• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tamasha la ngonjera za jadi za kichina la Majie lenye historia ya miaka 700

    (GMT+08:00) 2016-02-26 13:08:58

    Ijumaa iliyopita wakati sherehe za mwaka mpya zilipokaribia kumalizika kwenye sehemu nyingi nchini China, tamasha kubwa la ngonjera za jadi za kichina la kusherehekea mwaka mpya lilizinduliwa kwenye wilaya ya Baofeng mkoani Henan, katikati ya China.

    Mamia ya wasanii wa ngonjera ya jadi ya kichina walikusanyika kwenye mashamba ya kijiji cha Majie katika wilaya ya Baofeng, wakipiga ala mbalimbali za jadi na kuimba ngonjera za aina mbalimbali kuhusu hadithi za kale. Hili ndilo tamasha la ngonjera za jadi la Majie lenye historia ya miaka 700.

    Tamasha hilo linalojumuisha ngonjera na opera za jadi za sehemu mbalimbali zikiwemo mikoa ya Henan, Sichuan, Shandong, Hunan na Jiangsu, ni kama kumbukumbu ya kihistoria, na limeendelea kufanyika kila mwaka tangu enzi ya Yuan miaka zaidi ya 700 iliyopita hata kulipokuwa na vita au maafa, ndiyo maana tamasha hilo linasifiwa kuwa ni moja ya mambo 10 muhimu ya jadi ya kichina, na kuchukuliwa kwenye kundi la kwanza la mali za urithi wa kiutamaduni wa China.

    Msanii mashuhuri wa ngonjera wa China Bw. Liu Lanfang amefichua siri zilizofanya tamasha la ngonjera la Majie liweze kuendelea kufanyika na kustawi kwa miaka 700 mfululizo.

    "Kwanza, nchini China kuna sehemu hii moja tu inayorithi utamaduni huu, kurithi usanii wa ngonjera za jadi kwa miaka 700, hii ni sehemu ya kwanza na ya pekee; Pili ni wakazi wa hapa wanaopenda na kutunza sanaa hiyo. Zamani wakati wa sherehe za kuabudu miungu, au kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mama, kusherehekea mtoto kutimiza siku 100, wasanii wa ngonjera walialikwa kuja hapa, haijalishi wanatoka mikoa ya Hubei, au Liaoning, au Shandong, au Henan, walipokuja, familia zilizowapokea zilisafisha nyumba na kuchinja mbuzi ili kuwakaribisha, hali hiyo inamaanisha kwamba hapa kuna wapenzi wa ngonjera, na haikuwa rahisi kwa shauku hii kuendelea kwa kipindi chote cha miaka 700; mwishowe ni uungaji mkono wa viongozi wa hapa, mwanzoni ulikuwa ni wa kiraia, baadaye ukawa wa kiserikali, kwa nini? ni kwa kuwa hivi sasa sanaa na burudani mbalimbali zimeendelea sana na kujitokeza, kama vile filamu, tamthiliya za televisheni, pamoja na mtandao wa Internet, ukitaka chochote utapata tu, kwa hiyo serikali ya hapa kuendelea kuunga mkono sanaa hii ya jadi, kweli si rahisi. Katika miaka zaidi ya 30 iliyopita, nikipata nafasi nitakuja kwenye tamasha hilo."

    Kwenye tamasha la mwaka huu, wasanii wapatao elfu moja kutoka mikoa zaidi ya 20 nchini China walipanda jukwaani kuonesha ustadi wao wa kuimba ngonjera za jadi za kichina, na kugombea ubingwa wa tamasha hilo. Bingwa wa mwaka jana Bi. Li Dongmei amekuwa na umri wa miaka 60, na bado ameendelea kuimba ngonjera jukwaani. Akizungumzia mvuto wa tamasha hilo amesema, muhimu zaidi ni jukwaa la kushindana ustadi wa kisanii.

    "Kinachonivutia zaidi ni utamaduni wa kale wa tamasha la ngonjera la Majie. Baada ya kuja hapa, wasanii wamekuwa pamoja na kushindana ustadi wa kisanii. Baada ya maonesho ya mchana, wasanii wote hukaa pamoja usiku na kuwa na fursa za kufundishana. Kwa nini sitaki kukaa hotelini? Napendelea kukaa kwenye vituo vya kupokea wasanii, ili niweze kuwasiliana na wasanii wengine. Huu ni upande mmoja. Kwa upande mwingine, hapa kuna watazamaji wengi, kama hali ya afya ikiniruhusu, nitakuja kila mwaka!"

    Wasanii wamekusanyika kutoka sehemu mbalimbali kwa lengo moja tu, yaani kuonesha ustadi wao wa kisanii, ili kuwafahamisha watu wengi zaidi kuhusu usanii wao. Bw. Zhao Jianguo kutoka tarafa ya Shiqiao ya wilaya ya Baofeng ameshiriki kwenye tamasha hilo kila mwaka kwa miaka zaidi ya 10. Safari hii aliandaa ngonjera ya mtindo wa mkoa wa Henan. Akizungumzia lengo lake la kushiriki kwenye tamasha hilo, anasema,

    "Mimi ni mkulima, napenda kuimba ngonjera baada ya kazi. Wakati wa kipindi cha sikukuu ya mwaka mpya, hapa katika maskani yangu, tunaimba bila malipo kuwatumbuiza watazamaji."

    Kwenye tamasha hilo, wasanii wamejitahidi kuonesha ustadi wao, wapenzi wa ngonjera pia wamefurahi sana. Katika kijiji cha Majie ambacho tamasha hilo lilifanyika, watu wengi walikuwa wanasongamana kila mahali mitaani, na mzee Qiao na mke wake walikuwa miongoni mwa wapenzi hao wa ngonjera za jadi. Mzee Qiao amesema amesafiri kilomita 200 kwa ajili ya kushiriki kwenye tamasha hilo.

    "natoka wilaya ya Fangcheng, umbali wa kilomita 200 kutoka hapa. Niliwahi kusikia tamasha maarufu la ngonjera za jadi la Majie, kwa hiyo safari hii tumekuja kulitazama. Kweli ni zuri sana. Siondoki leo, kesho pia nitaendelea kutazama. Baada ya kurudi nitawaambia wenzangu na marafiki zangu kuhusu tamasha hili, mwaka kesho tuje wote pamoja!"

    Upendo wa watu wa huko kwa sanaa hiyo sio kama tu ni kupenda kutazama maonesho, bali pia unaonekana katika ukarimu wao kwa wasanii. Wanakijiji wa kijiji cha Majie na wakazi wa maeneo ya karibu huwatendea wasanii wa ngonjera kama marafiki na ndugu zao, wakiwapokea nyumbani na kuwakaribisha kwa chakula kizuri bila malipo yoyote, na wasanii pia wanajiona kama wako nyumbani tu, na kuimba ngonjera bila malipo kuwatumbuiza watazamaji. Hali hiyo imekuwa desturi maalumu ya jadi kwenye eneo la Majie. Watu wa huko husema, sherehe ya mwaka mpya inaweza kuwa ndogo, lakini ni tamasha la ngonjera za jadi lazima liwe kubwa. Upendo wao kwa sanaa hiyo na ukarimu kwa wasanii, pia vimewapatia wasanii wa ngonjera hisia maalumu kuhusu eneo la Majie.

    Kwenye tamasha la mwaka huu, msanii kutoka Ujerumani Bw. Bo Renrui aliimba ngonjera yake iitwayo "Mwenyeji wa Beijing", akishangiliwa sana na watazamaji.

    Mara baada ya kumalizika kwa maonesho ya Bw. Bo, sauti ya kijana ikaanza kusikika mara moja, kama akiwa mashindanoni.

    Ndio, ni kama msanii mashuhuri wa ngonjera za jadi za kichina Bw. Liu Lanfang alivyosema,

    "Hakuna mahangaiko ya kurithi sanaa hiyo, wacha iendelee kama kawaida, wafuasi na wapenzi wa sanaa hiyo watajitokeza tu."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako