Louis van Gaal atamba kwamba sasa Manchester City imeanza kuigopa Manchester United
(GMT+08:00) 2015-04-09 16:33:05
Kocha Mkuu wa Manchester United, Louis van Gaal ametamba kwamba kupanda kiwango kwa kikosi chake kumeanza kuwatia presha mahasimu wao, Manchester City katika mbio zao za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England. Manchester United itakuwa nyumbani Old Trafford Jumapili hii kumenyana na Man City katika mchezo wa Manchester 'derby', vita inayotajwa kuwa kali kutokana na timu zote kusaka nafasi ya pili ili kuifukuzia Chelsea kileleni kwenye msimamo. Kocha Van Gaal ameiongoza Man United kushinda mechi tano zilizopita kwenye ligi na kupanda kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi ikishika nafasi ya tatu kabla ya mchezo wa Jumatatu usiku kati ya Man City na Crystal Palace. Mdachi huyo alisema mastaa wake kwa sasa wanajiamini na wataendelea kutumia mbinu walizotumia katika kuzichapa Liverpool na Tottenham wakati watakapokipiga na Man City. Mchezo wa raundi ya kwanza kwenye Ligi Kuu uliofanyika Etihad baina ya timu hizo, Man United ilikubali kichapo cha bao 1- 0, straika Sergio Aguero akiwatesa wababe hao wa Old Trafford.