Msemaji wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya China Bw. Zhao Chenxin amesema, China ina uwezo wa kudumisha utulivu wa kiwango cha ubadilishaji cha RMB, na kwamba hatua za kudhibiti uzalishaji kwenye sekta ambazo uzalishaji wake umezidi mahitaji ya soko hazitasababisha mkondo mkubwa wa kupunguza wafanyakazi katika sekta hizo.
Hivi karibuni kiwango cha ubadilishaji wa sarafu ya China RMB kiliyumba, hali ambayo imefuatiliwa sana kwenye jamii. Akizungumzia suala hilo, msemaji wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya China Bw. Zhao Chenxin amesema, China ina uwezo wa kuendelea kudumisha utulivu wa kiwango cha ubadilishaji wa RMB.
"Kwanza, China bado ni nchi yenye akiba kubwa zaidi ya fedha za kigeni duniani; Pili, China bado inadumisha urali mzuri katika biashara na nje kila mwaka; Tatu, China bado inaendelea kuhimiza RMB iwe sarafu ya kimataifa; Nne, kiwango cha ubadilishaji wa RMB bado kinadumisha hali mpya ya kawaida ambayo kinaweza kuyumba kiasi juu na chini kwenye kiwango mwafaka."
Kabla ya hapo, mkurugenzi wa benki kuu ya China Bw. Zhou Xiaochuan pia alitoa maoni sawa kuhusu suala hilo. Alisema hivi sasa biashara ya China na nje iko katika hali nzuri, nguvu ya China kwenye ushindani wa kimataifa bado ni kubwa, mtiririko wa mitaji kati ya nchi uko kwenye kiwango cha kawaida, kiwango cha ubadilishaji wa RMB kwa jumla kimedumisha utulivu, na hakina msingi wa kudidimia.
Kuhusu wasiwasi wa kutokea kwa mkondo mpya wa kupunguza wafanyakazi, haswa kwenye sekta za makaa ya mawe na chuma cha pua, ambazo zinafanyiwa marekebisho ya kudhibiti uzalishaji, Bw. Zhao Chenxin anaona, kutokana na utendaji wa sasa wa uchumi wa China, mkondo huo hauwezi kutokea.
"Kwanza, uchumi wa China umeendelea kukua kwa utulivu, na kudumisha ongezeko la kasi, ambalo litaendelea kutoa mchango wa kuongeza ajira. Pili, utekelezaji wa mkakati wa kuhimiza uanzishaji biashara na kufanya uvumbuzi, utaendelea kusaidia kuboresha hali ya ajira. Tatu, soko la nguvu kazi nchini China liko kwenye hali nzuri, ambayo nguvu kazi inahamahama kwa urahisi ili kutafuta ajira. Nne, serikali kuu ya China inatilia maanani sana suala la ajira, na imetoa hatua mbalimbali za kuwapanga upya wafanyakazi waliopunguzwa kutoka kwenye sekta zenye uzalishaji unaozidi mahitaji ya soko."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |