• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sikukuu ya Qingming nchini China

    (GMT+08:00) 2015-04-07 10:24:14

     Siku ya Qingming ni siku ya jadi kwa Wachina kukaribisha majira ya mchipuko na kufanya matambiko kwa marehemu, na kwa mujibu wa mwenendo wa jua, siku hiyo huwa kati ya tarehe 4, 5, na 6 April, mwaka huu siku hiyo ni tarehe 5. Katika kalenda ya kilimo ya China, Qingming ni siku ya kuanza kwa kipindi kimoja kati ya vipindi 24 vya mabadiliko ya hali ya hewa katika mwaka mzima, maana yake ni "kipindi kiangavu". Kutokana na utamaduni wa jadi, siku hiyo Wachina wanasafisha makaburi, mila ambayo imedumu kwa miaka 2500 hivi.


    Kuna aina niyingi za mazishi nchini China, kama vile kuzika, kuchoma maiti na kuzika majivu, na kumwaga majivu baharini. Mazishi ya kuzika yalitumiwa sana na wachina katika historia. Katika enzi ya kikabaila, mazishi hayo yalionesha tofauti ya matabaka. Lakini mazishi ya aina hiyo yalitumia eneo kubwa la mashamba, hivyo mazishi ya kuzika majivu yanachaguliwa zaidi na wachina.

    Mazishi ya kuchoma maiti na kuzika majivu pia yana historia ndefu. Katika miaka 1,500 hivi iliyopita, wachina walianza kufanya mazishi hayo. Kuenea kwa mazishi hayo kulitokana na kusambaa kwa dini ya Buddha. Kwa sababu Buddha Sakyamuni alipofariki alichagua mwili wake uchomwe, hivyo mazishi hayo yalijulikana na duniani, na waumini wa dini ya Buddha walianza kuiga mfano wa Buddha Sakyamuni. Kuanzia karne 20, kufuatia upungufu wa eneo la mashamba duniani, nchi mbalimbali zilianza kuhimiza mazishi ya kuchoma maiti ili kuhifadhi mashamba, na serikali ya China ilianza kuwahimiza wananchi wake kuchagua njia hiyo ya mazishi.

    Lakini kutokana na idadi kubwa ya watu nchini China, mazishi ya kuzika majivu pia yanatumia eneo kubwa la ardhi. Ili kutatua suala hilo, miaka ya hivi karibuni, mazishi ya mtindo mpya yameibuka katika jamii ya China. Aina hiyo mpya ya mazishi ni kuchoma maiti na kuzika majivu chini ya miti, maua na majani au kumwaga majivu baharini. Mazishi hayo pia yanaitwa mazishi ya kijani, kwa sababu rangi ya kijani inaashiria moyo wa marehemu utadumu milele.

    Siku ya Qingming inakaribia, wachina wengi wanakwenda kusafisha makaburi. Suala la kupanda kwa bei ya ardhi kwa ajili ya makaburi linafuatiliwa tena na watu. Kwa upande mmoja, watu wanalalamikia gharamu kubwa ya mazishi ya kuzika, kwa upande mwingine mazishi ya mtindo mpya yanayopunguza gharama na kuweza kuhifadhi mazingira hayajapokelewa vizuri na watu kutokana na msimamo wa jadi kuhusu mazishi.

    Kutokana na utamaduni wa jadi wa China, mazishi ya kuzika yanahitaji kununua eneo la kuzikia. Lakini bei ya juu ya maeneo hayo inaleta shinikizo kubwa kwa watu wengi. Mkazi wa Beijing Bibi Zhang anasema,

    "Hatuna la kufanya, sisi ni wafanyakazi wa kawaida. Kununua eneo la kuzikia ni jambo la kifahari. "

    Mkazi Bw. Zhang anasema,

    "Baadhi ya mazishi yanafanywa kwa kifahari kupita kiasi, ambayo yanaleta shinikizo kubwa kutokana na wazo la kushindana na wengine."

    Nchini China, Watu wengi wanaendelea kuchagua mazishi ya kuzika, mazishi ya mtindo wa kisasa hayajapokelewa na watu. Kwa mfano, mwaka 2012 kati ya mazishi laki 7.22 yaliyofanywa hapa Beijing, idadi isiyozidi asilimia 10 ilikuwa ya mtindo wa kisasa, kama vile mazishi ya kumwaga majivu baharini, na kuzika majivu chini ya miti na maua.

    Mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi ya idara ya mambo ya umma ya Beijing Wang Qi anasema,

    "Mazishi ya kisasa yanayokalia ardhi ndogo au kutokalia ardhi ni mwelekeo mkuu wa mageuzi ya mazishi yanayoelekezwa na wizara ya mambo ya umma ya China. Kuna aina mbalimbali za mazishi ya kisasa, kama vile mazishi ya kumwaga majivu baharini, kuzika majivu chini ya miti, majani na maua. Natumai kutokana na juhudi zetu, kiwango wa mazishi ya kisasa kitaongezeka hadi kufikia asilimia 30 hadi 35, ili kupunguza matumizi makubwa ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa makaburi."

    Katika kutangaza aina mpya ya mazishi, idara za mambo ya umma za sehemu mbalimbali zimetekeleza sera za kutoa ruzuku. Mwaka 2012, mkoa wa Liaoning kaskazini mashariki mwa China, ulianza kutoa ruzuku kwa mazishi ya kumwaga majivu baharini. Serikali ya mkoa huo inalipia huduma kwa mashirika ya kufanya mazishi, na mashirika hayo yanatoa huduma ya mazishi bure. Aidha, kuanzia mwaka 2009 serikali ya Beijing pia ilianza kutoa huduma bure kwa wale wanaofanya mazishi ya kumwaga majivu baharini.

    Mkazi wa Beijing Bibi Feng anasema, anakubali mazishi ya kumwaga majivu baharini.

    "Majivu yatarudi katika mzingira ya kimaubile, naona ni mtindo mzuri."

    Sasa Tunageukia mkoa wa Yunnan ulioko kusini mwa China. Hali ya hewa ya mkoa huo ni ya fufutende, na mazingira yake yanafaa kupanda maua. Hivyo watu wa huko wanaanza kufanya mazishi ya maua, ambapoo mwili wa marehemu unachomwa na majivu yake yanazikwa ardhini na kisha juu yake yanapandwa maua. Meneja wa Kampuni moja ya Mazishi ya Yunnan Bw. Li Jianren anasema,

    "Mazishi ya maua ni mtindo mpya. Uzuri wake ni kupunguza matumizi ya ardhi na kutoharibu mazingira ya kiasili. Mazishi ya maua ni kuzika majivu chini ya ardhi, na juu yake unapanda maua, hivyo inaonekana kama bustani ya maua."

    Licha ya kuhifadhi mazingira, kubana matumizi ya fedha ya mazishi pia kunavutia. Bw. Li anasema,

    "Gharama ya mazishi hayo mapya ni chini, ambayo ni kama asilimia 10 hadi 16.7 ya mazishi ya kawaida."

    Ingawa mazishi ya maua yana mambo mengi ya kuvutia, lakini sio watu wote wanaokubali mazishi hayo. Bibi Wang anayefanya kazi katika idara ya wafanyakazi waliostaafu mkoani Yunnan anasema, anawasiliana na wazee wengi, kwa maoni ya wazee, hawapendi mazishi hayo.

    "Kwa sababu nashughulikia mambo ya wazee wanaostaafu, hivyo nawasiliana sana nao, naona si rahisi kuwafahamisha aina hii ya mazishi. Wazee wanafikiri kuwa baada ya kuaga dunia watazikwa kwenye makaburi ambako watoto wao wanaweza kufanya matambiko. Lakini kama akifanyiwa mazishi ya maua, wazee wanaona hawatakuwa na kaburi. Hivyo wana wasiwasi na kutokubali mazishi hayo."

    Lakini wapo watu wanaounga mkono mazishi ya maua, Bibi Li ni mmojawao, anasema,

    "Kwangu mimi naweza kukubali mazishi hayo, kwa sababu ardhi ni maliasili isiyotumiwa tena. Haifai kwa ujenzi wa makaburi kutumia ardhi kubwa, tena hausaidii uhifadhi wa mazingira, na gharama ni kubwa. Sisi hatuna haja ya kuwapatia watoto wetu shinikizo kubwa."

    Bw. Li anasema, mazishi ya maua yanaonesha kuwa msimamo wa kijadi wa China kuhusu mazishi uko katika mchakato wa mabadiliko, na idadi ya watu wanaokubali mazishi hayo inaongezeka mwaka hadi mwaka.

    "Kwa mujibu wa desturi ya jadi ya China, mazishi ya kawaida yanahitaji tofali lenye jina la marehemu linalowekwa mbele ya kaburi, lakini mazishi ya maua hayana tofali hilo, hivyo hilo ni badiliko kubwa kwa desturi ya jadi. Naona watu wanaopokea mazishi ya maua wanaongezeka mwaka hadi mwaka. Hivi sasa kuna asilimia 10 hadi 15 ya wakazi wanaokubali mazishi hayo. Naona hii ina uhusiano na ustaarabu wa jamii, maendeleo ya miji, mabadiliko ya mawazo ya watu. Mji ukiendelea zaidi, watu watapokea zaidi aina hii mpya ya mazishi"

    Inapokaribia siku ya Qingming, wachina wengi wanaenda kusafisha makaburi, ili kuonesha heshima kwa marehemu. Katika miaka ya hivi karibuni, huduma mpya ya kuwakilisha wateja kusafisha makaburi imeibuka nchini China.

    Katika sikukuu ya Qingming, kusafisha kaburi kunadhiniwa kama kitendo maalumu kwa jamaa wa marehemu. Lakini kutokana na umbali, msongamano wa watu na magari katika maeneo ya makaburi, huduma ya kuwakilisha wateja kusafisha makaburi imeibuka.

    Katika Taobao.com ambayo ni tovuti kubwa zaidi ya biashara nchini China, kuna maduka zaidi ya 20 yanayotoa huduma ya kuwakilisha wateja kusafisha. Yang Xuan ni msichana anayefanya kazi mbali kutoka maskani yake, anasema anapenda huduma hiyo.

    "Kama kaburi liko karibu mahali unakoishi, na una muda wa kusafisha kaburi, ni nzuri. Lakini siku hizi, kufanya kazi na kusoma katika mji mwingine au nje ya nchi ni jambo la kawaida. Umbali ni kikwazo. Kama huwezi kurudi, na unataka kuonesha huduma kwa marehemu, huduma hiyo itakuwa chaguo zuri sana."

    Lakini Dada Yang pia anasema, watu hawawezi kutegemea huduma hiyo. Kama unaweza kurudi nyumbani, unatakiwa kurudi nyumbani. Kwa sababu kila mwaka una sikukuu moja ya Qingming. Jing Xiao Wei ni mkazi wa Beijing, anasema,

    "Kwangu mimi, siku ya Qingming ni shughuli ya makini kwa kufanya matambiko kwa jamaa walioaga dunia. Kama unawataka watu wengine usiowafahamu kufanya jambo hilo, kama vile shirika la kuwakilisha kusafisha kaburi, sidhani ni nzuri. Kitendo hicho hakina uhusiano na hisia zako. Kwa hiyo, kama kila mmoja anachagua huduma hiyo, maana ya kusafisha kaburi ni nini?"

    Huduma hiyo pia inaleta wasiwasi kuhusu kuifanya siku ya Qingming kuwa fursa ya biashara.

    Profesa wa Taasisi ya Sayansi ya Kijamii ya China Yu Jianrong anasema, inaeleweka kuwataka wengine kusaidia kusafisha makaburi. Lakini wakati watu wanapopata faida kutoka kwa sikukuu, biashara inaifanya sikukuu ipotee maana yake. Asili ya kusafisha makaburi ni kuonesha heshima kwa marehemu. Asili hiyo itapotea wakati watu wanaanza kutafuta faida.

    Mpaka sasa, huduma ya kuwakilisha kusafisha makaburi zinazotolewa na maduka kwenye mtando wa Internet inawavutia wateja wachache tu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako