Wachumi na vyombo vya habari vya nchi za nje vinaona kuna mustakbali mzuri kuhusu itikadi ya maendeleo iliyomo kwenye mpango mpya wa 13 uliopitishwa na malengo yaliyowekwa kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya China katika miaka mitano ijayo.
Tovuti ya Vermelho ya Brazil imeandika kuwa China imetoa fursa nyingi kwa dunia kutokana na sera yake ya kufanya mageuzi ya kina na kutumia uvumbuzi katika miaka mitano iliyopita. Profesa mshiriki Zhou Zhaocheng wa Chuo cha Teknolojia cha Nanyang anasema, maendeleo ya uvumbuzi wa internet, hususan, yamepenya kwenye sekta zote za jamii na viwanda, na kubadili moja kwa moja mfumo wa kiuchumi na jamii wa China. Hivyo sera kuhusu maendeleo ya uvumbuzi wa internet, iliyowekwa kwenye Mpango wa 13 wa miaka mitano, itakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya baadaye ya China.
Mchumi kutoka Marekani Laurence J. Brahn ameliambia Shirika la Habari la Russia Sputnik kuwa, kuanzisha ustaarabu mpya wa kulinda mazingira, kuliko kuzingatia peke yake ukuaji wa GDP, itakuwa kipaumbele kipya cha serikali ya China kuelekea mwaka 2020. Amesema Chama cha Kikomunisti cha China CPC, kitaleta zama mpya wa ustaarabu wa kiikolojia, na kutoa wito wa aina mpya ya ukuaji ambao ni wa jumla na wenye uwiano, kuliko kusimamia maendeleo ya kasi ya uzalishaji viwandani kama ilivyokuwa kwenye karne iliyopita.
James Laurenceson wa kituo cha uhusiano wa China na Australia amesema, kufungua soko la ndani ni silaha muhimu ya mageuzi ambayo inaweza kuinufaisha China. Amesema ingawa kuna baadhi ya sekta ambazo bado zinalindwa, na ambazo zitafuatiliwa katika miaka mitano ijayo, anatarajia kuwa kupunguzwa kwa vikwazo vya kuingia kwenye sekta binafsi kwa kampuni za ndani na nje, itakuwa na umuhimu mkubwa katika mpango wa 13 wa miaka mitano.
Nicjolas Lardy, msomi kutoa kituo cha uchumi wa kimataifa cha Peterson anasema, ukuaji wa chini ya asilimia 7, au hata asilimia 6.5, ni lengo linalofaa ambalo bado litaifanya China kuwa mchangiaji mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa dunia. Nchini Thailand, mkurugenzi wa kitivo cha masomo ya China ASEAN kilicho kwenye chuo kikuu cha Usimamizi cha Panyapiwat, Tang Zhimin amesema, China iliyowazi zaidi inatoa fursa zaidi kwa bidhaa, huduma, na uwekezaji kutoka nchi za nje. Amesema mpango wa 13 wa miaka mitano wa China sio tu unalenga ukuaji wa uchumi, lakini pia maendeleo ya kina ya uchumi, siasa, jamii, utamaduni, na ustaarabu wa kiikolojia.
Mkurugenzi wa utafiti katika jopo la washauri la chuo cha masomo ya kimataifa cha Canon nchini Japan Kiyoyoki Seguchi amesema, watu wa China wanaongoza kwa maisha ya utulivu huku serikali ikihakikisha nafasi za ajira na kusimamia bei. Ameongeza kuwa, kama China itaendelea kushikilia sera zake kutokana na kupungua kasi ya ukuaji lakini kuwa na ukuaji imara, maisha ya watu yataendelea kuboreshwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |