• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China kuinua kiwango cha uhakikisho wa huduma za afya kwa walemavu

    (GMT+08:00) 2015-07-23 18:49:31

    Hivi karibuni ofisi ya mambo ya sheria ya Baraza la serikali la China ilitangaza mswada wa kanuni za kuzuia ulemavu na matibabu kwa walemavu, ukiagiza kuwa serikali katika ngazi mbalimbali inapaswa kuwajumuisha walemavu kwenye orodha ya watu wanaolipiwa gharama za matibabu na bima ya matibabu ya kimsingi.

    Bi. Huang Yonghong ni mlinzi shirikishi anayejitolea, na pia ni mlemavu. Kutokana na tatizo la uti wa mgongo, analazimika kupata matibabu mara kwa mara. Bi. Huang alimwambia mwandishi wa habari kwamba yeye ana bima ya matibabu, na anafuatilia sana sera mpya ya bima ya matibabu ya kulipia matibabu ya kuponesha kwa walemavu.

    "Hivi sasa bima ya matibabu haihusishi gharama za matibabu ya kuponesha, inalipa tu gharama za matibabu ya kawaida. Katika nyumba za kutunza wazee, wale wanaotimiza masharti wanapewa ruzuku na shirikisho la walemavu. Pia kuna aina nyingine ya ruzuku kwa ajili ya huduma za afya, lakini inatolewa tu kwa wale walioandikishwa kuwa na ulemavu mkubwa, na wenye ulemavu mdogo hawatapewa."

    Bi. Huang amesema kwa watu wanaohitaji huduma za kuponesha ulemavu, ingawa wanalipia viwango tofauti vya gharama kulingana na ulemavu wao, lakini kwa ujumla gharama hizo ni shinikizo kubwa kwa familia zao.

    Maoni ya Bi. Huang ni sawa na ya profesa Guan Xinping wa idara ya ujenzi na usimamizi wa jamii katika chuo kikuu cha Nankai, yeye pia anaona mswada huo mpya unaopendekeza gharama za matibabu ya walemavu kulipiwa kupitia bima ya matibabu, una athari kubwa ya kijamii.

    "swali la kwanza ni kwamba bima ya matibabu ina ngazi tofauti na aina tofauti, kuna bima ya matibabu kwa wafanyakazi ambayo ina ngazi ya juu zaidi, nyingine ni bima ya matibabu kwa wakazi, yenye ngazi ya chini kidogo. Pili ni huduma za kuponesha ulemavu, kwa muda mrefu uliopita huduma hizo hazikuhusishwa kwenye bima ya matibabu. Kama zikiingizwa kwenye bima, yatakuwa ni maendeleo makubwa."

    Bw. Jing Shan ni mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa afya ya umma katika chuo kikuu cha Qinghua. Anasema hivi sasa walemavu wengi wameingizwa kwenye bima ya matibabu ya kimsingi.

    "Vijijini kuna ushirikiano katika kulipia gharama za matibabu, na hapa mijini kuna bima za aina mbili, moja ni bima ya matibabu kwa wafanyakazi mijini, wakiwemo wafanyakazi walemavu, na nyingine ni bima ya matibabu kwa wakazi wa mijini, ambayo inanufaisha asilimia 96 ya wananchi kote nchini China, wakiwemo walemavu. Zamani kama huna ajira ina maana pia huna bima ya matibabu, lakini sasa hata kama huna ajira unaweza kuandikishwa kwenye bima ya matibabu. Walemavu ambao ni wafanyakazi, au wakazi wa mijini au vijijini, wote wameingizwa kwenye bima ya matibabu."

    Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya walemavu nchini China imefikia watu milioni 85, na zaidi ya milioni 50 kati yao wanahitaji huduma za kuponesha ulemavu.

    Profesa Guan anaona kama gharama za huduma za kuponesha ulemavu zikiingizwa kwenye bima ya matibabu, gharama za bima zitaongezeka. Kwa upande wa dunia nzima, China imefanya vizuri katika utoaji huduma za afya kwa walemavu.

    "Katika siku zijazo gharama za huduma za kuponesha ulemavu zitaongezeka, kwa kuwa gharama hizo ni kubwa ukilipia mwenyewe, hivi sasa ni watu wachache wanaotumia huduma hizo. Kama zikiingizwa kwenye bima ya matibabu na kulipiwa, hakika zitanufaisha walemavu wengi. Naona kiwango cha uhakikisho wa huduma kwa walemavu nchini China kinachukua nafasi ya mbele duniani."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako