• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mapishi ya Tambi za kukaanga, supageti na makaroni

    (GMT+08:00) 2015-09-01 10:11:04

    Wageni wengi wanaotoka katika nchi za nje waliopo hapa China wanapenda kula chaomian yaani tambi zinazokaangwa kwa mafuta, tambi hizi zinaweza kupikwa kwa namna mbalimbali, mbali na kutiwa zhajiangmian yaani vipande vya nyama zilizokaangwa na kuchanganywa na tianmianjiang, na tambi zilizochemshwa pamoja na nyama ya ng'ombe, tambi zinaweza kukaangwa na kuwa chakula kitamu sana. Kuna aina nyingi za mapishi ya chaomian, unaweza kuchagua yale unayopenda.

    Sasa tuangalie mapishi ya tambi za kukaanga au chaomian baadaye tutaangalia mapishi ya tambi za supageti na makaroni. Katika mapishi ya chaomian kwanza unatakiwa kufanya maandalizi: kwanza unatakiwa kuwekwa uyoga ndani ya maji na kuloweka kwa muda mrefu kidogo kabla ya kuanza kupika, halafu nyama ioshwe vizuri kwa maji, nyanya zikatwe vipande vidogovidogo, kabeji ya kichina, pilipili na vitunguu vikatwe vipande vyembamba, kisha vunja mayai na kuyapiga katika bakuli na uyaweke pembeni, mboga utakazoweka unaweza kuongeza au kupunguza kadiri utakavyo; baada ya hapo lamian yaani tambi ndefu unaziweka pembeni baada ya kuzichemsha na kupoozwa mara mbili kwa maji baridi, unatakiwa kukumbuka kuwa unapochemsha tambi, huna haja ya kuchemsha sana. Baada ya hapo unaweka mafuta kwenye sufuria, tia mayai katika sufuria na ukaange kidogo hadi yanapoanza kuwa magumu, kisha yatoe; weka vipande vya nyanya na chumvi kidogo katika sufuria, kisha ukaange kwa moto mdogo au mkubwa kiasi, wakati nyanya inapoanza kulainika, weka mboga nyingine zilizokatwa, na uzikaange kwa moto mkali kwa dakika moja hivi, kisha weka vitu vingine vyote vilivyobaki katika sufuria, vikaange tena kwa dakika moja, kisha weka mayai yaliyokwisha kaangwa pamoja na tambi zilizochemshwa katika sufuria, na kuzichanganya vizuri.

    Mmmh kwa kweli hiki ni chakula ambacho nakipenda sana kwani ni kitamu halafu kina lishe nzuri kwasababu ndani ya tambi hizi kuna mboga zinazochanganywa ambazo kila siku tunasisitiza kuwa ni muhimu sana.

    Sasa tunaendelea mbele na mapishi ya tambi aina za macaroni. Waswahili huwa wana msemo mmoja usemao mchele mmoja mapishi tofauti. Lakini leo tuna tambi tofauti kwa mapishi tofauti, lakini zote ni tambi. Haya pili tuendelee na upishi wetu wa macaroni.

    Katika upishi huu wa macaroni kwanza unatakiwa kuwa na macaroni, mayonnaise, mafuta, chumvi, tuna wa kopo, au kama unapendelea nyama ya kusaga au kuku wa kusaga pia sawa, kotmiri, kitunguu maji. Kwanza chemsha maji kwenye sufuria ndani ya maji tia mafuta na chumvi. Mafuta yatasaidia macaroni yasigandane. Yakishachemka tumbukiza macaroni yako. Wakati macaroni yanachemka anza kukata kitunguu maji kiwe vipande vidogo sana. baada ya hapo changanya vitunguu na chumvi kisha uvioshe ili kupunguza ukali, kama unapenda na ukali wake pia sawa. Kata kotmiri ndogondogo. Baada ya hapo tia kwenye bakuli la tuna, au nyama au kuku wa kusaga kisha changanya na mayonise pamoja na kotmiri. Halafu onja kama kila kitu kiko sawa. Wakati unafanya hivyo huku unaangalia macaroni yako, kama yamewiva yamwage maji uweke pembeni. Kisha pakua macaroni kwenye sahani halafu utie mchanganyiko wako wa mayonnaise, kotmiri samaki na kitunguu na hapo macaroni yako yanakuwa tayari kwa kuliwa.

    Na kama tunavyosisitiza kila siku kuwa unapopika chakula chochote hakikisha unapika kwa njia ya kuleta afya mwilini na sio kuridhisha mdomo na tumbo tu. Sasa tuaangalie manufaa ya mapishi yetu kwa afya ya mwili, kwanza katika tambi za chaomian kuna mboga kama kawaida, mfano kuna kabichi la kichina, nyanya, na vitunguu. Vitu hivi kama tulivyosema awali ni mbogamboga, na sote tunafahamu umuhimu wa mboga mwilini ingawa nyanya unaweza kuiweka kwenye kundi la mboga au tunda jinsi upendavyo, lakini inachukuliwa kama chakula muhimu mwilini. Nyanya inaongeza phytochemicals mwilini kama vile lycopene.

    Mbali na hayo nyanya ni chanzo cha vitamini A na C mwilini pamoja na folic acid. Pia nyanya inasaidia kupambana na uundwaji wa vitu vinavyojulikana kusababisha saratani. Nainasaidia mfumo wa ngozi kutokana na kuwa na vitamin C hivyo hufanya ngozi kuwa nyororo na yenye afya. Kwa hiyo kwa ujumla nyanya ina manufaa makubwa mwilini na kupikwa kwenye chakula kama tambi inafanya tambi zako ziwe chakula cha afya.

    Mbali na nyanya unatumia mayonnaise kitu ambacho ni kizuri kwa afya ikilinganishwa na mafuta, ingawa mimi mwenyewe sipendi mayonise lakini kwa kweli ina manufaa makubwa kwa afya ya mwili. Wataalamu pia wamethibitisha hilo kwani baadhi ya watu wanaamini kuwa mayonnaise sio nzuri kwa afya. Sosi ya mayonnaise ina omega 3 fatty acid na vitamin E vitu ambavyo ni vizuri kwa afya ya binadamu. Kwa hiyo mayonnaise inasaidia kuzuia kiharusi na ni nzuri kwa moyo. Pia inasaidia kufanya kazi vizuri kwa mapafu, kwani sote tunafahamu kuwa mapafu ni kiungo muhimu katika mwili wa binadamu.

    Ingawa mayonnaise ina umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu lakini ina calorie nyingi ambayo inaweza ikampelekea mtu kuongezeka uzito, hivyo ni vizuri ikaliwa kwa kiwango maalumu na sio kuliwa nyingi kwa wakati mmoja, na hii si kwa mayonnaise bali hata kwa vyakula vingine. Unapokula unatakiwa ule kidogo tu usile chakula kingi, ni bora ukala kwa siku mara nne chakula kidogo kuliko kula mara mbili chakula kingi kupita kiasi. Kwa hiyo kwa ujumla leo umeweza kufahamu umuhimu wa mlo wetu wa leo ambao ni tambi za kichina chaomian, supageti na macaroni ambapo tunashauri unapopika uchanganye na mboga na sio kupika halafu kuweka sukari kama watu wengi wanavyopendelea hususan kule Tanzania.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako