• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw John Kerry afanya ziara nchini China

    (GMT+08:00) 2016-01-28 10:49:19

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. John Kerry jana aliwasili hapa Beijing kutokana na mwaliko wa mwenyeji wake Bw Wang Yi. Kwenye ziara hii Bw Kerry na wenyeji wake wanatarajia kujadili suala la nyuklia la peninsula ya Korea, Bahari ya Kusini ya China, na suala la Taiwan.

    Tangu mwaka huu uanze, kumekuwa na matukio mengi makubwa yanayoathiri amani na utulivu wa kikanda ikiwemo kusimamishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Saudi Arabia na Iran na jaribio la nne la nyuklia la Korea ya Kaskazini. Bw. Kerry anafanya ziara nchini China wakati vyombo vya habari duniani vimekuwa vinafuatilia kama China na Marekani zinaweza kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja. Kwenye mkutano kati ya Bw. Kerry na rais Xi Jinping wa China, rais Xi amesisitiza kuwa, kama China na Marekani zitaimarisha ushirikiano, basi zinaweza kufanya mambo mazuri yanayosaidia dunia. Rais Xi anasema,

    "Kwa ujumla, kama China na Marekani zikifanya juhudi za pamoja zinaweza kufanya mambo mazuri yanayonufaisha nchi hizo mbili, na kuhimiza amani, ustawi na utulivu wa dunia. Tunapenda kuendelea kushirikiana na Marekani na rais Barack Obama ili kuendelea kujenga uhusiano wa aina mpya wa kutopambana, kuheshimiana na kunufaishana."

    Siku hiyohiyo, waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi pia alifanya mazungumzo na Bw. Kerry, na baadaye kukutana na waandishi wa habari. Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Bw. Wang Yi alisema, wamekubaliana kuwa China na Marekani zinapaswa kuendelea kutekeleza matunda mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa ziara ya rais Xi nchini Marekani, kudumisha mawasiliano ya viongozi wa nchi hizo mbili, na kushauriana kwa wakati juu ya masuala makubwa yanayofuatiliwa kwa pamoja. Kuhusu suala la Taiwan, Bw. Wang Yi anasema,

    "Nasisitiza kuwa suala la Taiwan ni suala kubwa linaloathiri uhusiano kati ya nchi zetu. Bila kujali ni mabadiliko gani yanayotokea huko Taiwan, ukweli ni kwamba kuna China moja tu duniani na haubadiliki na hautabadilika. Ni lazima Marekani itekeleze ahadi yake ya kushikilia sera ya kuwepo kwa China moja duniani, kufuata Taarifa tatu za pamoja zilizotolewa na China na Marekani, na kupinga "Taiwan kujitenga na China", na kuchukua hatua za kivitendo za kuhimiza uhusiano kati ya China bara na Taiwan uendelezwe kwa amani."

    Bw. Kerry amesisitiza kuwa, Marekani inashikilia sera ya kuwepo kwa China moja, haiungi mkono "Taiwan kujitenga na China", na kuunga mkono China bara na Taiwan kuendelea na mazungumzo.

    Kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea, Bw. Wang amesema, utatuzi wa suala hilo unapaswa kushikilia kutimiza lengo la kutokuwa na silaha za nyuklia katika peninsula ya Korea, kulinda amani na utulivu wa peninsula hiyo, na kutatua suala kupitia mazungumzo. Na kuhusu suala la Bahari ya China Kusini, Bw. Wang anasema, tangu zamani visiwa vya Bahari ya Kusini ni ardhi ya China. Vifaa vya ulinzi vya lazima vya China ni kwa ajili ya kujilinda, havihusiani na "mambo ya kijeshi".

    Bw. Kerry amesema, uhusiano kati ya Marekani na China ni muhimu, na nchi hizo mbili zina maslahi mengi ya pamoja katika mambo ya kimataifa. Marekani inakubali kuwa ushirikiano kati yake na China unaweza kuhimiza utatuzi wa masuala mengi duniani. Bw. Kerry anasema,

    "ushirikiano kati ya Marekani na China umefanya kazi muhimu katika masuala mengi,. Nadhani katika mambo ya kidiplomasia ya kimataifa, Marekani na China zikiweza kushirikiana, zitaweza kupata maendeleo, na kufanya maisha ya watu yawe mazuri zaidi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako