China yatangaza ripoti kuhusu hatua na sera za China katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa mwaka 2015
(GMT+08:00) 2015-11-19 17:37:30
Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China imetoa ripoti kuhusu hatua zilizochukuliwa na sera za China katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa mwaka huu. Ripoti hiyo inasema, katika miaka mitano iliyopita, China imepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kupitia marekebisho ya mwundo wa viwanda, kubana matumizi ya nishati na kuinua ufanisi wake, kuongeza nishati safi na kupanda miti. Katika mkutano wa hali ya hewa utakaofanyika huko Paris, China iko tayari kushirikiana na pande mbalimbali kuhakikisha mkutano huo unafikia makubaliano yanayotarajiwa kwenye msingi wa haki na kanuni ya "wajibu mmoja majukumu tofauti".
Ripoti hiyo imejulisha kwa pande zote hatua mbalimbali zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini China. Kiwango cha utoaji wa hewa ya carbon dioxide nchini China kwa mwaka 2014 kilishuka kwa asilimia 15.8 ikilinganishwa na kile cha mwaka 2010 na matumizi ya nishati isiyo ya mafuta yameongezeka huku eneo la misitu likiongezeka na kupita kiwango tulichoahidi.
Mwezi wa Juni mwaka huu, serikali ya China ilitoa waraka wa kutoa mchango katika mabadiliko ya hali ya hewa kwa sekritariati ya makubaliano ya mabadiliko ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa, ikibainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2030 utoaji wa hewa ya carbon wa China utafika kileleni, ambapo matumizi ya nishati isiyo ya mafuta yataongezeka zaidi huku ufanisi wa matumizi ya nishati utaongezeka zaidi.
Naibu mkurugenzi wa Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China ambaye pia ni mjumbe maalumu wa China anayeshughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, Bw. Xie Zhenhua anasema, kubana matumizi ya nishati na kuongeza ufanisi wa nishati ni njia muhimu za kutimiza malengo hayo.
"Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia, katika miaka 20 iliyopita, kiasi cha nishati iliyobanwa nchini China kinachukua asilimia 52 ya kile cha jumla cha dunia nzima. Katika miaka mitano iliyopita, robo ya nishati safi iliyotumiwa duniani, ilitumiwa nchini China."
Mkutano wa hali ya hewa utakaofanyika mwezi wa Desemba huko Paris, unatarajiwa kutoa azimio la kuongeza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa baada ya mwaka 2020. Bw. Xie anaona kuwa katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, haki, uwezo wa kila nchi na kanuni ya "wajibu mmoja majukumu tofauti" zinatakiwa kuzingatiwa.
"Nchi mbalimbali zinatakiwa kutekeleza kwa makini makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo yaliyopita. Kwa mfano, kabla ya mwaka 2020 nchi zilizoendelea zinatakiwa kupunguza utoaji wa hewa ya carbon kwa asilimia 25 hadi 40 kulingana na kiwango cha mwaka 1990. Na nchi hizo zimeahidi kuwa kabla ya mwaka 2020 zitatoa uungaji mkono wa dola bilioni 100 za kimarekani kila mwaka kwa nchi zinazoendelea na kuanzisha utaratibu wa kuhamisha teknolojia. Tunatarajia ahadi hizo zitatekelezwa, huu ndio msingi wa kujenga uaminifu wa kisiasa."