Kwa mujibu wa mpango uliowekwa wa kutekeleza mkakati wa kuondoa umaskini kwa hatua madhubuti, ifikapo mwaka 2020, watu wote maskini nchini China wataondokana kabisa na umaskini. Utekelezaji wa mkakati huo umefuatiliwa sana na wajumbe wa mkutano wa baraza la mashauriano ya kisiasa la China, na mkutano wa bunge la umma la China.
Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na idara ya takwimu ya China zinaonesha kuwa mwaka jana idadi ya watu maskini vijijini ilipungua kwa milioni 14.42 kuliko mwaka 2014, na kutimiza vizuri lengo la kupunguza idadi hiyo kwa watu wasiopungua milioni 10 kila mwaka. Lakini kama China ikitaka kutimiza lengo la kuondoa umaskini kabisa ifikapo mwaka 2020, katika miaka kadhaa ijayo, inapaswa kusaidia watu maskini wasiopungua milioni 10 waondokane na umaskini kila mwaka, hali ambayo ni changamoto kubwa kwa utaratibu uliopo wa kupambana na umaskini.
Akizungumzia suala hilo, mjumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bw. Jiang Gangjie amesema, mkakati wa kuondoa umaskini kwa hatua madhubuti unahitaji kurekebishwa kwa njia na mbinu zinazotumiwa zaidi kwenye kazi ya kuondoa umaskini.
"Kwanza, mpaka sasa bado hakuna takwimu sahihi za idadi ya watu maskini. Idara husika zinatakiwa kuhakikisha hali halisi ya familia zilizoandikishwa kuwa maskini, kwa kuwa baadhi ya viongozi wa kamati za vijiji wanatumia madaraka yao kunufaisha ndugu na jamaa zao kwenye kazi hiyo. Tatizo lingine, ni kuwa tumetuma maofisa kwenye serikali za ngazi mbalimbali kwa ajili ya kazi za kuondoa umaskini, kwa njia hiyo nguvu hii ikasambazwa, na si rahisi kwao kuratibu na kutumia kwa pamoja rasilimali walizonazo, naona nguvu hiyo inapaswa kukusanywa ili kuweza kutumia rasilimali kwa ufanisi zaidi. Masuala kama hayo yote yanatakiwa kujadiliwa zaidi na kutekelezwa."
Kwenye mchakato wa kutekeleza mkakati wa kuondoa umaskini kwa hatua madhubuti, moja ya masuala yanayofuatiliwa zaidi ni namna ya kugawa raslimali na kuinua ufanisi wa kazi hiyo. Mjumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa, ambaye ni mkaguzi mkuu wa usalama katika wizara ya mawasiliano na uchukuzi ya China Bw. Cheng Ping amesema, idara husika zinapaswa kuunganisha miradi ya ujenzi wa barabara na mipango ya maendeleo ya maeneo ya miradi hiyo, ili kuiwezesha itoe mchango zaidi katika kuhimiza maendeleo ya huko.
"Maeneo yenye mahitaji halisi yanapaswa kuwekezwa zaidi na kupewa misaada zaidi, mahitaji hayo yanatuhitaji tufanye uchunguzi na tathmini kuhusu hali halisi ya maeneo hayo, haifai kwamba maeneo fulani yanahitaji barabara, lakini baada ya kupata maendeleo, watu wengi wakahamia sehemu nyingine, barabara zilizojengwa hazitumwi sana, kwa hiyo ufanisi wa kujenga barabara hiyo utakuwa wa chini. Kwa hivyo kwa upande mmoja tunapaswa kufanya utafiti wa makini kuhusu hali halisi ya sasa, na kufanya uchunguzi kuhusu maendeleo ya maeneo yanayolengwa, kama vile maendeleo ya maeneo hayo yanategemea nini, na kama yana mahitaji makubwa ya mawasiliano ya barabara, baada ya kufanya kazi hizo, uwekezaji utakuwa na wenye ufanisi zaidi."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |