• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yahamasisha "watu wote kusoma vitabu"

    (GMT+08:00) 2015-12-17 16:34:18

    Kuanzia mwaka 2006, China imependekeza na kuhamasisha "watu wote kusoma vitabu", na sehemu mbalimbali zimefanya shughuli za uhamasishaji. Ofisa mhusika wa idara kuu ya habari, uchapishaji, radio, filamu na televisheni amesema, katika miaka iliyopita ya hivi karibuni idadi ya watu wanaosoma vitabu imeongezeka kidhahiri. Hata hivyo, wataalam wamesema shughuli za kuwahimiza watu kusoma vitabu bado zinaweza kuendelezwa zaidi, na mashirika ya uchapishaji yanapaswa kuchapisha vitabu bora, kufanya uvumbuzi katika njia za uenezi wa vitabu na usomaji vitabu vya digitali, ili kukidhi mahitaji ya jamii.

    "Napenda kusoma vitabu vya utamaduni na sayansi ya kijamii, na ninapendelea kusoma vitabu vya historia. Kila mwaka nasoma vitabu 20 hadi 30 hivi."

    "Hivi sasa soko la vitabu ni zuri, napenda vitabu vinavyochapishwa na mashirika ya uchapishaji ya Zhongxin na Lixiangguo."

    "Kwa kawaida nasoma vitabu vya kitarakimu kwa kutumia Kindle, na kila mwezi nasoma kitabu kimoja au vitabu viwili hivi, siku hizi sisomi sana vitabu vya karatasi."

    Kuanzia mwaka 2006, China ilianza kampeni za kuwahimiza watu kusoma vitabu, na kuzidisha nguvu katika kutangaza vitabu bora. Kwa nyakati tofauti, ilitenga dola za kimarekani zaidi ya elfu 155 kujenga "maktaba vijijini", na miji zaidi ya 400 nchini China imeandaa shughuli mbalimbali za "usomaji wa vitabu".

    Kwenye mkutano kuhusu kampeni za kuhimiza wananchi wa China kusoma vitabu uliofanyika tarehe 25 Novemba, naibu mkuu wa idara kuu ya habari, uchapishaji, radio, filamu na televisheni Wu Shangzhi alisema, kwa mujibu wa uchunguzi kuhusu watu kusoma vitabu uliofanyika kuanzia mwaka 2010 hadi 2014, idadi ya watu wanaopenda kusoma vitabu imeongezeka kidhahiri, akisema,

    "Kiwango cha idadi ya watu wazima wanaosoma vitabu kimeongezeka hadi asilimia 58 kutoka asilimia 52.3, huku kile cha idadi ya watu wazima wanaosoma vitabu vya kitarakimu kimeongezeka hadi asilimia 58.1 kutoka asilimia 32.8. Kwa wastani kila mtu anasoma vitabu vyingi zaidi. Takwimu hizo tatu zimeonesha matokeo mazuri yaliyopatikana katika shughuli za kuhamasisha watu kusoma vitabu."

    Hata hivyo Bw. Wu Shangzhi pia amesema, kampeni za kuhamasisha watu kusoma vitabu zinatakiwa kufanyika kwa muda mrefu ili kupunguza pengo la ujuzi miongoni mwa wananchi na kulinda haki ya wananchi ya kupata elimu, na kampeni hizo bado zinakabiliwa na changamoto nyingi, Bw. Wu alisema,

    "Nchini China idadi ya vitabu maktaba kwa mtu mmojmmoja ni 0.55, kiwango ambcho ni cha chini kikilinganishwa na kilichopendekezwa na Shirikisho la vitabu la kimataifa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO, ambacho ni vitabu 1.5 hadi 2.5 vya maktaba kwa mtu. Vilevile ujenzi wa maktaba mitaani na maktaba ndani ya idara za serikali na makampuni bado uko katika kipindi cha majaribio. China ina watu milioni 260 wanaotafuta vibarua mijini na watoto wao milioni 23 wanaohamahama na wazazi hawalengwi na huduma za umma za miji mingi nchini China, na watoto wengine wanaobaki nyumbani vijijini hawana mazingira mazuri ya kusoma. Aidha, vitabu kwa ajili ya watu wasioona havitoshi."

    Ofisa mhusika wa idara kuu ya habari, uchapishaji, radio, filamu na televisheni amesema, idara hiyo itaharakisha utungaji wa mpango wa kuwahamasisha watu kusoma vitabu, kujenga utaratibu wa kuongoza kazi hiyo, na kuhimiza utungaji sheria husika, ili kujenga "Jamii yenye tabia ya kusoma vitabu". Idara hiyo pia imezitaka sehemu mbalimbali zijumuishe usomaji wa vitabu kwenye mpango wa maendeleo ya uchumi na jamii, na kukamilisha utaratibu husika wa usimamizi na tathmini.

    Lakini kuhamasisha watu kusoma vitabu hakuwezi kutegemea serikali tu. Mashirika ya uchapishaji yanabeba jukumu la moja kwa moja. Kampuni ya uchapishaji na vyombo vya habari ya China ni shirika kubwa zaidi la uchapishaji nchini China, ambayo chini yake kuna mashirika maarufu ya uchapishaji kama vile The Commercial Press, Joint Publishing na Zhonghua Book Company, na duka la vitabu linalokuwa wazi saa 24 mjini Beijing, ambalo linasifiwa sana na kuyafanya maduka ya vitabu yaliyoanza kutoweka kupata uhai tena.

    Naibu mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Sun Yuemu amesema, mashirika ya uchapishaji yanapaswa kuendana na matakwa ya jamii, cha muhimu zaidi ni vitabu kuwa na yaliyomo mazuri, na njia za uenezi pia zinatakiwa kuzingatiwa. Bw. Sun alisema,

    "Kama tuna machapisho mazuri tu bila njia nzuri ya uenezaji, machapisho hayo mazuri hayawezi kuuzwa vizuri. Tunavyofanya ni kupanua uenezi, kwa mfano kuzindua duka la vitabu la saa 24 la Taofen, jambo ambalo waziri mkuu wetu Bw. Li Keqiang aliandika barua na kulisifu, kwani linawaletea watu uzoefu mzuri wa kusoma, pia linaandaa semina, kutoa mapendekezo ya vitabu vizuri, kujadili baadhi ya masuala ya jamii yanayofuatiliwa na watu wengi, na kuandaa kongamano la kusoma vitabu, kwa kufanya hivyo linavifanya vitabu vyetu vizuri viingie katika familia na kwenye jamii."

    Katika kipindi cha sasa, tukipendekeza watu wasome vitabu, hatuwezi kupuuza mwelekeo wa kuibuka kwa vitabu vya kitarakimu. Hivi sasa, APP ya usomaji kwenye simu za mkononi na vitabu vya kitarakimu vimekuwa sehemu muhimu ya usomaji. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye uraibu wa kusoma kupitia simu za mkononi, Bw. Sun amesema wamepata mafanikio katika uchapishaji wa kitarakimu, hali ambayo imethibitisha ulazima wa kufanya uvumbuzi katika njia za uchapishaji. Bw. Sun amesema,

    "Tuna 'tovuti ya Dajia" ambayo tunaonesha machapisho yetu, na imekuwa jukwaa muhimu la uenezi wa vitabu nchini China. Kwa mfano, The Commercial Press ilitoa kauli mbiu ya "vitabu vya karatasi na toleo la kielektroniki vitolewe kwa wakati mmoja", yaani vitabu vyote vya karatasi vikitolewa, pia kuwe na toleo lake la kielektroniki, na wakati huohuo tunashirikiana na kampuni ya amazon na kutoa toleo hilo kwenye mtandao wa internet, na imekuwa biashara nzuri, kufanya hivyo si kama tu kunakidhi mahitaji ya jamii, bali pia kuna faida ya kiuchumi, na hii inathibitisha kuwa mahitaji ya wasomaji yanakidhiwa."

    Wataalamu wanasema kampeni za kuwahamasisha watu kusoma vitabu sio tu zinawanufaisha watu kiakili, pia zinayanufaisha zaidi makampuni ya utamaduni yanayofanya uvumbuzi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako