• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wakulima wa mpunga wanavyofaidika kutokana na kilimo hicho

    (GMT+08:00) 2015-09-19 18:50:38

    Katika ziara yangu mkoani Hunan, katikati ya China, pia nimeweza kutembelea mji wa Yiyang, hususan kaunti ya Nanxian.

    Katika kaunti hii, nilitembelea mradi wa ngazi ya juu wa ujenzi wa maji salama ya kunywa. Afisa mmoja wa kituo hicho kwa jina la Cai Jiaming alifahamisha kuwa wakazi wa kaunti hiyo walikuwa wakisumbuliwa sana na ugonjwa wa mawe kwenye figo. Baada ya wataalam kufanya uchunguzi, waligundua kuwa tatizo hilo linatokana na maji ya kunywa ambayo hayakuwa salama. Hivyo serikali ya kaunti hiyo iliamua kujenga kituo cha mradi wa maji salama ya kunywa kwa wakazi hao. Maji hayo yanachimbwa kutoka ardhini, umbali wa mita 100 chini ya ardhi, na yanapitia katika sehemu kadhaa kabla hayajasambazwa kwa wakazi.

    Tangu mradi huo uanze kutekelezwa, idadi ya wanakijiji wanaokutwa na tatizo la mawe kwenye figo imepungua kidhahiri, na hii ni hatua kubwa iliyopigwa katika kuhakikisha afya ya wakazi wa kaunti hiyo.

    Baada ya kutoka kwenye kituo hicho, nilipata fursa ya kutembelea shamba la mpunga katika kaunti ya Huarong. Wakulima nilioongea nao wanasema huu ni wakati wa mavuno, na wakimaliza, msimu wa baridi unakuwa umefika, hivyo wanapumzika kwa muda mpaka msimu mpya wa kilimo utakapofika.

    Kitu kiliconifurahisha zaidi ni kuwa, wakulima hao wameunda ushirika na kuingia ubia na kampuni ya kuuza mchele iitwayo Ming Tai. Nchini China kuna utaratibu unaoiwezesha kampuni kuingia ubia na ushirika. Kampuni hiyo hutoa mbegu bora na msaada wa kifundi kwa wakulima, pamoja na kufuatilia mchakato mzima wa kilimo husika. Baada ya mavuno, mkulima anaiuzia kampuni husika mavuno yake na kupata malipo yake papo hapo, hivyo mkulima anafaidika kutokana na jasho lake na kampuni nayo inafaidika maana ina uhakika na ubora wa bidhaa.

    Hivyo ndivyo kampuni ya Ming Tai ilivyofanya kwa ushirika wa wakulima wa mpunga wa kaunti ya Huarong. Wakulima hao wamenieleza kuwa kampuni hiyo imewapatia mbegu bora na teknolojia bila kuwatoza gharama yoyote, hivyo kufanya kiasi cha mavuno yao kuongezeka kwa kiasi kikubwa, na kama hiyo haitoshi, kampuni hiyo pia imetoa msaada wa kiteknolojia na kiufundi, hivyo kufanya mpunga unaozalishwa nao kuwa wa ngazi ya juu.

    Nilipotoka hapo shambani nilitembelea kiwanda cha Ming Tai, na nilipofika, nilikutana na mkulima mmoja akihesabu mafao yake, na nilipomuuliza kwa mwaka anapata kiasi gani, alisema si chini ya Yuan laki tano kutokana na mauzo ya mpunga wake kwenye kampuni hiyo. Kwenye uwanja wa kampuni hiyo, kuna malori yameongozana ya wakulima ambao nao wamekuja kuuza mpunga wao.

    Binafsi jambo hili nimeona lina manufaa makubwa kwa wakulima na pia kwa kampuni. Kama ushirikiano huu ungekuwepo kwenye nchi nyingi za Afrika, ni wazi kuwa kilimo kingekuwa ni cha kisasa zaidi, hali ya maisha ya wakulima ingekuwa ni ya juu, na hata kampuni zinazoshughulika na uzalishaji wa ngano, mchele, na hata mahindi zingeweza kufaidika. Kwa mfano, kampuni inayoshughulika na uuzaji wa mchele au hata ngano, ikiingia ubia na ushirika wa wakulima wa kijiji fulani, na kutoa teknolojia ya kisasa, mbegu bora, na kufuatilia mchakato mzima wa kilimo, ni wazi kuwa bidhaa zingekuwa na ubora wa juu, na hata watumiaji wasingekuwa na malalamiko. Lakini kutokana na kununua hapa na pale, bila ya kujua ubora wa bidhaa, mara nyingi kampuni hizo zimekuwa zikilalamikiwa na watumiaji kwa kuuza bidhaa zisizo na ubora.

    Licha ya makampuni, mfumo huu wa ushirikiano pia unaweza kuwasaidia wakulima kwa kiasi kikubwa. Kwani mkulima anaondokana na matumizi ya mbegu zisizo na ubora, teknolojia duni, na adha ya kutafuta soko, na pia anaondokana na mtu wa kati (middleman) ambaye kwa kawaida anadai pesa aweze kumsaidia mkulima kuuza mazao yake kidogo yaliyopatikana. Lakini kwa mfumo huu niliouona hapa China, mkulima anawasiliana moja kwa moja na kampuni kupitia ushirika, na kizuri zaidi, mkulima yeye mwenyewe anapeleka mazao yake na kupokea fedha yake yeye mwenyewe, bila ya mtu wa kati, hivyo anaona matunda ya kazi yake ngumu anayoifanya.

    Kama wakulima kwenye nchi zetu wakitumia vilivyo ushirika wao, na ushirika huo ukasimamia maslahi ya wakulima, ni dhahiri kuwa hali ya maisha ya wakulima hao itabadilika, na faida ya jasho lao wataiona. Jambo hili linawezekana, ni kuamua, na kutenda.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako