Katika hali isiyotarajiwa bondia raia wa Marekani Floyd Mayweather ameamua kufanya mazoezi ya wazi na kuruhusu vyombo vya habari kuchukua picha ikiwa ni maandalizi kuelekea katika pambano lake dhidi ya bondia Manny Pacquiao raia wa Philippine. Mayweather ambaye ni bingwa wa WBA na WBC, ameweka rekodi ya kucheza mapambano 47 ya kulipwa bila kupoteza hata moja wakati mpinzani wake amepigana mapambano 57, akiwa amepigwa mara tano na kutoka sare mara mbili.
Pambano kati ya wawili hao linatarajiwa kufanyika Mei 2 mwaka huu, huku pigano hilo likitajwa kuwa ndio la pesa nyingi zaidi katika historia ya ngumi duniani. Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne Las Vegas Mayweather amesema hana wasiwasi wa kuharibu rikodi yake ya kutoshindwa. Amesema yeye ni bondia bora na Pacquiao pia ni bondia bora kwa hiyo pambano hilo litaleta msisimko mkubwa. Pambano hilo sio tu litakuwa pambano litakaloingiza pesa nyingi lakini pia litaamua nani bondia wa enzi hii. Wakati huohuo kwa mujibu wa taarifa kutoka jarida la Forbes la nchini Marekani Mayweather atatumia kifaa cha kulinda meno chenye gharama ya dola za kimarekani elfu ishirini na tano.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |