingereza Sunderland imemtimua kocha Gus Poyet kufuatia kuwa na mfulululizo wa matokeo mabaya. Sunderland imeshinda mara moja tu kati ya mechi 12 za ligi kuu nchini Uingereza. The Black Cats wamesalia nje tu ya eneo la hatari ya kushushwa daraja hasa baada ya kuambulia kichapo cha mabao 4-0 siku ya Jumamosi walipovaana na Aston Villa. Mwenyekiti wa klabu hiyo Ellis Short amesema kwa sasa wanahitaji mabadiliko ili kuinusuru klabu yao. Hivyo klabu ya Sunderland imetoa taarifa ikisema kuwa meneja atakayemrithi Poyet atatangazwa karibuni. Hali sasa ni tete kwao wakijiandaa kuchuana dhidi ya West Ham bila ya mkufunzi siku ya Jumamosi. Aidha Sunderland itakabiliana na Newcastle Aprili 5. Poyet mwenye miaka 47, alifahamishwa hatima yake baada ya mazoezi ya siku ya Jumatatu na mkurugenzi mtendaji wa klabu hiyo Margaret Byrne. Raia huyo wa Uruguay alishika hatamu Sunderland baada ya Paolo Di Canio kuondoka mwezi Oktoba 2013.