• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Athari zinazotokana na bidhaa bandia

    (GMT+08:00) 2015-03-19 15:26:49
    A Wasikilizaji wapendwa, karibuni katika kipindi cha uchumi na maendeleo, mimi ni Carolin Nassoro na mwenzangu ni Fadhili Mpunji. Tarehe 15 mwezi Machi ni siku ya kimataifa ya haki na maslahi ya wateja. Nchini China kila ifikapo siku hiyo, televisheni ya taifa CCTV inatangaza kipindi maalumu ambacho kinataja orodha ya kampuni zilizovunja haki na maslahi ya wateja na vitendo vya biashara vinavyowadanganya wateja.

    B. Ndiyo. Kipindi hiki kinafuatiliwa sana na wachina. Mbali na juhudi za vyombo vya habari, katika kulinda haki na maslahi ya wateja, pia zipo hatua mbalimbali, kama vile inaweza kuunda shirika la kulinda haki na maslahi ya wateja, na serikali kutunga sharia husika. Lakini, Carol, naona kuwa licha ya hatua zilizochukuliwa na serikali, wateja pia wanalazimika kujenga wazo sahihi wa ununuzi.

    A. Nakubaliana na wewe. Unajua kwenye maisha ya kawaida, watu hutaka kununua bidhaa zenye bei nzuri, hata kama wanajua bidhaa hizo si za halisi, bado tu watazinunua, mtazamo ambao umewapa fursa wafanyabiashara wanaouza bidhaa za bandia. Mwandishi wetu wa habari hivi karibuni alifanya mahojiano na wateja kuhusu ununzi wa bidhaa ghushi. Tumsikilize.

    "Je, uliwahi kununua bidhaa bandia?"

    "Ndiyo. Nilinunua viatu vya chapa ya Nike, lakini ni bandia, viliharibika baada ya wiki moja."

    "Kabla ya kuvinunua, ulifahamu kuwa ni chapa bandia?"

    "Ndiyo, nilijua. Lakini bei yake ilikuwa nzuri"

    "Baadaye utaendelea kununua chapa bandia?"

    "Hapana. Ingawa bei ni nzuri, lakini sifa ni mbaya sana."

    Sauti 2

    "Je, Uliwahi kununua bidhaa bandia?"

    "Ndiyo. Nilinunulia mwanangu mdoli wa chapa ya Hasbro kwenye duka la mtandao wa Internet. Mfanyabiashara alisema chapa hiyo ni halali, lakini baada ya kuupata, niliunusa na ulikuwa na harufu mbaya. Nilikwenda duka lililoko kwenye shopping mall, na karani wa duka hilo aliniambia mdoli huo ni bandia."

    "Utaendelea kununua vitu kwenye maduka ya mtandao wa Internet?"

    "Ndiyo. Lakini nitaangalia kwa makini, sasa sina imani na maduka kwenye Internet."

    A. Baada ya kusikiliza mahojiano hayo, naona bidhaa bandia ziko karibu sana na maisha yetu. Kwa kweli hata mimi pia niliwahi kununua bidhaa bandia kwenye mtandao wa Internet kutokana tu na bei nzuri. Bila shaka sifa zao kweli si nzuri. Naona ununuzi wa bidhaa bandia una athari mbaya kwetu kwa upande za fedha na moyo. Licha ya hasara ya pesa, wateja husikitika sana baada ya kununua bidhaa bandia.

    B. Ndio maana kwenye kipindi hiki tunazungumzia athari zilizoletwa na bidhaa bandia. Kama wateja wakitambua vema athari hizo, hawatanunua tena bidhaa bandia. Kwa kweli naona wateja hao walikuwa na bahati nzuri, kwani walinunua viatu na midoli, wala si pombe bandia,dawa bandia na vyakula vingine vyenye sumu, ambavyo vitatishia maisha ya watu.

    A. Haswa. Pombe bandia, sigara bandia, dawa bandia, mbolea bandia, chapa bandia, Bidhaa bandia zimeathiri vibaya ujenzi wa uchumi na usalama wa fedha na maisha ya watu. Hebu sasa tuzungumzie athari mbaya za bidhaa hizo.

    B. Kwanza, bila shaka bidhaa bandia zinatishia afya na usalama wa maisha ya watu. Kama ulivyosema, pombe bandia, dawa bandia na vifaa vya mashine vyenye ubora mbaya, vitatishia maisha ya wateja. Kuna tukio moja lilitokea mwaka 2003, maziwa ya unga ya watoto yenya sumu yaliuzwa mjini Fuyang, Anhui, nchini China lilifuatiliwa sana na wachina. Watoto wengi walikufa au kupata ulemavu kutokana na kunywa maziwa hayo. Tukio hilo pia liliathiri uuzaji wa maziwa ya unga ya chapa nyingine hapa China.

    A. Unajua wakati bidhaa bandia zinapokiuka maslahi ya wateja, pia zinapunguza uaminifu kwenye soko. Kwa mfano, mwezi Januari mwaka 2013,Uingereza na Ireland zimegundua wafanyabiashara wametumia nyama wa farasi badala nyama wa ng'ombe na kuwadanganya wateja, takwimu zilizotolewa na televisheni ya Sky nchini Uingereza zinaonesha kuwa, asilimia 20 ya wateja walisema watabadilisha desturi ya matumizi, na hawatanunua vyakula vilivyotengenezwa na nyama. Bidhaa bandia zinawafanya wateja wapunguze imani kwa bidhaa za chapa maarufu. Ni rahisi sana kuvunja uaminifu wa soko, lakini ni vigumu sana kurudisha uaminifu huo.

    B. Wateja wanakosa imani kwa chapa nyingine, na hii ni athari ya bidhaa bandia kwa sifa za chapa maarufu. Watengenezaji wa bidhaa bandia hupenda kutengeneza bidhaa za chapa maarufu, au bidhaa zinazopendwa na wateja,. Baadhi ya wafanyabiashara waliweka chapa maarufu kwenye bidhaa bandia, hivyo kuwafanya wateja wapunguze imani kwa bidhaa za chapa maarufu,hali hii itatishia maendeleo ya viwanda vinavyotengeneza bidhaa za chapa maarufu.

    A. Sasa licha ya hatua za idara husika za serikali kuhusu kupinga bidhaa bandia na kulinda maslahi ya wateja, sisi wateja tunapaswa kutambua vema athari mbaya zinazotokana na bidhaa bandia kwa taifa, kampuni na wateja binafsi. Kama hatutanunua bidhaa bandia, uwepo wa bidhaa hizo utapungua na hata kufutika kabisa.

    B. Si China pekee inayokabiliana na uwepo wa bidhaa bandia, nchi nyingine hasa barani Afrika pia zinaathiriwa na bidhaa bandia. Kiwango cha biashara ya bidhaa bandia nchini Kenya kinaendelea kuongezeka kwa kasi ya kutia hofu kila mwaka.Hali hii sasa imewakera wafanyibiashara wanaouza bidhaa halisi kutokana na hasara kubwa wanayopata kwa kupungua kwa kipato pamoja na kupoteza wateja wao. Mwadishi wetu Ahmed Bahajj kutoka Nairobi anatuarifu zaidi.

    Tatizo hili sugu hata hivyo linashuhudiwa katika nchi nyingi duniani na wala sio Kenya pekee. Uzalishaji wa bidhaa feki ni biashara haramu na uhalifu wa kimataifa wa thamani ya mabilioni ya pesa. Katika bishara hii China imetajwa kuhusika pakuwba japo pia inafanyika katika nchi nyingine duniani. Utafiti wa Radio China Kimataifa jijini Nairobi umedhihirisha kuwa wafanyibiashara wengi hununua bidhaa zao halisi kutoka China. Baadhi yao kama vile Gloria Mulimo anayeuza bidhaa halisi za elektroniki kutoka China anasema wanapenda kununua bidhaa za China kwani zinawapa faida kubwa na wateja wanazipenda kutokana na ubora wake.

    "sisi tunauza Computer na vifaa vyake vya matumizi kama charger za simu. Tunauza vitu halisi, tunapenda kuuza bidhaa za china kwa sababu wao ndio wana ujuzi wa hali ya juu wa kutenengeza bidhaa za elektroniki."

    Gloria anasisitiza kwamba licha ya bidhaa bandia kuenea katika maduka mengi jijini Nairobi, biashara yao haiathiriki kwa kiasi kikubwa kwani wateja wanajua kutofautisha ubora.

    "sisi haituathiri sana kwani wanaelewa ubora hawawezi kwenda kununua bidhaa bandia, hata wakiuziwa wanarudi hapa hapa kutafuta bidhaa halisi"

    Kwa upande wa Jane Karanja pia aneuza bidhaa za China, maoni yake yanafanana na Gloria lakini analalama kwamba, wanapata kazi ngumu ya kuwafahamisha wateja jinsi ya kutofautisha bidhaa halisi na feki. Anasema wateja kutoka sehemu za vijijini hawawezi kutofautisha.

    "Tunauza bidhaa halisi za mawasiliano kutoka China, wateja wanapenda bidhaa zetu halisi za China, shida ni kwamba wateja sasa wanasema wanapata bidhaa kwa bei rahisi kwa maduka mengine. Wateja wanapenda bidhaa zetu na tunajitahidi kuwafahimisha lakini inakuwa vigumu wakati mwengine kwa sababu wanapenda bei ya chini."

    Aidha Jane ameitaka serikali ya Kenya kupiga marufuku uingizaji wa bidhaa hizo kwani zinapunguza mapato yao na pia hazidumu kutokana na ukosefu wa ubora.

    "Tunataka zifungwe ziachwe kuuzwa nchini Kenya,kwa maana mwaka 2010 wateja walikuwa wengi lakini sasa wananunua bidhaa bandia, mimi ningemueleza mteja awe makini kabla ya kununua bidhaa, afanye utafiti kwanza ama atauziwa bidhaa mbaya"

    Mubaraka Mohamed anauza simu aina ya Techno na Huawei kutoka China, bidhaa zake ni halisi. Mubaraka anaeleza kwamba tofauti ya bidhaa zao halisi na za bandia ni waranti. Wao wanawahakikishia wateja wao uhalisi wa bidhaa. Wanatoa waranti na kubadilisha bidhaa kwa mteja iwapo itakuwa na matatizo kulingana na wakati iliyotolewa na watengenezaji wa simu hizo. Mohamed anasema bidhaa za China ndio bidhaa bora zaidi duniani lakini wafanyibiashara feki wanachangia kuharibu sifa ya bidhaa hizo.

    "Sisi tunauza simu za Techno, simu zetu ni halisi tunauza kwa bei ghali kiasi, wao wanauza bei rahisi sana. Wateja wanakimbilia kununua simu bandia lakini kesho zinaharibika wanarudi hapa kwetu. Wao hawana waranti. Simu zetu zimesajiliwa na kampuni kuu. Bidhaa hizi za China zinapendwa sana Afrika mashariki."

    Sharmake Abdukadir anatoa maelezo muhimu kwa mteja kununua bidhaa halisi.

    "Sisi tunauza bidhaa zetu China na pia tunanunua bidhaa kutoka huko. Biashara ya bidhaa bandia ni mbaya sana. Mteja anaponunua bidhaa halisi hapati shida yoyote, unaweza kutumia zaidi ya mwaka mmoja. Mteja anaridhika na matumizi na wengi wanapenda bidhaa bora, nawasihi wateja wanunue bidhaa nzuri wasipate matatizo"

    Hata hivyo wafanyibiashara wa bidhaa bandia wanajitetea kwa kusema kwamba, wateja wanazipenda na hawaoni kama zina matatizo yoyote. Maoni yao ni kuwa, wanatoa fursa kwa wateja wasioweza kugharamia bidhaa halisi kupata fursa ya kutumia bidhaa mbadala. Hali hii imeungwa mkono na baadhi ya wateja wanaopenda kununua na kutumia bidhaa bandia, wanasema zinawasaidia wasiokuwa na fedha. Bidhaa za kughushi zinapatikana katika sekta tofauti kama vyakula, elektoniki, nguo na hata dawa. Wafanyibishara wa bidhaa hizi huwahadaa wateja kwa kuwauizia bidhaa hizo kwa bei rahisi sana. Licha ya kuuza bidhaa bandia, wafanyabiashara hao wana soko zuri na hupata faida kubwa kutokana na ukosefu wa ufahamu wa wateja na pia ukosefu wa fedha za kutosha kununua bidhaa halisi.

    Shirika la Kimataifa la Forodha limeripoti kuwa, bidhaa bandia husafirishwa kwa zaidi ya nchi 140 duniani. Kenya hupata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 35 kila mwaka kutokana na biashara ya bidhaa bandia. China imehusishwa sana na bidhaa hizi bandia japo biashara hii inafanyika katika nchi nyingi duniani na China ni mwenzi mkubwa wa biashara halisi wa Kenya wala sio za bandia. Mwaka huu China itaandaa kongamano la kimataifa la mauzo ya bidhaa halisi za China jijini Nairobi. Kongamano hilo litajumuisha zaidi ya wawekezaji mia 3 wa China na lengo kuu ni mijadala kuhusu biashara ya China na Afrika. Wafanyinbiashara wa Kenya wana imani kuwa kongamano hili litajaboresha ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako