• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Chakula cha kichina chatarajia kuorodheshwa kuwa urithi wa kiutamaduni duniani

    (GMT+08:00) 2015-08-14 14:20:24

    Mwaka huu ni mwaka wa tano tangu China ijiandae kutoa ombi la kuorodhesha mapishi ya kichina kuwa urithi wa kiutamaduni duniani. Kwa hiyo katika kipindi cha leo tutazungumzia maendeleo ya kazi hii pamoja na hali ya vitoweo vya kichina katika nchi za nje, haswa Afrika.

    Naibu mkurugenzi wa Shirikisho la mapishi ya China CCA Bw. Feng Enyuan hivi karibuni alisema, China imepanga kuwasilisha ripoti inayohusu kuorodhesha chakula cha kichina kwenye urithi wa kiutamaduni duniani, ili kuenzi na kuhifadhi ustadi maalumu wa mapishi ya kichina.

    Bw. Feng amesema, chakula cha kichina ni utajiri wa taifa la China, na pia ni urithi muhimu kwa ustaarabu wa dunia. Kusukuma mbele mchakato wa kuorodhesha chakula cha kichina kwenye urithi wa kiutamaduni wa dunia, si kama tu kutahimiza maendeleo ya sekta ya chakula cha kichina, bali pia kunakifanya chakula hicho kijulikane zaidi duniani.

    Bw. Feng amesisitiza kuwa lengo la kuorodhesha chakula cha kichina kuwa urithi wa dunia ni kuenzi na kuhifadhi vizuri zaidi mapishi ya kichina. Amesema, utamaduni wa chakula cha kichina unapaswa kuchukuliwa kuwa ni moja ya ushawishi wa kiutamaduni wa China, na kujulikana duniani.

    Kila baada ya miaka miwili Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO linapitisha maombi ya kuorodheshwa kwenye orodha ya urithi wa dunia, na mwaka huu ndio kipindi cha kutoa ombi. Shirikisho la mapishi ya China lilianza kushughulikia kazi hiyo mwaka 2011, baada ya maandalizi ya miaka minne, limekuwa tayari kuwasilisha ripoti kuhusu kuorodhesha chakula cha kichina kuwa urithi wa kiutamaduni duniani kwenye makao makuu ya UNESCO.

    Kwa hiyo ni kitoweo gani cha jadi cha China kitakacho chaguliwa kuwasilisha chakula cha kichina? Hivi sasa vinavyopendekezwa zaidi ni bata wa kuokwa wa Beijing, andazi la kichina au Jiaozi, keki ya mwezi Yuebing, tofu ya kichina, hotpot, wali wa kunata unaofungwa kwa majani au kwa kichina Zongzi, na hata tambi za kuvutwa, Lamian. Naibu mkuu wa shirikisho la mapishi ya China Bw. Bian Jiang amesema, hivi sasa vitoweo vinavyowakilisha mapishi ya China bado havijaamuliwa, na shirikisho hilo litachagua vitoweo vya kichina vinavyolingana zaidi na vigezo vya urithi wa kiutamaduni duniani vilivyowekwa na UNESCO.

    Bw. Bian Jiang amesema, lengo la kazi hiyo si kupata kutambuliwa tu, muhimu zaidi ni kufahamisha kwa kina zaidi wachina na ndugu walioko ng'ambo kuhusu undani wa utamaduni wa vyakula vya kichina. Akifahamisha kuhusu shughuli za utangazaji wa vitoweo vya kichina zilizofanyika, amesema, baada ya shughuli ya kutangaza chakula cha kichina iliyofanyika mwaka 2013 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mwaka jana shirikisho la mapishi ya China liliandaa shughuli mbalimbali za kuutangaza utamaduni wa chakula cha kichina kwenye nchi na sehemu mbalimbali duniani kama vile Marekani, India na Ujerumani.

    "Katika nusu ya pili ya mwaka jana ujumbe wa shirikisho letu ulifanya shughuli mbalimbali za kutangaza mapishi ya Kichina kwenye vyuo 6 vya Confucious nchini Marekani, vyuo vitatu nchini India na pia kwenye shughuli zilizoandaliwa na Shirika la UNESCO huko Paris, Ufaransa. Mwezi Novemba mwaka jana pia tulifanya maonesho ya mapishi ya kichina katika shughuli za kutangaza utamaduni wa China zilizofanyika Ujerumani. Lengo la shughuli hizo ni kutangaza dhana ya urithi wa kiutamaduni ya mapishi ya China kwenye jukwaa la kimataifa, ili kufanya maandalizi zaidi ya kuweza kufanikisha kuorodheshwa kwa mapishi ya kichina kwenye urithi wa kiutamdunia duniani."

    Hatua hiyo pia inafuatiliwa sana na watu wa sekta ya vyakula vya kichina nchini China na katika nchi za nje. Bw. Zhao Hui ni raia wa New Zealand mwenye asili ya China, ameendesha mikahawa ya vyakula vya kichina kwa miaka 25 mjini Wellington. Bw. Zhao ambaye pia ni mwenyekiti wa Shirikisho la mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na New Zealand, amesema, yeye mwenyewe aliwahi kuwa mpishi, hivi sasa aina za vyakula vya kichina vinavyoandaliwa kwenye mikahawa yake zimeongezeka kutoka chakula cha awali cha mkoa wa Guangdong tu, hadi vyakula vya mitindo mbalimbali ya kichina. Amesema, Katika miaka ya hivi karibuni, vyakula vya kichina vimekuwa vikipendwa zaidi na watu wa nchi mbalimbali duniani, kama kikifanikiwa kuorodheshwa kuwa urithi wa kiutamaduni wa dunia, sekta ya vyakula vya kichina katika nchi za ng'ambo itapata fursa nzuri zaidi ya maendeleo.

    "Bila shaka maendeleo zaidi yatapatikana katika sekta ya vyakula vya kichina nje ya China, kwa mfano hapa New Zealand, mikahawa mingi zaidi ya kichina imefunguliwa, kwa hiyo wenyeji wa hapa pia wanafahamu vizuri vyakula vya kichina. Kila baada ya muda, tunaalika wapishi hodari kutoka China kuja kwenye mikahawa yangu, ili kuandaa vyakula vya mitindo mbalimbali ya kichina kwa wateja wetu. Kwa hiyo watu wa hapa wanafahamu vizuri vyakula vya kichina. Kwa sababu vyakula vya kichina pia ni sehemu ya utamaduni wa China, kama vikifanikiwa kuchukuliwa kuwa urithi wa dunia, itakuwa rahisi zaidi kwa vyakula vya kichina kuingia kwenye jamii ya kienyeji. Ni jambo zuri kuandaa vyakula mbalimbali vya kichina kwa ajili ya wateja wa nchi za nje, ili kuwafahamisha zaidi kuhusu vyakula vya kichina."

    Akizungumzia jinsi ya kuenzi na kueneza vyakula vya kichina katika nchi za nje, Bw. Zhao Hui pia ametoa mapendekezo yake.

    "Naona inatubidi sisi wachina wanaoishi katika nchi za nje tufanye kazi halisi, kwa mfano kila baada ya muda, tualike wapishi hodari wa China kuja hapa, tufanye maonesho ya vyakula vya kichina katika nchi za nje, ili kuongeza ufahamu wa wenyeji kuhusu vyakula vya kichina, mitindo tofauti na ladha mbalimbali, kwa njia hiyo, lengo la kueneza vyakula vya kichina litafikiwa hatua kwa hatua."

    Ingawa mikahawa ya kichina inapatikana karibu kila sehemu duniani, haswa katika nchi zenye wahamiaji wengi wa China, lakini hakuna chapa maarufu za vyakula vya kichina zinazojulikana duniani.

    Bw. Lu Wenbin ni maneja mkuu wa kampuni ya vyakula ya Xiaofeiyang ya mkoa wa Mongolia ya Ndani ya hapa nchini China, anaona kuwa vyakula vya kichina mara kwa mara vinaeleweka vibaya katika nchi za nje, kwa kuwa ndugu wengi wa China wa sekta hiyo wanaendesha vibanda vya vyakula vya kichina katika nchi za nje, na kuwafanya wageni wafahamu kwamba vyakula vya kichina ni vya ngazi ya chini tu. Bw. Lu amesema, sekta ya chakula haina vizuizi vikubwa vya kuingia, lakini hali hiyo haimaanishi kuwa sekta hiyo ni ya ngazi ya chini. Vyakula vya kimagharibi hujitokeza kuwa vya ngazi ya juu nchini China, lakini vyakula vya kichina vikoje katika nchi za nje? Bw. Lu ameongeza kuwa, ingawa vyakula vya kichina vimeingia kwenye masoko ya nchi za nje kwa miaka mingi, na ukubwa wa sekta hiyo umeendelea kuongezeka, lakini ushawishi wake bado haujapanuliwa kama ilivyotarajiwa, haswa kwa upande wa ujenzi wa chapa maarufu.

    Tuseme, Utamaduni ni kama mlango. Lakini kwa upande wa sekta ya chakula, Utamaduni ni kama mlango uliofungwa, unaweza tu kupata mafanikio baada ya kupata ufunguo sahihi wa kufungua mlango huo. Kwa hiyo ladha nzuri na mitindo ya kuvutia ni hatua za kimsingi tu kwa ajili ya kufanikisha sekta ya chakula na kueneza vyakula vya kichina duniani.

    Bw. Lu Wenbin anaona, sekta ya vyakula vya kichina katika nchi za nje ikitaka kupata mafanikio, muhimu zaidi ni kurekebisha mbinu za uendeshaji na usimamizi kwa kuendana na mahitaji kwenye masoko ya kienyeji, ili kupunguza au kuondoa tofauti za kiutamaduni. Akitolea mfano wa Hotpot, akasema, njia ya jadi ya chakula cha hotpot cha kichina ambayo wageni wote wanakula chakula kwenye chungu kimoja haikubaliki nchini Marekani, kwa hiyo inatakiwa kubadili kuwa kila mgeni anatumia mlo wake kwenye chungu kimoja kidogo. Mbali na hayo, Bw. Lu amesisitiza kuwa katika kueneza vyakula vya kichina katika nchi za nje, jambo jingine muhimu ni kuzingatia tofuati za kidini na kuheshimu tabia za wenyeji.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako