• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maelewano ni muhimu katika juhudi za kueneza lugha na utamaduni wa China kwa nje

    (GMT+08:00) 2016-03-03 16:22:54

    Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, vyuo 500 na madarasa 1000 ya Confucious vilianzishwa katika nchi na sehemu 134 duniani, na vimekuwa taasisi muhimu za kueneza lugha na utamaduni wa kichina. Katika kipindi cha leo, tutatupia macho taasisi hizo barani Ulaya na kuangalia jinsi zinavyojitahidi kueneza utamaduni wa China.

    Semina ya kwanza ya walimu wanaofundisha lugha ya kichina nchini Ubelgiji ambayo iliandaliwa na chuo cha Confucious cha Liège, ilifanyika Jumamosi iliyopita, ambapo wataalamu wa mafunzo ya lugha ya kichina kutoka Ufaransa, Hispania, Japan, China na Ubelgiji, pamoja na walimu wapatao 60 wa lugha ya kichina kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini Ubelgiji, walijadiliana kwa kina namna ya kueneza utamaduni wa China kwa ufanisi, ili kuwafahamisha wageni kwa urahisi na kwa kina kuhusu utamaduni huo.

    Kwenye semina hiyo, mgeni aliyevaa tai pamoja na nguo nyeusi ya jadi ya kichina alivutia macho sana, huyo ni mkaguzi mkuu wa mafunzo ya lugha ya kichina katika wizara ya elimu ya Ufaransa, ambaye pia ni mtaalamu mashuhuri wa mambo ya kichina, Bw. Joel Bellassen. Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, amesema, katika karne kadhaa zilizopita, watu wa Ulaya walikuwa na hamu kubwa ya kuufahamu utamaduni wa China.

    "Kwa watu wa Ulaya, katika karne kadhaa zilizopita, utamaduni wa China ulikuwa ni utamaduni wa nje wenye mvuto zaidi. Kwa mfano, katika karne ya 18, matajiri wa Ufaransa walivutiwa sana, na kupenda sana tafrija ya jioni ya kichina, samani za kichina, pamoja na sanaa za kichina, hizo zote walizipenda sana."

    Kutokana na kuendelea kuongezeka kwa ushawishi wa China kwenye jukwaa la kimataifa, utamaduni wa China umekuwa na mvuto mkubwa zaidi kwa dunia nzima, na kuifahamu China kumekuwa hitaji la zama hizi. Kansela wa elimu wa Ubalozi wa China nchini Ubelgiji Bw. Tao Hongjian anaona, hivi sasa dunia imekuwa kama kijiji, na hali hii inahitaji zaidi maelewano na ushirikiano.

    "Sote tunaishi kwenye kijiji hiki kiitwacho Dunia, inaonekana kuwa ndogo sana, na sisi wote ni majirani au wanakijiji. Kwa mawazo yetu ya utamaduni wa China, zamani tuliona kwamba ukitoa sauti kubwa katika upande mmoja wa kijiji, utasikika mara moja kwenye upande mwingine, kwa hiyo mawasiliano na ushirikiano vingekuwa rahisi. Lakini kwa hali halisi sio rahisi hata kidogo, kwa kiasi kikubwa inatokana na kutokuwa na maelewano na ushirikiano wa kutosha. Kwa hivyo, tutaongeza vipi maelewano na ushirikiano? Kwa kiasi kikubwa inategemea lugha na utamaduni, ndiyo maana mawasiliano ya lugha na utamaduni ni muhimu sana."

    Kansela Tao pia amesema, ili kuzidisha mawasiliano na maelewano ya lugha na utamaduni, na kuhimiza maingiliano na ushirikiano kati ya China na nchi mbalimbali, serikali na sekta mbalimbali za China, haswa vyuo vikuu na taasisi za elimu vimefanya juhudi kubwa, na vyuo vya Confucious pia vimetoa mchango muhimu kwenye mchakato huo. Baada ya maendeleo ya zaidi ya miaka 10, vyuo 500 na madarasa 1000 ya Confucious vimeanzishwa kote duniani, na nchini Ubelgiji pekee kuna vyuo 6 vya Confucious.

    Hata hivyo, kama mada muhimu ya utafiti, bado kuna mambo mengi yanayostahili kujadiliwa kuhusu namna ya kueneza kwa nje lugha na utamaduni wa China. Bw. Joel Bellassen anaona, kuna dosari mbili dhahiri zilizopo kwenye juhudi za China za kueneza utamaduni wake.

    "Kuna baadhi ya dosari kwenye mafunzo ya kichina kwa wageni, mojawapo ni mawazo binafsi. Kwa mfano, nafahamu vizuri utamaduni wa chakula cha London, na uko tofauti kabisa na ule wa chakula cha Paris. Kwa hiyo, hakuna chakula cha kimagharibi, kitu hicho kiko kwenye uelewa wa wachina tu."

    Dosari nyingine ni kwamba, walimu wa Kichina wanapozungumzia utamaduni wa China, huanza moja kwa moja kutaja shughuli za utendaji halisi kuhusiana na utamaduni huo. Bw. Joel Bellassen alitoa mfano ufuatao,

    "Walimu wazawa wa China wanapozungumzia utamaduni wa China, hupenda kuzungumzia utendaji halisi. Nimeshuhudia mara nyingi hali kama hiyo, kwa mfano, utamduni wa chakula, walimu hao baada ya kutoa maelezo mafupi ya dakika moja au mbili tu, wanaanza kusema, utamaduni wa chakula, haya basi, tuweke muda wa kujifunza namna ya kutengeneza Jiaozi yaani dumpling…Lakini kwa mtizamo wa sisi watu wa nchi za magharibi, kwa mtizamo wa watu wa Ufaransa, namna ya kutengeneza jiaozi na utamaduni wa chakula havihusiani hata kidogo."

    Bw. Joel anaona, dosari hizo mbili zinapaswa kuondolewa kabisa ili kuweza kuwafahamisha vizuri wageni kuhusu utamaduni wa China. Pia amependekeza kuoanisha utamaduni wa China na wa kienyeji kwenye mafunzo ya kiutamaduni, ili kuwawezesha wanafunzi waelewe kwa urahisi na kuwa na hamu ya kuufahamu zaidi utamaduni wa China.

    Chuo cha Confucious cha Liège kilichoanzishwa miaka 10 iliyopita, kimepata uzoefu mkubwa katika mafunzo ya lugha ya kichina na kueneza utamaduni wa China. Shughuli mbalimbali zilizoandaliwa na chuo hicho mwaka jana, ikiwemo kongamano la uchumi na maonesho ya wachina kuimba opera za kimagharibi, zimepata mafanikio. Mkuu wa upande wa China wa chuo cha Confucious cha Liège Zhang Dan amesema,

    "Kama ukitaka kueneza utamaduni wako kwa nje, na kuwafanya wageni wengi waukubali na kuuelewa, huwezi kuzingatia tu utamaduni wako wa jadi, bali unapaswa kutupia macho tamaduni mbalimbali duniani. Umaalumu wa utamaduni unaonekana tu wakati ukilinganishwa na tamaduni nyingine, na kwa hivyo tu umaalumu wa taifa lako pia utaonekana. Kama hazitalinganishwa, wewe ni wewe tu, utakuwa peke yako. Ndio kwa njia hii, tumejitahidi kuwafahamisha lugha ya kichina ni ya namna gani, na lugha hiyo ina utamaduni gani, na umaalumu gani wa kitaifa."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako