• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Watu wa jamii ya Bushmen

    (GMT+08:00) 2015-08-21 15:37:40

    Msikilizaji mpendwa, karibu katika kipindi cha utamaduni wetu. Na leo hii tutazungumzia watu wa jamii ya Bushmen. Jangwa la Kalahari lililoko nchini Botswana, kusini mwa Afrika, siku zote lina ukame na ukosefu wa mvua, lakini hapa ni nyumbani kwa watu wa jamii ya Bushmen ambao wana asili ya Afrika Kusini na nchi jirani za Botswana na Namibia. Katika jangwa hilo, watu wa jamii ya Bushmen wanasifiwa kama wataalamu wa mimea, udaktari na uwindaji. Lakini baada ya kulazimishwa kuhama kwenye jangwa hilo, wanakabiliana na matatizo mengi wakati wakiishi mijini. Mwandishi wetu wa habari Ronald Mutie anatuletea maelezo zaidi.

     


    Katika miaka elfu 15 kabla ya kristo, watu wa Bushmen walikuwa wameenea kusini mwa Afrika, na wao pia ni miongoni mwa watu wa kwanza walioishi barani Afrika. Lakini kutokana na uvamizi na mauaji ya wakoloni kutoka nchi za Magharibi, katika karne ya 15 idadi ya watu wa jamii ya Bushmen ilipungua haraka, baadhi yao walikimbilia jangwa la Kalahari. Lakini kufuatia amri ya kupiga marufuku uwindaji iliyotolewa katika miaka ya tisini karne iliyopita na serikali ya Botswana, wengi wa watu wa jamii ya Bushmen waliokuwa wakikaa katikati ya jangwa la Kalahari walilazimishwa kuhamia ukanda wa kando wa jangwa hilo. Sehemu ya Ghanzi ikawa ndio makazi ya watu wa jamii ya Bushmen.

    Douglas ni mwongozaji watalii kutoka Zimbabwe, katika miaka kadhaa iliyopita alikuja hapa Ghanzi kufanya kazi na kuishi pamoja na watu wa jamii ya Bushmen, hivyo anafahamu lugha yao. Anapokutana na watu wa jamii ya Bushmen wanasalimiana kwa lugha yao. Watu wa jamii ya Bushmen wanavaa mavazi yanayotengenezwa kwa ngozi ya wanyama, na kutokana na maisha magumu yanayowakabili hata mtu mwenye umri wa miaka 30 hivi, anaonekana amezeeka zaidi kuliko hali halisi. Awali watu wa jamii ya Bushmen waliishi kwenye ukoo mkubwa wenye jamaa 20 hadi 60, lakini kufuatia kupungua kwa chakula, ukoo mkubwa unagawanywa katika familia ndogo kadhaa.

    Wakati wakoloni kutoka nchi za Magharibi walipokutana na watu hao wa asili, waliwapatia jina la Bushmen, likiwa na maana watu wanaoishi misituni. Jina hilo lina maana ya kuwadharau watu hao, pia linaonesha uhusiano kati ya watu wa jamii ya Bushmen na misitu. Watu wa jamii ya Bushmen wanafahamu kila aina ya mmea, baadhi ya matunda yanaweza kuliwa, na baadhi ya matunda yanaweza kutumiwa kama dawa. Douglas anasema, baadhi ya mimea inayoweza kutengenezwa dawa ambayo iligunduliwa na watu wa jamii hiyo hivi sasa imeingizwa barani Ulaya.

    "Madaktari kutoka nchi za Magharibi walikuja katika jangwa la Kalahari, walichukua mimea inayoitwa 'mkono wa shetani' ambayo iligunduliwa na watu wa jamii ya Bushmen na kupeleka kwenye maabara zao kufanya uchunguzi, na kufahamu mimea hiyo inafanya kazi ya kutibu magonjwa. Hivi sasa, mimea hiyo inauzwa barani Ulaya na kutibu magonjwa ya baridi yabisi na magonjwa ya mifupa. "

    Mbali na hayo, watu wa jamii ya Bushmen pia ni wawindaji hodari. Katika miaka zaidi ya elfu moja iliyopita, hawakuwa wakifuga wanyama wala kulima mashamba, bali waliishi maisha kwa kutegemea kuwinda wanyama au kukusanya matunda. Watu wa jamii ya Bushmen wanafahamu sana kutumia upinde na mshale. Walitumia mifupa ya wanyama na matawi ya mti kutengeneza upinde, na kung'arisha mifupa na mawe kuwa alama ya mshale.

    Lakini kutokana na amri ya kupiga marufuku uwindaji iliyotolewa na serikali ya Botswana, watu wa jamii ya Bushmen hawawezi kuishi maisha kwa kutegemea uwindaji, ustadi wao wa kuwinda pia unapotea siku hadi siku. Watu hao walilazimishwa kubadilisha mtindo wa maisha, familia nyingi za watu wa jamii ya Bushmen wamehamia sehemu zilizoko karibu na hoteli, na kufanya maonesho kwa watalii, ili kupata mapato na maji bure kutoka kwenye Mahoteli. Hawataki kuishi mjini, hivyo wanaendelea kushikilia mtindo wa maisha ya jangwani kadri iwezekanavyo.

    Douglas anawaonea huruma watu hao waliopoteza makazi, anasema,

    "Serikali iliwahamisha watu wa jamii ya Bushmen kutoka jangwa la Kalahari na kuwaleta kwenye jamii ya kisasa, lakini hawana uwezo wa kuishi maisha ya kisasa, wanao ustadi wa kuishi misituni, hivyo wanaishi katika hali ngumu."

    Habari kutoka vyombo vya habari vya nchi za Magharibi zinasema, wafanyabiashara wa almasi wa nchi za Magharibi waligundua madini ya almasi katika jangwa la Kalahari, hivyo waliitaka serikali ya Botswana kuwafukuza watu wa jamii ya Bushmen kwenye jangwa hilo. Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali ya Botswana ilitoa amri ya kupiga marufuku uwindaji na kuwalazimisha watu hao kuhamia makazi ya nje ya jangwa hilo.

    Lakini habari hiyo imekanushwa na serikali ya Botswana. Profesa Andy Chebanne kutoka Chuo kikuu cha Botswana anasema, hatua hiyo ya serikali ya Botswana inalenga kuwahamisha watu wa jamii ya Bushmen katika eneo moja la makazi, ili kujenga shule, hospitali na kutoa huduma ya maji.

    "Sidhani kama lengo la serikali kuwahamisha watu wa jamii ya Bushmen ni kuchimba almasi, kwa sababu madini ya almasi pia yaligunduliwa katika sehemu nyingine. Serikali iliwahamisha wanavijiji wanaofuga wanyama katika sehemu ya kando tu, lakini haikuwahamisha nje ya sehemu hiyo. Nafikiri sababu kuu ya serikali kuwahamisha watu wa jamii ya Bushmen nje ya jangwa ni kupunguza gharama ya kuwajengea watu hao walioenea jangwani hospitali, shule. Hivyo ilitaka kuwahamishia watu hao katika sehemu moja, kuwapatia chakula na kuwasomesha watoto wao shuleni."

    Mkuu wa shule ya msingi ya Ghanzi Bw. Muller anasema, lengo la serikali kuwahamisha watu wa jamii ya Bushmen ni kulinda wanyamapori na mazingira ya asili.

    "Uwindaji sio tatizo, tatizo ni watu wa mijini wanawatumia watu wa jamii ya Bushmen kuwinda, na kununua wanyama waliowawinda. Watu wa jamii ya Bushmen pia wanahitaji pesa, hivyo waliwauza wanyama waliowawinda. Hali hiyo itafanya wanyama watoweke, wanawinda kwa ajili ya pesa wala sio chakula. "

    Hivi sasa watu wa jamii ya Bushmen ni suala nyeti nchini Botswana. Kwa sababu watu wengi wa jamii hiyo wamelazimishwa kuhama kutoka jangwa la Kalahari, na kuishi kando ya miji. Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vinaendeleae kuikosoa serikali ya Botswana, na kuwataka watu hao warudi katika mazingira yao ya maisha ya asili. Lakini profesa Chebanne anaona hatua ya kuwahamisha watu wa jamii ya Bushmen si kosa, isipokuwa isingetumia njia ya kuwalazimisha. Anatoa mfano wa Namibia.

    "Ukienda Namibia, utaona serikali ya nchi hiyo imetenga sehemu kubwa kwa ajili ya watu wa jamii ya Bushmen wanaoishi nchini humo, serikali iliwajengea makazi, maduka ya kazi za mikono, shule, na kuwapatia madaraka ya kutawala sehemu hiyo. Watalii wanaweza kuja kupiga picha, kuangalia jinsi wanavyoishi, na kutembea nao misituni. Serikali ya Botswana inatakiwa kujifunza mtindo huo, kuwafanya watu wa jamii ya Bushmen kutawala sehemu kadhaa, na kuwaambia kuwa kama mkishindwa, mtapoteza vitu vyote. "

    Katika shule ya msingi ya Ghanzi, wanafunzi wengi ni watoto wa watu wanaotoka jamii ya Bushmen. Mkuu wa shule hiyo Muller anasema, watoto hao wanaweza kupata elimu bure. Pia anasema, shule za msingi na sekondari zote za Botswana ikiwemo shule hiyo, zinafundisha lugha rasmi za Kingereza na Kitswana tu, hazifundishi lugha za makabila madogomadogo. Muller anaeleza kuwa kujifunza Kingereza na Kitswana kutavisaidia vizazi vijavyo vya watu wa jamii ya Bushmen kuwasiliana na watu wengine.

    Profesa Chebanne anasema, anapochunguza utamaduni wa watu wa jamii ya Bushmen, anagundua kuwa watoto wa watu hao hawafahamu ustadi wa kuishi misituni kama mababu zao. Kutokana na kuondoka kwenye mazingira ya asili, ujuzi wa watu wa jamii hiyo kuhusu mazingira ya asili unapotea siku hadi siku. Anaona utamaduni wa jadi wa kipekee wa watu wa jamii ya Bushmen unastahili kuhifadhiwa, lakini pia wana haki ya kupata elimu shuleni, kufahamu dunia ya nje na kujifunza uwezo wa kujiendeleza kama watu wa nchi nyingine duniani.

    "Wakati aina mbili za utamaduni zinapokutana, kukwepa si njia nzuri, bali tungejifunza mambo mazuri ya utamaduni mwingine kwa msingi wa kudumisha mila na desturi zetu. Awali watu wa jamii ya Bushmen walipokutana na ustaarabu wa kisasa, walikimbia, inaonekana wanataka kulinda utamaduni wao, lakini ukweli ni kwamba utamaduni wao unatoweka haraka zaidi kutokana na kutawaliwa na kulazimishwa kuhama, hawana nguvu ya kuzuia utamaduni kutoka nje na kudumisha mila na desturi zao."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako