• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Uzinduzi wa wiki ya matangazo ya redio na maonyesho ya picha za mji wa Zhengzhou

    (GMT+08:00) 2015-08-18 10:14:33

     

     

     

    Ujumbe kutoka mji wa Zhengzhou nchini China umeandaa maonyesho ya wiki moja ya matangazo ya redio na maonyesho ya picha za mji huo mjini Nairobi.

    Maonyesho hayo ya wiki moja yalizinduliwa jana jioni katika hoteli ya Safari Park kwa ushirikiano wa serikali ya mji wa Zhengzhou,ubalozi wa China nchini Kenya na Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa,kwa ajili ya kuwajulisha wakenya kuhusu historia na utamaduni wa mji wa Zhengzhou,ambao ndio chimbuko la Kungfu ya Shaolin.

    Haya ni maonyesho ya Kungfu ya Shaolin yakiendelea wakati wa maonyesho ambayo yatadumu kwa muda wa wiki moja mjini Nairobi ili kuwajulisha wakenya kuhusu historia na utamaduni wa mji wa Zhengzhou wa China.

    Zhengzhou ni mji mkuu wa mkoa wa Henan nchini China. Ni mji unaojulikana kama mojawapo ya miji minane yenye historia kuu nchini China.Kungfu ya China inatoka mji wa Zhengzhou.

    Ujumbe kutoka Zhengzhou ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya mawasiliano ya umma wa manispaa ya mji huo Bw Wang Zhe ulifika Nairobi kwa ajili ya maonyesho haya.

    Katika hotuba yake kwenye uzinduzi wa wiki ya matangazo ya redio na maonyesho ya picha za mji wa Zhengzhou Bw Wang Zhe alisema katika wiki hii mji wa Zhengzhou utatangazwa na kuonyeshwa kwa wakenya wote kupitia picha na filamu.

    Aidha alisema mji huo utashirikiana na Kenya katika mambo ya maendeleo.

    "Kutokana na mikakati ya maendeleo ya Rais Xi Jinping ya ujenzi wa njia za Hariri,afrika mashariki itafurahia fursa nyingi zaidi za maendeleo katika siku za usoni.Na kutokana na hayo tunatafuta fursa nyingi zaidi za ushirikiano kwa ajili ya maendeleo kati ya sehemu nyingine duniani ikiwa ni pamoja na Kenya."

    Wakati huohuo Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya teknolojia ya mawasiliano nchini Kenya Bw Victor Kyallo alisema kuna mambo mengi ambayo Kenya na hasa Nairobi inafaa kuiga kutoka mji wa Zhengzhou.

    Alisema licha ya maendeleo ya kiuchumi,usafiri,na teknolojia mji wa Zhengzhou haujapoteza asili ya utamaduni.

    "Naamini mojawapo ya somo kubwa ambalo tutasoma ni kuwa unaweza kufanya maendeleo kama ilivyo katika mipango yetu lakini bado ukasalia na utamaduni wako.Baadhi ya picha tulizoona zinaelezea hayo kwa njia nzuri kabisa"

    Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu ulinzi na masuala ya kigeni Mheshimiwa Ndung'u Githinji alisema Kenya na China zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na China imekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia Kenya katika Nyanja mbalimbali.

    Alisema ili kuboresha uhusiano kati ya nchi hizi mbili na uhusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili ni muhimu kwa China kufikiria kujenga chuo cha mafunzo ya kungfu ya china mjini Nairobi.

    "Katika kuimarisha zaidi uhusiano baina ya mji wa Zhengzhou na Nairobi tungependa kuona ujenzi was hue ya mafunzo ya kungfu ya shaolin hapa Nairobi ikiongozwa na watawa wa shaolin.Hii itasaidia kuboresha mabadilishano ya utamaduni na kuimarisha ushirikinao baina ya watu wa nchi hizi mbili"

    Balozi wa China nchini Kenya Bw Liu Xianfa alisema mabadilishano ya utamaduni baina ya watu kati ya nchi hizi mbili yamekuwa karibu zaidi kadri siku zinavyosonga.

    Taasisi nne za Confucious na darasa moja la Confucius zimeanzishwa nchini Kenya na kuifanya Kenya kuwa mojawapo ya nchi zenye taasisi nyingi za Confucius barani Afrika.

    Balozi Xianfa alisema utamaduni ndio daraja muhimu la mawasiliano.

    "Utamaduni ni daraja la mawasiliano na kiunganishi cha kufanikisha maelewano na uaminifu baina ya nchi.China na Kenya zina tamaduni sawa,ambazo zinasisitiza umuhimu wa amani na maelewano,urafiki na majirani na kutafuta maisha ya furaha"

    Kungfu ya China imepata umaarufu duniani kote na watalii kutoka pande mbalimbali za dunia huzuru hekalu la Shaolin mjini Zhengzhou ili kushuhudia ustadi wa kungfu katika hekalu hilo lenye historia ndefu.

    Maonyesho haya kuhusu mji wa Zhengzhou na utamaduni wake mjini Nairobi yatakamilika wiki ijayo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako