• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tibet, chimbuko la Dansi ya Shon na nyimbo za mishale za Kongpo

    (GMT+08:00) 2015-09-18 17:59:29

    Huu ni mwaka wa 50 tangu mkoa unaojiendesha wa Tibet uanzishwe, kwa ajili ya kuadhimisha jambo hilo muhimu la kihistoria, tumeandaa vipindi viwili mfululizo kuhusu utamaduni maalumu wa kitibet na juhudi zilizofanywa kuhifadhi na kuenzi utamaduni huo. Na hii ni sehemu ya pili na ya mwisho ya mfululizo wa vipindi kuhusu Tibet.

    Katika kipindi kilichopita, tulifahamisha kuhusu utenzi wa mfalme Gasar na wasanii wanaoghani utenzi huo mkoani Tibet. Leo hii tutaangalia dansi na nyimbo zenye mitindo maalumu ya kitibet.

    Kaunti ya Zanda iko kaskazini magharibi mwa mkoa unaojiendesha wa Tibet, watalii wengi kutoka nchini na nchi mbalimbali duniani hwenda kwenye kaunti hiyo kuona mandhari ya kushangaza ya kijiografia iitwayo misitu ya udongo au kwa kiingereza "Soil forest", pamoja na mabaki ya kale ya enzi ya mfalme Gurge iliyoanzia karne ya 10 na kudidimia ghafla baada ya miaka 700. Lakini kwa Bi. Ren Yunjuan aliyetembelea kaunti ya Zanda mara nyingi, ardhi hiyo ina mvuto mwingine maalum.

    "mimi ni mwanafunzi wa shahada ya udaktari katika chuo kikuu cha Minzu cha China. Miaka miwili iliyopita nilipokuja kushiriki kwenye mkutano mmoja kuhusu utamaduni, kwa mara ya kwanza nilitazama dansi ya Shon iliyochezwa na wasichana nikavutiwa sana. Hii ni mara yangu ya tatu kuja hapa kutazama dansi hiyo."

    Dansi ya Shon iliyotajwa na Bi. Ren inatoka katika lugha ya Kisanskrit, ikiwa na maana ya dansi kwa lugha ya kitibet. Dansi ya Shon iliyoanzia kwenye eneo la Ngari kaskazini magharibi mwa mkoa wa Tibet, ni moja ya dansi za kasri katika Tibet ya kale, ambayo inajumuisha usomaji, uimbaji na dansi yenyewe, na kila muondoko wa dansi hiyo una vigezo vyake.

    Ingawa ni vigumu kuthibitisha dansi ya Shon ilianzishwa mwaka gani, lakini ni hakika kwamba dansi hiyo ina historia ya zaidi ya miaka elfu moja. Kwa sababu kwenye mabaki ya enzi ya Gurge, bado unaweza kuona wazi michoro kwenye ukuta wa kasri inayoonesha wasichana zaidi ya 10 wakicheza dansi ili kuwaburudisha mfalme na wageni wake.

    Mwongoza watalii kwenye mabaki ya enzi ya Gurge Bazan Ciugene anaona, dansi hiyo iliyochezwa na wasichana kwenye michoro ya ukuta ndiyo ni dansi ya Shon.

    "Katika enzi ya Gurge, kuna hekalu moja linaloitwa hekalu jekundu, ambalo kuna michoro ya aina hii kwenye ukuta wa hekalu hilo. Dansi hiyo ni ya kidini, inasemekana kwamba dansi hiyo ilikuwa inachezwa kwenye sherehe za kidini tu. Baadhi ya nyaraka zinasema dansi hiyo inatoka dini ya kienyeji ya Tibet iitwayo Bon, kwa kuwa wacheza dansi hiyo wanazunguka kinyumenyume, halafa ikaenezwa katika jamii. Hadi leo pia kuna warithi wa dansi hiyo ambao bado wanacheza."

    Mzee Zhuoga mwenye umri wa miaka 84 aliyezaliwa katika kaunti ya Zanda ni mmoja wa warithi wa dansi ya Shon. Amesema alianza kujifunza dansi hiyo akiwa na umri wa miaka 21 hadi 22, wakati ambapo Tibet bado ilikuwa ikitekeleza mfumo wa kilimo wa utwana wa kikabaila, mzee Zhuoga akiwa ni mtwana, mwanzoni hakujifunza dansi ya Shon kwa hiari.

    "Wakati huo kila famila ya watwana ililazimika kutoa mwanamke mmoja kujifunza dansi katika nyumba za maofisa. Licha ya watu waliochaguliwa, wengine hawakuruhusiwa kucheza dansi ya Shon, kwa kuwa ilikuwa ni dansi ya kuburudisha mfalme. Dansi hiyo si ngumu kujifunza, lakini nilikuwa na hofu sana, kwa kuwa kama sikujifunza vizuri nisingeweza kumaliza jukumu langu nililopewa, na badala yake ningelazimika kuwa mke mdogo wa maofisa, ambayo ilikuwa ni kama adhabu."

    Mzee Zhuoga akikumbusha maisha yake ya zamani, amesema kabla ya Tibet kufanyiwa mageuzi ya kidemokrasia mwaka 1959, kucheza dansi ya Shon kulikuwa ni kama aina moja ya kazi ya utwana. Baada ya mageuzi, dansi hiyo ikapewa hadhi mpya. Haswa ilipofika mwaka 2008, dansi ya Shon ya Gurge iliorodheshwa kuwa urithi wa kiutamaduni wa taifa la China na wizara ya utamaduni ya China. Bibi Zhuoga akiwa mcheza dansi mzee zaidi, alitambuliwa kuwa mrithi wa dansi hiyo wa ngazi ya kitaifa. Ili kurithi na kuenzi dansi hiyo ya kale, mpaka sasa mzee Zhuoga amesajili wanafunzi wanawake 9.

    "Kutokana na msaada wa serikali, nimeanza kusajili wanafunzi. Bila kujali nitakuwa na machofu kiasi gani, na baridi kiasi gani katika siku za baridi, nitaendelea na mafunzo yangu."

    Dansi ya Shon ina sehemu 13. Kutokana na uzee, Bibi Zhuoga hawezi kukumbuka vizuri sehemu zote za dansi hiyo. Lakini kwa wanafunzi wake, anawafundisha kadri anavyojua.

    "Naweza kucheza sehemu zote 13 za dansi ya Shon, lakini sio kamili sana, nakumbuka vizuri sehemu 9. Kwa sababu dansi hiyo ni ya kihistoria, na ina hadithi zake, kwa hiyo nawafundisha kwa kufuata miondoko ya asili bila mabadiliko yoyote."

    Siku hiyo, kwenye hekalu la Tholing ambako bibi Zhuoga alikuwa akicheza dansi ya kuwaburudisha wakuuu na matajiri, wanafunzi wake walikuwa wakishikana mikono, na kudansi huku wakiimba kwa ajili ya kuwakaribisha wageni. Wakati huo, unaweza kujihisi kwamba umerudi kwenye historia na kuona mwenyewe wacheza dansi waliochorwa kwenye ukuta wakidansi mbele yangu.

    Bi. Yang Jin mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akijifunza kwa mzee Zhuoga kwa miaka 10. Kila ifikapo sikukuu na mashindano ya dansi yanayoandaliwa na vijiji au kaunti, Bi. Yang Jin hupenda kuonesha ustadi wake hodari wa kucheza dansi. Anasema, mashairi mazuri ya nyimbo za dansi ya Shon ndiyo yanayomvutia aendelee kucheza dansi hiyo.

    "Mashairi ya nyimbo nyingi za dansi ya Shon yanahusiana na mambo ya kidini kuhusu mahekalu, budhaa wanaoishi na watawa, au sehemu tunapoishi sisi watu wa Tibet, wazazi wetu, au hata misitu na kadhalika, dansi ya Shon inahusisha mambo yote. Kulingana na kaulimbiu tofauti, mbinu ya kuimba nyimbo hizo pia ni tofauti."

    Baada ya kupata wanafunzi, mzee Zhuoga pia ana wasiwasi, kwa kuwa tofauti na dansi nyingi za kitibet zenye vitendo vikubwa na miondoko ya haraka, dansi ya Shon inazingatia zaidi miondoko ya taratibu. Wasiwasi wake ni kwamba kutokana na mabadiliko ya maisha ya watu, mashairi ya kale na vitendo vya taratibu vya dansi ya Shon yataweza kuwavutia vijana wa sasa au la.

    Mwaka 2011, kundi la kwanza la wacheza dansi ya Shon liitwalo Kundi la wasanii wa jadi la Kaunti ya Zanda lilianzishwa. Serikali ya huko inatumai kuandaa wasanii wa kizazi kipya wa dansi ya Shon miongoni mwa vijana wenyeji, ili waweze kuenzi usanii huu wenye historia ya karne kumi.

    Kwenye jumba la mazoezi la kundi la wasanii wa jadi la Zanda, wacheza dansi walikuwa wakiandaa mchezo wa dansi ya Shon unaoeleza historia ya enzi ya Gurge, kwa ajili ya tamasha la sanaa za kijadi la Xiangxiong ambalo ni shughuli kubwa ya kiutamduni ya huko. Tofauti na dansi ya jadi ya Shon, vitendo vikubwa na miondoko ya kasi pia vimeingizwa kwenye mchezo huo wa Shon. Pembezoni mwa jumba hilo, mzee Zhuoga ambaye ametoka hospitali hivi karibuni alikuwa amekaa na kutamaza kimya.

    Mkuu wa kundi hilo Kelsang Yuzhen amesema, mzee Zhuoga amekuwa na umri mkubwa na pia amefanyiwa upasuaji, kwa hiyo hafai kucheza dansi mwenyewe jukwaani, ingawa ni hivyo anafuatilia sana urithi na maendeleo ya dansi ya Shon.

    "Leo tunafanya mazoezi ya mchezo ya dansi ya Shon, bibi Zhouga amekuja kutuelekeza. Tumevaa nguo za michezo ili kumonyesha. Mchezo wetu una sehemu nne, nilimwelezea kila sehemu ya mchezo huo, halafu akatupa maoni yake."

    Alipoulizwa kama amehisi uchovu, mzee Zhuoga mwenye mikunjo mingi usoni anaonekana kuwa na utulivu na kuridhika.

    "Nimeanza kupenda kuimba na kucheza dansi tangu nilipokuwa mtoto, kwangu mimi kucheza dansi si jambo la kuchosha hata kidogo. Sasa maisha yamekuwa mazuri, nafurahi sana kuona vijana wakiimba na kucheza dansi. Nikitazama mchezo huo, najisikia kwamba nimerudi zamani wakati ambapo wote walikuwa wanaweza kucheza dansi ya Shon, ninafurahi sana."

    Chini ya misitu ya udongo ya Zanda, kandoni mwa mto Xiangquan, wanafunzi wa mzee Zhuoga wanaghani mashairi ya kale, na kwa njia ya kucheza dansi, wanaonesha kumbukumbu za ardhi hiyo zenye historia ya zaidi ya miaka elfu moja.

    Baada ya kumfahamu mzee Zhuoge na juhudi alizofanya kuenzi dansi ya Shon, sasa tutupie macho sanaa nyingine ya uimbaji mkoani Tibet.

    Kwenye eneo la Nyingchi, kuna sanaa moja maalumu ya uimbaji iitwayo nyimbo za mishale za Kongpo, ambazo huimbwa kwenye mashindano ya kurusha mishale. Usanii huo wa kale si kama tu haujatoweka, bali umeendelea kung'ara kwa uhai wake mpya jukwaani, na kuwa shughuli maalumu za burudani zinazopendwa sana na wenyeji na watalii.

    Uliosikia ni wimbo wa mishale wa Kongpo unaoimbwa na bibi Sangye Kangco mwenye umiri wa miaka 75. Mashari ya wimbo huo yanasema, "katika mahali wanakoishi ndege wengi, unatakiwa kutafuta mwenye busara zaidi; ingawa unatakiwa kufanya hivyo, lakini kwa kweli hakuna mwenye busara, wapo tu ndege wa mapenzi wanaoruka kutoka katikati ya ziwa." Huu ni wimbo wa mapenzi ambao mashairi yake ni marefu na yenye maana ya ndani. Nyimbo kama hizo huimbwa wakati watu wa Tibet wakishindana kurusha mishale yenye milio ya mluzi, ndiyo maana zikapewa jina la nyimbo za mishale za Kongpo.

    Katika tarafu ya Mainri ambayo ni chimbuko la nyimbo hizo, wakati wa mashindano ya kurusha mishale, unaweza kuona wanaume wanaovaa nguo za kijadi za kabila la Kongpo la Tibet wakivuta upinde kwa nguvu na kisha kurusha mishale yenye ncha maalumu zinazoweza kutoa sauti za mluzi kwa kulenga shabaha iliyoko umbali wa mita 40. Kama wakipata shabaha, wapiga mishale hupongezana, huku watazamaji wanaoimba nyimbo za mishale wakija mbele na kuwapongeza kwa pombe ya shayiri. Tofauti na sehemu nyingine kwenye uwanda wa juu wa Tibet, eneo la Nyingchi lililoko chini kidogo, limejaa misitu pamoja na hali ya hewa mwanana. Katika zama za kale, uwimbaji kwa kutumia upinde na mishale ulikuwa ni njia muhimu ya uzalishaji mali kwa kabila la kienyeji la Kongpo. Lakini kutokana na mabadiliko ya wakati, desturi hiyo ya kale imebadilika kuwa shughuli muhimu ya burudani kwa wenyeji wa huko, yaani mashindano ya kurusha mishale ya milio ya mluzi. Zikiwa ni sehemu muhimu katika mashindano hayo, nyimbo za mishale pia zinapendwa na kuimbwa sana na wenyeji wa huko.

    Mzee Sangye Kangco ambaye ni mrithi wa nyimbo za mishale za Kongpo wa mkoa wa Tibet, pia ni mwimbaji mzee zaidi wa nyimbo hizo kwenye eneo analoishi. Miaka 30 iliyopita, yeye na wenzake wa rika moja walianza kujifunza kuimba nyimbo hizo kutoka kwa mzee Lordan, lakini kwa sasa wasanii wengine wote wamefariki dunia, bibi Sangye Kangco amekuwa mwimbaji wa pekee anayeweza kuimba nyimbo hizo kwa mitindo ya asili, hali ambayo imemfanya ajisikie mpweke sana. Binti yake Tsering ameona upweke wake akamwambia mama yake kwamba anataka kujifunza nyimbo hizo za mishale. Sasa mara kwa mara wanaimba nyimbo hizo kwa pamoja. Bi. Tsering anasema:

    "Nafurahi sana kila mara ninapoimba nyimbo hizo, haswa wakati wa kuimba pamoja na mama yangu."

    Mbali na nyimbo za mapenzi, nyimbo za mishale pia zinasifu ustadi hodari na ushujaa wa waimbaji. Kama ilivyo nyimba za jadi za Tibet, nyimbo za mishale za Kongpo pia hazina mabadiliko makubwa katika miondoko yake, lakini zina mashairi mengi tofauti, haswa unaweza kutunga mashairi mwenyewe wakati wa kuimba. Ni kutokana na sababu hiyo, mpaka sasa bado hakuna rekodi za maandishi kuhusu miondoko na mashairi ya nyimbo hizo, ambazo zinafundishwa tu kutoka kwa walimu hadi kwa wanafunzi.

    Baada ya kuchaguliwa kuwa mrithi wa nyimbo za mishale za Kongpo, kufundisha nyimbo hizo kwa vijana kumekuwa sehemu muhimu ya maisha ya mzee Sangye Kangco. Hivi sasa zaidi ya watu 10 miongoni mwa wote 60 wa kijiji anachoishi wanaweza kuimba nyimbo hizo, wakiwemo binti na mjukuu wake. Pia kuna watu wengi kutoka vijiji vingine wanaokwenda kwa mzee huyo kujifunza nyimbo na kuandika mashairi yake. Bibi Sangye Kangco anasema:

    "Hivi sasa watu wengi wameweza kuimba nyimba za mishale za Kongpo, nafurahi sana. Wakati wa mapumziko, tunakunywa pamoja pombe ya shayiri, tukikaa pamoja na kuimba nyimbo. Nafurahi sana nikiwaona watu wengi wakiimba nyimbo hizo."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako