Takwimu mpya zilizotolewa hivi karibuni na wizara ya fedha ya China zinaonesha kuwa mwaka jana mapato ya serikali ya China yaliongezeka kwa asilimia 8.4, ambayo ni kiwango cha chini zaidi tangu mwaka 1988.
Wizara ya fedha ya China imesema, kupungua kwa ongezeko la mapato ya serikali kunatokana kupungua kwa ukuaji wa uchumi na biashara na nje, kushuka kwa uzalishaji viwandani na sera za kupunguza kodi. Profesa Hu Yijian wa chuo kikuu cha uchumi na fedha cha Shanghai amesema,
"Mwaka jana kutokana na sera za kupunguza kiwango cha kodi, kwa ujumla kodi yenye thamani ya yuan bilioni 200 imepunguzwa, pamoja na hatua nyingine za kupunguza kodi kwa makampuni madogo na yenye ukubwa wa kati, na yale yanayofanya uvumbuzi."
Takwimu kutoka idara za kodi zinaonesha kuwa mwaka jana kwa ujumla China ilipunguza kodi zaidi ya yuan bilioni 300 kwa makampuni mapya na yanayofanya uvumbuzi. Akizungumzia hali hiyo naibu mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa sera za kifedha katika wizara ya fedha ya China Bw. Bai Jingming amesema,
"hatua hizo zinalenga kuongeza nguvu ya msukumo kwa ukuaji endelevu wa uchumi katika siku zijazo, hasara za sasa hatuwezi kukwepa, zote hizo ni kwa ajili ya maendeleo endelevu katika siku za baadaye."
Bw. Bai Jingming pia amesema, kwa upande wa gawio la kodi na kasi ya ongezeko la kodi, sekta ya huduma na ya teknolojia ya hali ya juu zinachukua asilimia kubwa zaidi, hali ambayo inaonesha mabadiliko yanayotokea kwenye muundo wa uchumi wa China.
"Kwa mujibu wa takwimu za mapato ya kodi ya mwaka jana, tunaweza kuona kwamba sekta ya teknolojia ya hali ya juu inachangia zaidi mapato ya kodi, na mchango wa sekta ya huduma pia umeongezeka. Mwaka jana, sekta ya huduma ilichangia asilimia 54 ya mapato ya kodi, kwa hiyo China inapaswa kuendelea kusukuma mbele marekebisho ya muundo wa viwanda, na kuhimiza ongezeko la mapato ya kodi kupitia marekebisho hayo."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |