• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kijana wa Misri anayetimiza ndoto yake mkoani Ningxia, China

    (GMT+08:00) 2016-01-13 14:30:03

    Bw. Ahmed Saeed kutoka Misri mwanzoni alikuja China kutokana na makubaliano ya kazi ya miezi mitatu tu, lakini miaka mitano imepita, na bado hana mpango wa kurudi Misri. Labda hata yeye mwenyewe hakufikiria kwamba mkoa wa Ningxia si kama tu umekuwa maskani yake ya pili, bali pia umekuwa mahali ambapo amejitahidi kutimiza ndoto yake.

    "Vitabu vya Kingereza, nitawatafutia mashirika ya uchapishaji wa vitabu vya kichina na kingereza, wao pia wanataka kuchapisha vitabu hivyo, lakini ninyi hapa mnachapisha vitabu vya kiarabu tu."

    Kwenye ofisi moja iliyoko ghorofa ya tano ya jengo la ofisi huko Yinchuan, mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa kabila la wahui wa Ningxia, mmisri Ahmed Saeed alikuwa akiongea kwa kichina na mhariri Bw. Liu Yiwei wa shirika la uchapishaji la huko kuhusu kazi ya kutafsiri na kuchapisha kitabu kimoja. Bw. Liu Yiwei anasema,

    "Tumeshirikiana naye kwa muda mrefu katika kutafsiri na kuchapisha vitabu kati ya lugha za kiarabu na kichina, naona yeye ni kama daraja moja kati ya tamaduni za China na nchi za kiarabu."

    Bw. Ahmed Saeed mwenye umri wa miaka 32 alihitimu kwenye chuo kikuu cha Azhar cha Misri mwaka 2005, na ni mmoja ya wahitimu wa awamu ya kwanza wa masomo ya lugha ya kichina katika chuo kikuu hicho.

    "Naona wachina wanachukua asilimia 20 ya idadi ya jumla ya watu duniani, lakini hatujawafahamu sana, kwa hiyo nimeanza kujifunza Kichina ili kuweza kuwafahamu vizuri."

    Mwaka 2010, Bw. Saeed ambaye alikuwa mwongozaji watalii kwa lugha ya kichina huko Dubai, alialikwa kwenda mkoani Ningxia kwa kazi ya kutafsiri na kusahihisha tovuti rasmi ya kiarabu ya Baraza la kwanza la uchumi kati ya China na nchi za kiarabu. Muda wa kazi hiyo ulikuwa ni miezi mitatu.

    "Kabla ya kuja hapa, sikuwahi hata kusikia kama kuna sehemu inayoitwa Ningxia nchini China, baada ya kukaa kwa miezi mitatu nikaona hapa kweli pana mustakbali mzuri wa maendeleo, lakini si ya kiuchumi na kibiashara, bali hata kwa upande wa kiutamaduni."

    Mwezi Septemba mwaka 2011, Bw. Saeed na vijana wawili wa China walianzisha kwa pamoja kampuni ya huduma za kiutamaduni ya Wisdom Palace, inayoshughulikia kazi za kutafsiri na kuchapisha vitabu kwa lugha za kichina na kiarabu, pamoja na mafunzo ya lugha ya kiarabu. Bw. Saeed anasema, mkoa wa Ningxia umebadili maisha yake.

    "Ningxia, hasa baadhi ya sehemu za kusini, ukienda huko unaweza kujihisi kama umefika katika nchi za kiarabu, tofauti ya pekee ni lugha ya kichina tu, wala si Kiarabu. Lakini tabia zao, pamoja na sherehe za kidini na mikahawa yote ni ya kiislamu, kweli najisikia kama niko nyumbani kabisa."

    Ni muda mfupi tu, lakini Bw. Saeed amezoea maisha ya Ningxia kama mwenyeji, na amekuwa mgeni wa kwanza kununua gari lake binafsi mkoani humo.

    "wakati ninapoenda safari za kikazi, nikisema nataka kurudi nyumbani, wanajua namaanisha kurudi mjini Yinchuan, sasa Yinchuan imekuwa maskani yangu ya pili. Nafurahia maisha ya kila siku mkoani Ningxia. Jamaa zangu wananitania mara kwa mara kwamba muda wako wa miezi mitatu utamalizika lini? utarudi lini? Na huwa nawajibu hata mimi pia sijui."

    Bw. Saeed amesema anataka kuwafahamisha waarabu wengi zaidi kuhusu utamaduni wa China na kujua hali halisi ya China.

    "Naona hata maendeleo ya utamaduni pia yanaenda sambamba na maendeleo ya uchumi, kama nikiwa nakujua vizuri, basi wewe pia utanifahamu sana, na hapo ushirikiano kati yetu utakuwa mzuri, kama marafiki tu."

    Si kuongea tu, Bw. Saeed pia anatumia kichina kutuma ujumbe wa SMS kuandikia barua pepe. Anasema, asilimia 90 ya muda wake kila siku anatumia lugha ya kichina. Katika muda wa zaidi ya miaka minne, kundi linaloongozwa na Bw. Saeed limemaliza kazi ya kutafsiri na kuchapisha vitabu zaidi ya 560 vya kichina na kiarabu. Mwezi Agosti mwaka jana, Bw. Saeed alipewa tuzo ya mchango maalumu kwa sekta ya vitabu ya China na Idara kuu ya uchapishaji habari na usimamizi wa radio, filamu na televisheni ya China. Naibu maneja mkuu wa kampuni ya Wisdom Palace Bw. Zhang Shirong amesema,

    "kampuni yetu inachapisha zaidi ya asilimia 70 ya vitabu vya kichina vinavyotafsiriwa kwa kiarabu na kutolewa kwenye soko la nchi za kiarabu, na kampuni yetu pia inachangia asilimia 90 ya vitabu vyote vinayopatikana kwenye soko la nchi za kiarabu."

    Kutokana na kupanuliwa kwa biashara yake, hivi sasa mashirika mengi ya uchapishaji na waandishi mashuhuri wa vitabu wanakwenda kutafuta ushirikiano na kampuni yao. Bw. Zhang Shirong anasema,

    "Mapato ya kampuni yetu yanaongezeka maradufu kila mwaka, haswa kutoka mwaka jana hadi mwaka huu, hadi sasa tumetimiza ongezeko la mapato kwa asilimia 150."

    Kwa upande wa Bw. Ahmed Saeed, amesema faida ya kiuchumi si lengo la kwanza kwenye sekta ya utamaduni.

    "Kitu tunachofikiria sio kwamba kitabu hiki kinauzwa kwa bei gani, kwa mfano wa kitabu hiki kinachotolewa leo hii, nahisi kama mtoto wangu, najivunia sana. Kwa sasa napenda kuifahamisha China kwa dunia nzima, ili waweze kuipenda moyoni."

    Mwaka 2014, Bw. Ahmed alitembelea wataalamu na wasomi wa sekta ya uchapishaji nchini China, na aliandika kitabu kiitwacho "Njia ya China: Miujiza na Siri zake" ambacho kiliuza nakala zaidi ya elfu 10. Kwa kawaida katika nchi za kiarabu, kitabu kikiweza kuuza nakala elfu tatu basi ni mafanikio. Kitabu hicho kilifika hadi kuhukuliwa kama zawadi ya kitaifa na kupeana kati ya viongozi wa China na nchi za kiarabu.

    Mkakati wa Ukanda mmoja na Njia moja umemsaidia Bw. Saeed atimize ndoto yake. Mbali na shughuli za sasa, pia anapanga kutoa nakala za kielektroniki za vitabu vya kichina na kiarabu, na kushiriki kwenye kazi ya kutafsiri filamu na tamthilia za kichina, ili kuonesha uhalisi wa China kwa pande zote kwa dunia ya kiarabu.

    "Wakati nilipoanzisha kampuni ya kwanza nchini Misiri, niliipatia jina Njia mpya ya hariri. Ndoto yangu kubwa ni kuweza kuona waarabu na wachina wanaimarisha zaidi ushirikiano wa kiutamaduni mbali na ushirikiano wa kiuchumi, pande hizo mbili zinaweza kuelewana, kusaidiana na kufundishana, na kuunganisha sehemu zote za China zilizoko kwenye njia ya hariri na nchi zote za kiarabu zilizo kwenye njia hiyo kwa kupitia mawasiliano ya kiutamaduni."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako