• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Malezi ya mzazi mmoja

    (GMT+08:00) 2015-04-20 15:16:07

    Leo hii tutazungumzia masuala mawili ambayo yanaendana kabisa. Kwanza kabisa tutazungumzia idadi inayoongezeka ya kina mama wanaotunza familia zao wenyewe. Maana yake ni "single parent", mzazi mmoja, tena mwanamke.

    Idadi hiyo inaongezeka kwa kasi. Lakini pia tutazungumzia tatizo au ugumu wa kupata mchumba, na hivyo mtu kujikuta akitumia tovuti za kutafutia wachumba ili kujipatia mwenza!

    Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha McGill nchini Canada mapema mwezi huu umeonyesha ongezeko kubwa la kina mama wanaoamua kulea familia zao bila kuolewa. Katika utafiti huo, eneo la Afrika Mashariki na Kati limeonekana kuwa na asilimia kubwa ya kina mama hao, ambapo watatu kati ya kila wanawake kumi wanaona siku hizi hakuna haja ya kuolewa ili uweze kukuza familia.

     Mwenzetu Mark Muli kutoka Kenya alizungumza na baadhi ya wanawake ili kujua mtazamo wao juu ya suala hilo.

    Neller Wangari akipiga chapa katika tarakilishi yake kwenye ofisi yake iliyopo mtaa wa Parklands hapa jijini Nairobi. Yeye ni mmoja wa kina dada ambao wanajikuzia familia zao bila waume. Ninamuuliza Neller ni kwa nini akaamua hivyo?

    Iwapo mambo yanakwenda katika hali hiyo, je kuna shida yoyote na pia kunayo shida katika maisha ya kijamii? Profesa Susan Mwangi ni mhadhiri wa sayansi wa jamii katika chuo kikuu cha St Paul's hapa jijini Nairobi na anaeleza.

    Kulingana na Musyimi Mutuku ambaye ni kiongozi wa kidini ni kwamba hali hiyo imekataliwa hata katika Maandiko Matakatifu.

    Katika utafiti huo kina mama wengi walisema kwamba kulea familia pekee haina ubaya wowote mradi familia iwe na furaha wakitolea mfano ya baadhi ya watu maafuru walilelewa na mzazi mmoja kama vile rais wa Marekani Barack Obama. Lakini Prof. Susan Mwangi anasema pengo la baba haliwezi kuzibwa na chochote chini ya Jua.

    Hata hivyo kulinagana na Neller ni kwamba kila mtu anafaa kuishi maisha yake bila kuzingatia wengine.

    Lakini Musyimi Mutuku ambaye ni kiongozi wa kidini anasema iwapo familia itakuzwa na mama iwe tu ikiwa ni sababu ya kifo ama talaka.

    Kando na hayo Prof Susan Mwangi anasema kizazi cha sasa kinafaa kuelewa kuwa maisha ya familia sio tu kwa sababu ya pesa kuna mambo mengine mengi.

    Ni wazi kuwa kila mtu ana mtazamo wake kuhusu familia. Kuna mtazamo wa kijamii, kidini, na hata kifamilia. Enzi za mababu zetu, haikuwa rahisi kwa binti kupata mtoto nje ya ndoa, kwanza ilikuwa ni aibu kwa familia, na mama wa binti huyo alionekana kuwa ameshindwa kulea. Lakini pia kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuwafanya wakina dada kulea familia zao wenyewe.

    Inawezekana kuwa baba/kijana aliyempa mimba binti amekana kuwa ni mhusika, au huenda amefariki dunia, au kumetokea kutoelewana kati ya wapenzi hao na hivyo kuvunja uhusiano wakati tayari binti ni mjamzito. Lakini kwa sasa kuwa "single parent" imekuwa kama mtindo. Binti anaweza kusema nina uwezo wa kulea mtoto mwenyewe, sihitaji kuolewa. Lakini kama alivyosema Prof. Susan Mwangi, ni kumyima mtoto raha ya kuwa na baba!

    Hilo suala la kuwa mzazi pekee, huenda pia likasababishwa na ugumu wa kupata mchumba kwani siku hizi kuna tatizo moja, vijana wanakuwa na shughuli nyingi kiasi kwamba, suala hilo wanaliweka kando kwanza. Wanajitahidi kuhakikisha wanajiweka vizuri kiuchumi, kwamba ana nyumba, gari, na akiba ya kutosha, ndipo sasa anaanza kutafuta mchumba.

    Na mpaka hayo yote yatimie, muda unakuwa umekwenda, umri nao umesogea, hajui hata pa kuanzia. Ndio maana katika nchi nyingine kuna zile tovuti zinazotumiwa kutafutia watu wachumba. Maana mwisho wa siku mtu anaona afadhali apeleke maelezo yake na picha kwenye tovuti hizo ambazo zitamtafutia mwanaume au mwanamke ambaye wanaendana, kisha kuwakutanisha pamoja.

    Hivi karibuni, tovuti maalumu ya kutafuta wachumba ya China, ilitangaza ripoti ya kwanza kuhusu mapenzi. Tovuti hiyo ilifanya uchunguzi kwa wanachama wake milioni 80, kupata maoni ya vijana wa kisasa wa China kuhusu mapenzi, nusu yao walisema wanatafuta wachumba kutokana na shinikizo la familia au kulazimishwa na marafiki zao. Lakini karibu nusu ya wanaume na zaidi nusu ya wanawake waliohojiwa, walisema kama hawawezi kupata mchumba mzuri, hivyo wanaona bora wawe peke yao. Bw. Li anasema:

    "Sisi vijana, mawazo yetu ni tofauti na ya zamani, tunajenga kila aina ya uhusiano wa kijamii, na hatutegemei uhusiano wa ndoa, tuna fursa kubwa ya kuchagua, tukikutana na wasichana tunaowapenda sana, tutafunga ndoa."

    Vijana wa sasa wana mawazo tofauti na ya kizamani. Pili nadhani utakumbuka zamani wazazi wetu walitafutiwa waume/wake na wazazi wao. Kwanza kabisa wanauchunguza huo ukoo wanaotaka kuoa/kuolewa, kama kuna ugonjwa au kama kuna kitu chochote kinachoweza kuleta mushkeri katika maisha ya mtoto wao.

    Walikuwa makini sana kuangalia tabia ya familia, hususan binti au kijana anayetaka kuoa au kuolewa, kuangalia kama kweli ni mvumilivu na anaweza kuishi vema na familia ya mke/mume. Walikuwa na mambo mengi sana wanayofuatilia ili tu kuhakikisha familia hizo mbili hazitakuja kujuta kutokana na uamuzi huo. Lakini Bi. Chen ana mtazamo gani?

    "Hii ni karne ya 21, hakuna ulazima wa kufunga ndoa, familia zinatofautiana, wazazi wako wanapenda uwe na furaha katika ndoa, lakini siku hizi mambo ya kufunga ndoa haraka na kutalikiana yanatokea mara kwa mara. Vijana hawapendi kuachana kama hawawezi kuishi pamoja kwa furaha. Nataka kufunga ndoa na kuishi kwa furaha pamoja na mchumba mwafaka, na pia wazazi wa pande mbili waridhie ndoa yetu"

    Bi. Chen anataka wazazi wa pande zote mbili waridhie ndoa yake. Na kwa kweli binafsi naona kupata baraka kutoka kwa wazazi wa pande zote mbili ni muhimu kwa maisha ya amani na furaha kwa wanandoa, au unaonaje Pili?

    kusema ukweli bila ya radhi ya wazazi, si rahisi kuwa na amani na furaha kwenye ndoa. Hii ni karne ya 21, na ndoa za siku hizi sio mapenzi tu, bali pia inahusiana na uchumi. Katika uchunguzi kuhusu tofauti ya mapato kati ya wapenzi, asilimia 0.1 ya wanawake wamekubali kuwa kipato chao ni kikubwa kuliko wachumba wao, na zaidi asilimia 70 ya wanawake wanaridhika kama kipato cha wapenzi wao kitawazidi kidogo.

    Lakini kwa upande mwingine, karibu nusu ya wanawake wanaona ni vizuri sana kama kipato cha wapenzi kikilingana, na asilimia 20 ya wanaume wanapendelea wachumba au wake zao wasifanye kazi yoyote bali wawe mama wa nyumbani. Pia kuna vijana wengi ambao hawatilii maanani uwezo wa kiuchumi wa wachumba wao na wanaona kuwa mawasiliano mazuri kati yao ni muhimu zaidi. Bibi Chen Juan anasema:

    "Nataka yeye awe mchapa kazi, na tuwe tunaelewana katika mambo tunayoamini, kwa sasa sijali kama kipato chake ni kidogo, muhimu zaidi ni siku za mbele, kama akifanya kazi kwa bidii atapata kila kitu."

    Lakini wengi wanafuatilia sana kipato cha mume/mke au mpenzi, kwani wanaona kuwa, kama mtu hana kipato kizuri, atawezaje kutunza familia? Basi, msikilizaji unaonaje? Unaona kipato kizuri ni kitu muhimu katika uhusiano wa wapenzi wanaotarajia kufunga ndoa?

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako