• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maskani yetu mjini Shanghai

    (GMT+08:00) 2016-03-03 09:17:44

    Mkahawa wa Yelixiali ni mkahawa mkubwa zaidi wa kabila la Wauyghur mjini Shanghai. Kila inapofika jioni, mkahawa wa Yelixiali unafurika wateja. Si kama tu mgahawa huu una vitoweo halisi vya Xinjiang, bali pia una vitoweo vya mkoa huo vilivyotekebishwa kutokana na upendeleo wa Washanghai, na kila usiku lazima kuna nyimbo na ngoma za Xinjiang. Chakula kitamu, pamoja na nyimbo na ngoma za kienyeji vinawafanya wateja wafurahi midomoni na mioyoni, na pia zinapamba usiku wa mji wa Shanghai.

    Neno Yelixiali katika lugha ya Kiuyghur lina maana "dunia", yaani mchanganyiko na mawasiliano kati ya tamaduni mbalimbali. Katika miaka 13 iliyopita, Waxinjiang kadhaa walianzisha mkahawa mdogo wa nyama choma, na sasa mkahawa huo mdogo umekuwa mkahawa mkubwa, na umekuwa na matawi 9 mjini Shanghai, na wafanyakazi zaidi ya 800 wa makabila 17, yakiwemo Wahan, Wahui, Wauyghur, Wakazakh, Watibet n.k. Kwa hiyo wafanyakazi zaidi ya 300 kutoka Xinjiang wakawa na maskani mpya huko Shanghai. Mpishi Sawuerjiang alizaliwa huko Hetian, kusini mwa mkoa wa Xinjiang, lakini sasa amezoea kuishi mjini Shanghai. Anasema,

    "Watu wananiuliza, umekuwa hapa Shanghai kwa miaka mingapi? Huwa nawajibu, kwa miongo ya miaka, kwa hiyo wanasema, ah, wewe ni mwenyeji wa shanghai, na mimi naona hivyo pia."

    Baada ya kuishi Shanghai kwa miaka 14, Sawuerjiang sasa anaupenda mji huo. Anaanza pilika za kazi kila siku saa nne asubuhi. Katika mkahawa wa Yelixiali, kila siku licha ya kupika bakuli zaidi ya 300 za tambi na wali maalum wa kixinjiang, pia anashughulikia usimamizi wa usalama wa vyakula vya mkahawani. Lakini kabla ya kwenda Shanghai, ndoto yake kubwa ilikuwa ni kwenda kusoma Urumqi ili aweze kuwatunza wazazi wake. Anasema,

    "Nilipokuwa kijijini, kila siku nilikuwa nafikiria kupata ujuzi, hivyo baba yangu alinipa senti 50, nikaweka akiba senti 20, baada ya nusu mwaka, kibuyu changu cha akiba kilikuwa na Yuan 270."

    Mwaka 1995 Yuan 270 kwa Sawuerjiang aliyeishi katika kijiji cha Hetian zilikuwa nyingi. Akiwa na pesa hizo na ndoto yake, Bw. Sawuerjiang alikwenda Urumqi. Akiwa huko alifanya juhudi na hatimaye katika mwaka wa nne, alikuwa na uwezo wa kupika tambi mbalimbali na vitoweo vingine. Mwaka 2000 wazazi wake walimhimiza Bw. Sawuerjiang aoe. Bw. Sawuerjiang anasema,

    "Wakati ule sikuwa na pesa kwa ajili ya harusi, na wala sikutaka kutumia pesa za wazazi kwa ajili ya harusi. Nilitaka kuchuma pesa mimi mwenyewe. Wakati ule rafiki yangu mmoja aliniuliza kama ninataka kwenda Shanghai au la, maana kulikuwa na nafasi ya kazi."

    Mwaka 2001, Bw. Sawuerjiang alipanda treni kwa mara ya kwanza kwenda Shanghai. Wakati ule Yelixiali ilikuwa mkahawa mdogo wa nyama choma ulioanzishwa na kijana wa kabila la Wahan wa mkoa wa Xinjiang Bw. Yang Jian, na Bw. Sawuerjiang alianza maisha yake mjini Shanghai katika mkahawa huo. Bw. Sawuerjiang anasema,

    "Nilipokuja Shanghai kwa mara ya kwanza sikujua basi lipi naweza kupanda kwenda kununua nguo, tulipokwenda nje hatukujua namna ya kurudi, hatukujua kuongea Kichina sanifu, hivyo hatukuweza hata kuwauliza watu, hali ilikuwa ngumu."

    Mawasiliano yalikuwa ni kikwazo kikubwa kwa wafanyakazi wengi wa makabila madogomadogo wanaokwenda kufanya kazi kwenye mazingira mapya, kwa hiyo kila mwezi mkahawa wa Yelixiali ulikuwa unatoa mafunzo kuhusu chakula cha Kiislamu, na kila wiki ulikuwa unawasaidia wafanyakazi wa kabila la Wahan kujifunza lugha ya Kiuyghur na kuwasaidia wafanyakazi wa kabila la Wauyghur kujifunza lugha ya Kichina. Wafanyakazi wa mkahawa huo pia wamekuwa walimu na kumsaidia Bw. Sawuerjiang kujifunza lugha ya Kichina. Baada ya miaka karibu mitatu, Bw. Sawuerjiang aliweza kuongea Kichina, na kuanza kujaribu kuwasiliana na watu wa sekta mbalimbali.

    Aliyekuwa na bahati nzuri zaidi kuliko Bw. Sawuerjiang, katika miaka mitatu iliyopita, msichana wa kabila la Wahui Zhang Famai ambaye kwake lugha haikuwa tatizo, lakini alikuwa mbali na jamaa zake, na kuwa peke yake mjini Shanghai akiwa mhudumu katika mkahawa huo, alikuwa anjisikia upweke. Bibi Zhang anasema,

    "Mwanzoni kila siku nilifanya kazi kwa saa zaidi ya 10, wateja wakiisha ndio na sisi tuliweza kuondoka. Nilikuwa nachoka sana kila siku. Lakini nilipokumbuka shinikizo la mama yangu, niliona napaswa kuvumilia, na polepole nikazoea."

    Katika tawi la Tianshan la Yelixiali, zaidi ya nusu ya wafanyakazi ni wa makabila madogomadogo. Katika mkahawa huo anachoona bibi Zhang Famai ni ufuatiliaji kama kutoka jamaa zake. Bibi Zhang anasema,

    "kuna siku nilikuwa na mafua na homa, na jambo lililonigusa ni kuwa mchana viongozi wetu walikuja kunitazama na kuniletea chakula bwenini. Nimefanya kazi kwa muda mrefu, lakini sikuwahi kuona viongozi kama wa mkahawa huo wanavyojali wafanyakazi wake."

    Kwenye mtandao wa internet, wateja wa Shanghai wanasifu mkahawa wa Yelixiali hivi kuwa una vitoweo vingi maalum, na vitamu sana! Katikati ya mkahawa huo kuna jukwaa dogo, maonesho ya nyimbo na ngoma, ambayo yana umaalum wa kabila la Kiuyghur.

    Maonesho ya nyimbo na ngoma ya kixinjiang ni umaalum wa mkahawa wa Yelixiali. Kundi la ngoma liliundwa miaka sita iliyopita, na wachezaji wote wanatoka mkoa wa Xinjiang. Mvulana wa kabila la Wauyghur Tuerhongjiang ni msanii mkuu wa kundi hilo. Changamoto inayomkabili Bw. Tuerhongjiang ni namna ya kuchanganya vitu vya kisasa na mambo ya jadi, na kueneza tamaduni mbalimbali za Xinjiang. Bw. Tuerhongjiang anasema,

    "Katika nyimbo au ngoma za kixinjiang, nataka kuwafanya watu wahisi uchangamfu wa watu wa Xinjiang na uundani wa utamaduni wa Xinjiang."

    Katika soko la mikahawa lenye ushindani mkali, vyakula katika mkahawa wa Yelixiali vinachanganywa na tamaduni mbalimbali. Umaalum wa vyakula vyake unatambuliwa na waislam. Wakati wa Maonesho ya kimataifa ya Shanghai, nchi 57 za kiislam na jumuiya 6 za kimataifa za kiislam zilizoshiriki kwenye maonesho hayo, zilisifu sana vyakula na huduma za mkahawa wa Yelixiali. Bila kujali kama ni Sawuerjiang, Zhang Famai au Tuerhongjiang, wafanyakazi wa makabila 17 wanaishi kama familia moja mjini Shanghai.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako