Kama nilivyosema kwenye makala yangu ya jana, mjini Changsha kuna vivutio kedekede vya utalii. Leo hii baada ya kustaftahi, nilitembelea Bustani ya Machungwa. Bustani hii iko kwenye kisiwa cha Juzi na ina ukubwa wa karibu 60 Mu sawa na hekta 4, na katika bustani hiyo, kuna aina takriban 44 za machungwa ambazo idadi yake inafikia 4000.
Wakati huu wa majira ya moukutiko (autumn), upepo mwanana kutoka Mto Xiang unapuliza na kuleta harufu nzuri ya machungwa yanayokaribia kuiva. Katika bustani hii nimekuta watu wengi, wenyeji kwa wageni, wakifurahia mandhari na kula machungwa matamu yanayopatikana kwenye bustani hiyo.
Kivutio kingine kikubwa nilichokiona kwenye kisiwa hicho ni sanamu kubwa ya mwanzilishi wa China mpya, Mao Tse Tong, ama wengi tunavyomfahamu, Mao Zedong. Sanamu hii inamwonyesha kiongozi huyo wakati akiwa na umri wa miaka 25, kijana mdogo, na ilimazilika na kuzinduliwa Septemba 26, 2009, wakati wa kumbukumbu ya 116 ya siku ya kuzaliwa kwa mwenyekiti huyo. Sanamu hii ilisanifiwa na mkuu wa chuo cha sanaa cha Guangzhou aitwaye Li Ming, na ni sanamu kubwa zaidi kwa sasa ya Mwenyekiti Mao, yenye urefu wa mita 32 na upana wa mita 83. Sanamu hii imechongwa ikiangalia mwelekeo wa mawio ya jua na ardhi aliyoipenda na hata kuipigania. Sanamu hiyo inachukuliwa kama chachu kwa vijana, ambayo ni alama ya vizazi vilivyomwaga damu yao na kutoa maisha yao kwa ajili ya mapinduzi ya China.
Baada ya kutoka kwenye eneo iliko sanamu ya Mwenyekiti Mao, nilifika kwenye jumba ambalo linatumika kuonyesha jinsi mji wa Changsha unavyoishi kirafiki na mazingira. Jumba hilo linatumia umeme wa jua. Na nilipata fursa ya kutazama filamu fupi kuhusu vyanzo vya uchafuzi wa hewa, ambavyo ni pamoja na kukata miti ovyo, kumwaga maji machafu kwenye vyanzo vya maji, pia athari za kimaumbile kama moto na hata mafuriko. Lakini mji wa Changsha umechukua hatua kadhaa ikiwemo kupanda miti, kutumia nishati mbadala, na umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza hewa chafu.
Kilichonivutia zaidi kwenye jengo hilo, ni kwamba kwenye uwanja ulio mbele yake, kuna sanamu mbalimbali zilizochongwa kwa kutumia mabaki ya chuma cha pua. Hii inaonyesha wazi kuwa, kuliko kutupa mabaki hayo ambayo baadaye yatakuwa na athari mbaya kwa jamii, wasanifu wameunda sanamu mbalimbali kwa kutumia mabaki hayo, na hivyo kuendelea kuufanya mji wa Changsha kuwa mji wa Kijani.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |