• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • AIIB yalenga kupaza sauti za nchi zinazoendelea katika kusimamia uchumi wa dunia

    (GMT+08:00) 2016-01-27 10:29:08

     


    Tangu msukosuko wa fedha duniani utokee mwaka 2008, uchumi wa dunia na muundo wa kifedha vimeshuhudia mabadiliko makubwa, na kufuatia kupungua kwa ongezeko la uchumi wa dunia, nchi nyingi zinazoendelea zimekabiliwa na changamoto kubwa katika kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, kazi ambayo inahusu maendeleo ya uchumi katika siku za baadaye, na pia utaratibu wa kifedha duniani unahitaji marekebisho mapya. Katika mazingira hayo, Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia AIIB ilianzishwa.

    Hivi sasa, Benki ya Dunia ni chombo kikuu cha kusimamia uchumi wa dunia, na benki za maendeleo za kikanda zinatumika kama vyombo vya utendaji. Utaratibu uliopo wa kusimamia uchumi wa dunia unaongozwa zaidi na Marekani, nchi kadhaa za Ulaya magharibi, Japan na nchi nyingine zilizoendelea, ambapo sauti za nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo China hazisikiki, na uwiano unakosekana katika mgao wa maslahi katika muundo wa utaratibu huo.

    AIIB ni benki ya maendeleo ya pande nyingi barani Asia, mtaji wake wa usajili ni dola za kimarekani bilioni 100, makao makuu yako hapa Beijing, na inaangazia kuunga mkono ujenzi wa miundombinu barani Asia. Tangu rais Xi Jinping wa China apendekeze kuanzishwa kwa Benki hiyo mwezi Oktoba mwaka 2013, hadi sherehe za uzinduzi rasmi zifanyike katikati ya mwezi huu, katika miezi 27 iliyopita, AIIB ilipata uungaji mkono mkubwa na ushiriki mpana wa nchi mbalimbali duniani, na hadi sasa imekuwa na nchi wanachama waanzilishi 57. Afisa wa taasisi ya utafiti wa uchumi kwa nje iliyo chini ya Kamati ya Kitaifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China Zhang Jianping anaona kuwa, kuanzishwa kwa AIIB kunaendana na mahitaji ya nchi nyingi duniani, na benki hiyo inaungwa mkono na pande mbalimbali. Anasema,

    "Kwa upande mmoja, baada ya kujiunga na AIIB, nchi hizo zitaweza kuungwa mkono kifedha na AIIB katika siku za baadaye ili kuboresha miundombinu, mazingira ya kibiashara na uwekezaji na kuvutia zaidi mtaji wa kigeni. Kwa upande mwingine, ushirikiano wa kiutaratibu kama vile AIIB unaweza kuweka mazingira mazuri kwa ushirikiano mpana na maendeleo ya kikanda katika siku zijazo."

    Mambo ya fedha ni roho na msingi wa uchumi wa kisasa. Kabla ya hapo, China, ikiwa mshiriki, ilijiunga na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Asia, na kuanzisha AIIB ni mara ya kwanza kwa China kutunga kanuni katika kujihusisha kwenye usimamizi wa uchumi wa dunia. Hii sio tu inapaza sauti ya nchi zinazoendelea katika kusimamia uchumi wa dunia, bali pia inaonesha kuwa China inabeba wajibu zaidi wa kimataifa. Bw. Zhang anasema,

    "Tumefuata msimamo wa kushauriana, kujenga na kufaidika kwa pamoja, hii inaonesha kuwa bila kujali ni nchi kubwa ama ndogo, tuna uhusiano wa usawa na ushirikiano, na ushirikiano wetu unahimizwa katika msingi wa uwepo wa makubaliano. Wazo la ushirikiano kama hilo ni mwelekeo wa maendeleo ya dunia kwa sasa."

    Mkuu wa AIIB Bw. Jin Liqun

    Aidha, uzoefu pekee ulio nao China katika ujenzi wa miundombinu pia ni sababu zilizohamasisha nchi nyingi kujiunga na AIIB. Mtafiti wa ngazi ya juu wa Chuo Kikuu cha Cambridge cha Uingereza Martin Jacques amesema kama duniani kuna mtaalam pekee wa ujenzi wa miundombinu, huyo ni China, kwani China ina uelewa mpana kuhusu sekta hiyo.

    Mwezi Aprili mwaka jana, nchi 57 ziliidhinishwa kuwa wanachama waanzilishi wa AIIB, kati yao 37 ni nchi za Asia na nyingine 20 ni kutoka nje ya Asia. Tarehe 29 Juni, sherehe za kusaini kanuni za AIIB zilifanyika hapa Beijing, ambazo zimechukuliwa kuwa ni sheria kuu ya uendeshaji wa Benki hiyo. Kwa mujibu wa kanuni hizo, China inachukua asilimia 30.34 ya hisa, asilimia 26.06 ya haki ya kupigia kura, na kuwa nchi yenye hisa nyingi na haki kubwa zaidi ya kupigia kura.

    Tarehe 25, Disemba mwaka jana, nchi 17 wanachama waanzilishi waliidhinisha kanuni hizo na kuwasilisha vitabu vya idhini, hisa walizo nazo zilichukua asilimia 50.1, kiasi ambacho kilifikia sharti la uendeshaji, ambapo AIIB ilizinduliwa rasmi. Waziri wa fedha wa China Lou Jiwei anasema,

    "Hili ni tukio kubwa katika mageuzi ya utaratibu wa kusimamia uchumi wa kimataifa, AIIB ikiwa chombo kipya cha kuhimiza maendeleo kinachoshirikisha pande nyingi, imeingia kwenye utaratibu uliopo sasa wa maendeleo ya pande nyingi."

    Hata hivyo, mafanikio yaliyopatikana katika maandalizi ya AIIB yalikuwa ni hatua ya kwanza katika safari ndefu. Ikiwa benki ya uwekezaji wa miundombinu, jinsi ya kukidhi madai ya maslahi ya nchi mbalimbali wananachama, na jinsi ya kutoa mkopo wa fedha kwa usalama na ufanisi ni masuala yanayofuatiliwa zaidi. Kuna tofauti kubwa kati ya AIIB na Benki ya Dunia au Benki ya Maendeleo ya Asia. Madhumuni ya China kupendekeza kuanzishwa kwa AIIB sio kubadili utaratibu uliopo sasa, bali ni kutoa nyongeza na ujenzi wa utaratibu huo. Kwa mfano, Benki ya Dunia, ilitoa msaada na mkopo wa dola za kimarekani bilioni 61 kwa nchi zinazoendelea kwa mwaka wa bajeti wa 2014, lakini kati ya fedha hizo, ni dola bilioni 24 tu iliyohusika na miundombinu, kiasi ambacho kilikuwa ni kidogo sana ikilinganishwa na hitaji halisi la dola trilioni 1.5. Mkuu wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim anasema,

    "Kundi lolote linalohimiza utatuzi wa tatizo la umaskini kwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ni rafiki, naona AIIB itakuwa mmoja kati ya wenzi wanaowekeza kwenye ujenzi wa miundombinu duniani, jambo ambalo lina maana kubwa. Uanzishwaji wa AIIB unatokana na ukosefu wa uwekezaji katika miundombinu, wala hauna lengo la kisiasa, Benki ya Dunia sio shirika la kisiasa."

    Kwa mujibu wa makadirio ya Benki ya Dunia, katika miaka kumi ijayo, dola za kimarekani trilioni 8 zinahitajika katika sekta ya miundombinu barani Asia, lakini Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Asia ambazo zinalenga zaidi kupunguza umaskini hazitaweza kukidhi mahitaji hayo. Wakati huohuo, baada ya uendeshaji wa miaka mingi, benki hizo mbili zimelalamikiwa kutokana na ufanisi mdogo. Katika mashirika hayo, kutoka kupitishwa kwa mradi fulani hadi kusanifiwa, kufanyiwa utafiti na kutolewa ripoti, mchakato huo unachukua muda wa miaka mitatu hadi minne, lakini baada ya muda huo, nchi nyingi zilizotoa madai zimekuwa na matatizo mapya. Mtafiti wa taasisi ya uhusiano wa kimataifa wa kisasa ya China Chen Fengying anaona kuwa,

    "Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Asia na Benki ya Ujenzi na Maendeleo ya Ulaya zote ni mifano tunayopaswa kuiga, kwani wao wana uzoefu mwingi wenye mafanikio. Kwa upande mwingine, AIIB ina muundo safi wa kiutawala, na pia katika mashirika mengi ya kimataifa, nafasi za uongozi zinagawanywa kwa mujibu wa kiasi cha hisa ilizo nazo nchi mwanachama, na nchi wanachama wote wana wajumbe katika ngazi ya kiutawala. Lakini maofisa wakuu wa AIIB waliajiriwa kutoka dunia nzima, wao si wa kudumu, bali ni wa kuteuliwa, na wanawakilisha maslahi ya AIIB."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako