Walcott akubali kuketi na Arsenal kuzungumzia hatima yake
(GMT+08:00) 2015-04-17 14:17:02
Hatimaye nyota Theo Walcott amekubali kuketi kuzungumzia hatima yake na kikosi cha Arsenal, na miamba hiyo imepanga kumpa mkataba mpya ili kumzuia asiende Liverpool. Walcott amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa ambapo anaingiza Pauni 90,000 kwa wiki na baada ya kugoma kusaini mkataba mpya, Liverpool ilionyesha nia ya kutaka kumsajili. Ripoti zimebainisha kwamba winga huyo Mwingereza anaweza kukamilisha kila kitu na kusaini mkataba mpya ndani ya wiki mbili zijazo. Hata hivyo, Arsenal bado haijaweka mezani ofa yao kuhusu mkataba huo mpya. Wakati Kocha Arsene Wenger akifichua kwamba mazungumzo yameisha, kambi ya Walcott imedai kwamba hakuna ofa yoyote iliyowekwa mezani. Liverpool iliweka wazi mwezi uliopita kwamba inahitaji saini ya Walcott ili kurithi mikoba ya Raheem Sterling, ambaye kwa sasa anaringa juu ya mpango wa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Anfield.