• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mabadiliko ya Ziwa Honghu yaonesha juhudi za China kuhifadhi ardhi oevu

    (GMT+08:00) 2015-12-31 10:00:22

    "Katika ziwa la Honghu mawimbi yanapigana pigana, nyumba yangu iko kando ya ziwa. Asubuhi nakwenda kuvua ziwani, jioni narudi na samaki wengi. Bata na mayungiyungi vinaonekana ziwani, katika majira ya mpukutiko watu wanavuna mpunga mashambani."

    Huu ni wimbo maarufu unaojulikana kwa wachina wengi, unaelezea mandhari nzuri na mali nyingi za ziwa Honghu, ambalo ni ziwa la saba kwa ukubwa kati ya maziwa ya maji badiri nchini China, na pia ni ardhi oevu muhimu duniani. Lakini katika miaka ya 80 na 90 ya karne iliyopita mandhari hiyo nzuri ilitoweka kutokana na matumizi makubwa kupita kiasi, lakini sasa kutokana na juhudi za uokoaji ambazo zimekuwa zikifanywa hatua kwa hatua, zimefanya hali ya kawaida ianze kurejea.

    China ina eneo la zaidi ya hekta milioni 53 za ardhi oevu, ambalo ni eneo kubwa zaidi barani Asia, na la nne kwa ukubwa duniani. Mabadiliko ya ziwa Honghu pia yanaonesha ugumu ulioikabili China na maendeleo yaliyopatikana katika kuhifadhi ardhi oevu. Bw. Zhang Shengyuan mwenye umri wa miaka 58 anaishi kando ya ziwa Honghu, na aliwahi kuona mandhari ya asili ya ziwa hilo inayoelezewa katika wimbo. Anasema,

    "Wakati ule, maji ya ziwa Honghu yalikuwa ni mazuri zaidi hata kuliko maji ya chupa, na yalikuwa na ladha nzuri. Hata samaki walikuwa wengi, pia walikuwa na samaki bora ziwani, ambao kwa sasa wako kwenye hatari ya kutoweka."

    Hii ilikuwa ni mandhari ya ziwa Honghu katika miaka ya 50 na 60 ya karne iliyopita. Kuanzia miaka ya 80 ya karne iliyopita, watu wa maeneo ya karibu na ziwa Honghu walianza kuendeleza shughuli za ufugaji wa samaki, na baadhi ya wakulima waligundua kuwa biashara ya samaki ni nzuri, hivyo waliacha kilimo na kujihusisha na ufugaji wa samaki. Lakini uendelezaji kupita kiasi wa ufugaji wa samaki na uroho wa pesa kupita kiasi vimefanya ziwa Honghu libadilike. Bw. Zhang Shengyuan pia ameyaona mabadiliko hayo. Anasema,

    "Karibu ziwa hilo liharibike kabisa. Samaki walitoweka, na ndege pia walitoweka. Wavuvi wetu waliona magugu maji yanastawi ziwani, haijaharibiwa, wakaweka wigo na kufuga kaa, ingawa walipata faida kubwa, hatimaye majani yote ndani ya ziwa iliharibika, wakatumia dawa za kuua wadudu ambazo imesababisha maji ya ziwa Honghu yawe na harufu mbaya. Majani ziwani yalikauka yote. Wakati ule wavuvi kando ya ziwa hilo walikubwa na magonjwa, wengi wao walisumbuliwa na ugonjwa wa lithiasis."

    Takwimu zinaonesha kuwa, mwishoni mwa mwaka 2004, eneo la ufugaji kwenye ziwa Honghu lilifikia hekta zaidi ya elfu 25, ambalo lilichukua asilimia zaidi ya 70 ya ziwa hilo. Ufugaji kupita kiasi ulifanya ubora wa maji ya ziwa Honghu uzidi kuwa mbaya, na idadi ya kuku maji na samaki asili kwenye ziwa hilo ilipungua kwa kiasi kikubwa, na mimea ya majini ilikaribia kutoweka. Ili kukabiliana na hali hiyo, kuanzia mwaka 2005, mkoa wa Hubei ulianza kuchukua hatua za kuhifadhi ziwa Honghu, ikiwemo kuondoa wigo uliowekwa na wavuvi, kuwapanga wavuvi hao, na kuratibu mfumo wa usimamizi. Baada ya juhudi za miaka 10, ubora wa maji ya ziwa hilo umekuwa mzuri kiasi. Mkuu wa idara ya usimamizi wa ardhi oevu ya Honghu Zhu Junhua alisema,

    "Njia ya kwanza ya kuinua ubora wa maji ni kufunga ziwa, na kusimamia kwa ngazi tofauti. Watu husika wanapigwa marufuku kabisa kuingia katika maeneo muhimu, ambapo eneo la majaribio wanaweza kufanya uvuvi baada ya kuidhinishwa. Kwa kupitia njia hiyo tunapunguza kadiri tuwezavyo uchafuzi maji kutokana na shughuli za binadamu. Ya pili tunafufua eneo la ardhi oevu, na tumeondoa wigo ili kupunguza athari ya ufugaji wa kibinadamu kwa ubora wa maji. Ya tatu tunafanya usimamizi kwa ziwa zima, ili kupunguza utoaji wa uchafu. Aidha tunaimarisha usimamizi wa maji, na kuongeza nguvu ya uhamasishaji, ili kuimarisha mwamko wa watu kuhusu kuhifadhi mazingira. Kabla ya kufanya uhifadhi kwa ubora wa maji, ubora wa maji ya ziwa Honghu ulikuwa wa ngazi ya nne na tano, lakini baada ya juhudi za miaka 10, umefikia ngazi ya tatu na ya pili."

    Hivi sasa ingawa imeingia katika majira ya baridi, lakini bado unaweza kuona majani ya yungiyungi na matete katika ziwa Honghu; ingawa maji yake si safi sana, lakini hayanuki tena. Kuboreshwa kwa ubora wa maji na kufufuka kwa hali ya kiviumbe pia kunawanufaisha zaidi wavuvi. Mwaka 2005 serikali ilipoondoa wigo iliwapa wavuvi zaidi ya 2,000 kila mmoja hekta 1.33 za eneo la maji, na kupanga vizuri eneo la ufugaji. Mvuvi Wang Yunlian ni mmoja wa walionufaika, yeye aligundua kuwa faida kutoka kwenye hizo hekta 1.33, ni kubwa zaidi hata kuliko hekta 6.66 za zamani. Anasema,

    "Wakati ule hakukuwa na majani, hivyo hatukuweza kufuga kaa. Lakini baada ya kufufuka kwa hali ya kiviumbe tunaweza kufuga kaa na samaki aina ya mandarin fish. Mwaka jana mauzo yalikuwa mazuri, tuliuza samaki na kwa uchache tulipata Yuan elfu 30, hata tuliweza kupata Yuan elfu 60 au 70. Ikilinganishwa na hekta 6.66 za zamani, ambapo tulifuga kambale, ambao faida yake si kubwa. Wakati ule kambale waliuzwa kwa Yuan 2.4 tu kwa kilo, lakini kaa kwa uchache waliuzwa kwa Yuan 40 au 60 kwa kilo, hata waliuzwa kwa Yuan 200 kwa kilo, mazingira yanayofufuka na kuboreshwa yanafaa kufanya ufugaji maalum."

    Kuliko njia ya zamani ya uendelezaji, hivi sasa watu wa ziwa Honghu wanazingatia zaidi kuendeleza ziwa hilo kwa kuunganisha maslahi ya uchumi na maslahi ya hali ya viumbe. Bustani ya ikolojia ya Lantian iko kaskazini magharibi mwa ziwa Honghu, ni sehemu ya utalii wa kiikolojia. Bustani hiyo imegundua kuwa maua ya yungiyungi ni maalum katika ziwa Honghu, hivyo inaingiza aina mbalimbali za maua ya yungiyungi kwa ajili ya watalii, wakati huohuo inaendeleza opera ya huko ya ngoma ya wavuvi ya ziwa Honghu, na kuwaajiri wanakijiji wa huko kufanya maonesho, hatua ambayo si kama tu inaunganisha utamaduni na mandhari ya maumbile, bali pia inatoa fursa kwa wanakijiji wa huko kupata mapato zaidi. Mwanakijiji mmoja Bw. Chen amesema,

    "Nimefanya kazi hapa kwa nusu mwaka. Katika siku za kawaida, nalima na kufuga samaki, na ninatumia muda mdogo kufanya maonesho hapa, ili kuongeza kidogo mapato. Kila mwezi naweza kupata Yuan zaidi ya 2,000."

    Mkuu wa idara ya usimamizi wa ardhi oevu ya Honghu Zhu Junhua amesema, matumizi ya ziwa Honghu lazima yafuate kanuni ya kulihifadhi kwanza, halafu kutafuta njia za uendelezaji kwa utaratibu katika uhifadhi wa kisayansi. Bw. Zhu anasema,

    "Uhifadhi na matumizi ni mambo yanayofuatiliwa, kwa sisi kwanza tunapaswa kushikilia kanuni ya kutoa kipaumbele uhifadhi. Kwa ziwa Honghu jambo ambalo kama linaendelezwa kwa kuharibu kazi ya uhifadhi, basi kamwe haliwezi kufanywa. Wakati huohuo katika mchakato wa uendelezaji, lazima tufanye mpango wa kisayansi. La tatu ni kuhakikisha kuendeleza ujenzi unaosaidia sehemu ya uhifadhi, na uhifadhi wa hali ya viumbe. Kwa mfano, uendelezaji wa bustani ya kiikolojia ya Lantian, ingawa tunafanya uendelezaji, lakini tunapoendeleza tunapaswa kutumia vizuri jukwaa hili, ili kulifanya litusaidie kutangaza uhifadhi wa hali ya viumbe, na tunaliendeleza kwa utaratibu chini ya uhifadhi wa kisayansi."

    Katika miaka 10 iliyopita, ubora wa maji na hali ya viumbe ya ziwa Honghu imefufuka hatua kwa hatua, na sura ya ziwa Honghu katika miaka 10 ijayo itakuwaje? Wasimamizi wa ziwa hilo wamekuwa na mpango. Bw. Zhu Junhua anasema,

    "Ya kwanza ni kudumisha eneo la sasa, ya pili ni kufanya ubora wa maji ya ziwa hilo ufikie kiwango cha II, na baadhi ya sehemu ya ziwa hilo hata kufikia kiwango cha I; ya tatu ni kuinua idadi na ubora wa wanyama pori na mimea pori, ili kulifanya ziwa Honghu kuwa pepo kwa wanyama pori na mimea pori, ya nne ni kufikia mapatano kati ya binadamu na maumbile, yaani kufanya shughuli za binadamu na uhifadhi wa hali ya viumbe viendane. Nadhani kwa juhudi za miaka 10 tutaweza kupata mafanikio zaidi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako