• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Watoto wakiwezeshwa kuwapenda wanyama pori itasaidia kupunguza ujangili katika siku zijazo

    (GMT+08:00) 2015-12-31 09:58:59

    Leo hii tutaangalia zaidi watoto wa shule nchini Kenya na fursa za kuangalia wanyama pori, kwani kama tunavyofahamu kuwa watoto ndio viongozi na walinzi wetu wa siku za baadaye, hivyo kama tukiwaandaa, kuwakukuza na kuwajengea tabia nyoofu itasaidia katika maisha yao ya baadaye.

    Watoto ndio viongozi wetu wa kesho, na ndio maana waswahili wanasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo au udongo upate ulimaji, hivyo tukiwalea na kuwakuza katika maadili na tabia njema za upendo kwa watu na kwa wanyama hususan wanyama pori basi baadaye hatutakuwa na matatizo makubwa kama vile ya kuwepo majangili au mauaji ya wanyama pori. Kwa hiyo msikilizaji leo hii tutawazungumzia watoto wa Kenya waliopata kwenda kujionea macho yao wanyama pori katika mbuga moja ya wanyama. Ingawa wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wanasafiri na kwenda Kenya kutembelea mbuga za wanyama, Lakini kwa watoto wengi wa Kenya hawajawahi kwenda kwenye mbuga hizo na kuangalia wanyama kama vile simba. Hata hivyo kwa sasa wanamazingira wanajaribu kubadilisha hilo.

    Richard Muchiri ni mwanafunzi wa shule mwenye miaka 14 ambaye anaishi kilomita chache kutoka Mbuga ya Taifa ya Aberdare nchini Kenya yeye ni miongoni mwa watoto waliobahatika kutembelea katika mbuga ya wanyama na hii ni mara yake ya kwanza kabisa kufika huko. Kama ilivyo kwa watoto wengine wanaokulia vijijini nchini Kenya, Richard Muchiri amewahi kukutana na wanyama pori wakati wanyama hao walipovamia shamba la mazao la wazazi wake. Lakini kwa vile misitu iliyo karibu na nyumbani kwao imeshonana sana hivyo kwa sasa ni nadra sana kwa wanyama pori kuingia kijijini kwao.

    Hivyo baada ya hivi karibuni mfuko wa kuhifadhi simba 'Ewaso Lions' kufanya mashindano na kuwaalika watoto wa shule za msingi kuandika kuhusu shughuli za uhifadhi, aliandika insha juu ya umuhimu wa misitu. Na kwa bahati nzuri alishinda na kupata nafasi katika Lion Kids Camp, ambayo ni matembezi ya mbugani katika hifadhi ya Salio kwa wanafunzi 16 wa shule ya msingi. Akiwa na hamu kubwa ya kutembelea mbugani Richard Muchiri anasema

    "Nataka kuona wanyama pori kwasababu watu wengi hawaelewi kwanini wanyama pori ni muhimu katika nchi yetu. Hivyo baada ya kujua kuhusu wanyama hao, nitaweza kuja na kuwafunza namna ya kuwalinda ili kumaliza ujangili."

    Ni maneno mazuri anayoyasema Richard Muchiri kwasababu elimu atakayopata sio tu itamfanya aondokane na dhana za ujangili bali pia itamuwezesha kuelewesha watu ubaya wa vitendo hivyo. Mfuko wa kuhifadhi simba 'Ewaso Lions' ulianzishwa mwaka 2007 na mwanasayansi wa mazingira na mchunguzi aliyejishindia tuzo Shivani Bhalla, ili kulinda simba wa Kenya walio hatarini na kuishirikisha jamii kuweza kuwahifadhi na kuwaenzi. Sera ya usimamizi wa wanyama pori nchini Kenya inaruhusu wanyama hao kutoka nje ya maeneo wanayohifadhiwa na kufika hadi kwenye maeneo yanayomilikiwa na watu binafsi au katika maeneo ya jamii, hivyo jamii ina umuhimu mkubwa wa kuwalinda.

    Mwaka 2013 Ewaso Lions ilianzisha kambi ya kwanza ya watoto ya kuhifadhi simba huko Samburu, ikiwa na lengo la kuwafanya watoto wa Kenya kuwa na hamu ya kulinda na kujitolea kulinda mazingira yao. Hivi sasa wanataka kupanua kazi zao kwa kushirikiana na wanajamii katika sehemu nyingine za Kenya.

    "Watoto wengi wa Kenya, hususan wa maeneo ya vijijini, hawana uzoefu mzuri na wanyama pori. Wana mtazamo mbaya tu juu ya wanyama hao. Kwa upande wa Samburu ambako ndiko ninakoishi, watoto wa huko huwa wanawaona duma wakiwaua mbuzi, tembo wakiwakimbiza watu, mizoga ya ngamia baada ya kuliwa na simba, yaani ni mambo mabaya tu. Hata hivyo watu kutoka maeneo yote duniani wanakuja kuwaona wanyama pori wa Kenya na wakenya hawaelewi kwanini huwa hawaoni uzuri wa wanyama hao. Hivyo kwa sisi ni muhimu kwamba tujaribu na kubadili hali hii, ni vyema tuwafanye watoto wawe na mtazamo mzuri juu ya wanyama pori".

    Kwa watalii wengi wanaotembelea mbuga za wanyama, kuona simba porini ni jambo muhimu sana, na kwa ziara hii watoto wana bahati sana, kwani wanaweza kuwa karibu na simba wakiwaona wamelala kwenye majani marefu mwanzoni mwa safari yao

    "Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona simba, simba dume, yaani nilikuwa naogopa, lakini kwa vile tulikuwa kwenye gari, muongozaji alinipa moyo hivyo woga ukaisha, nikaingiwa na moyo.

    Kwa kweli kwa mtoto mdogo kuwa karibu na simba ni jambo la kuogopesha na hii si kwa mtoto hata kwa mtu mzima pia, kwani sote tunafahamu hatari ya kuwa karibu na simba, hivyo Richard Muchiri alikuwa na kila haki ya kuogopa. Lakini mwalimu wake, Lucy Kamau, naye pia amekuwa na shauku kama wanafunzi wake na kuwapa matumaini kwa kuimba na kufurahia pamoja katika safari yao nzima. Akiwa kama mwalimu wao wa Kingereza na Sayansi katika shule ya msingi ya Laburra, alikuwa ni mtu muhimu aliyewatia moyo watoto kuwasilisha insha zao kwenye mashindano ya Lions Kids Camp.

    "Wakiwa hapa kitu kikubwa ni kwamba wataweza kujitambua wao na wanyama pori, watajua uzuri wake, hivyo pindi wanapomuona kindi mdogo, hawatamuua! Wanapaswa kujua kwanini wanyama wanapaswa kuishi pamoja na binadamu, na pia watajifunza uzuri wa kuwahifadhi."

    Lakini sio simba tu wanaowafunza watoto hao somo muhimu katika masuala ya uhifadhi. Muongozaji watalii wa mbugani Fred Kinaiyia anajua kuwa kwa watoto, viumbe vidogo kama vile kombamwiko vinaweza kuwavutia. Na pia kuweza kukutana kwa karibu zaidi na wanyama pori wa Kenya kutaweza kuwafanya wapate elimu kubwa ya zaidi ya siku mbili ambazo watakuwa kwenye matembezi ya mbuga za wanyama.

    "Wengi wao hata hawajui kwamba simba wako matatizoni, wanasema kwani simba wana matatizo? Kweli? Na ziara hii inahusiana na hilo, inawaelimisha, kwa hiyo wanaelewa, ndio, simba wapo kwenye matatizo, tuna simba chini ya 2000 hapa Kenya, ni hao tu. Ni idadi ndogo sana na kila siku tunapoteza simba hapa, kwa hiyo jambo hili tunataraji litabadilika kupitia kwa hawa watoto."

    Lakini sio simba tu walio matatizoni. Kuna spishi nyingi zilizo hatarini nchini Kenya, wakiwemo vifaru ambao wamekuwa wakiipa sifa hifadhi ya Salio. Na katika miaka ya mbele, eneo la wanyama pori la Kenya linaweza likapotea, kutokana na idadi ya watu kuendelea kukuwa zaidi. Hivyo wataalamu wa kuhifadhi mazingira wanatarajia kuwa watoto wanaweza kuwa viongozi, wavumbuzi na walimu wa kuhifadhi mazingira, na kusaidia kutunza na kuyalinda makazi ya asili ya Kenya kwa ajili ya vizazi vijavyo.

    Ni kweli kwani hata mimi naamini kuwa shughuli kama hizi za kuwafunza watoto mapema umuhimu wa mazingira na wanyama, tena sio kwa Kenya tu, au kuhifadhi mbuga za wanyama pamoja na hifadhi za wanyama ni suala zuri kwani kama tunavyofahamu hivi sasa vitendo vya ujangili, na mauaji ovyo ya wanyama pori yameshamiri. Hivyo elimu hii itasaidia kupunguza vitendo hivyo katika siku za mbele na kuvifanya vizazi vijavyo kuwa karibu na wanyama pori na kuwapenda.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako