• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Pengo la kijinsia barani Afrika lapungua

    (GMT+08:00) 2016-03-08 08:04:43

    Nchi za Afrika imepiga hatua kubwa katika kupunguza pengo la kijinsia, lakini bado kuna mambo mengine kadhaa ambayo yanatakiwa kuondolewa ili kuhakikisha wanawake wanapata elimu, huduma za afya, na fursa za kiuchumi. Pengo hilo linaendelea kupungua kutokana na hatua za baadhi ya wanawake kuingia katika ulingo wa siasa pamoja na kufanya kazi. Katika bara la Afrika, Rwanda imepata mafanikio zaidi katika kujumuisha wanwake kwenye nafasi za uongozi, hususan kwenye bunge la nchi hiyo. Mafanikio ya Rwanda yanatokana na kwamba kuna wanawake wengi sawa na wanaume wanaofanya kazi nchini humo, huku wanawake wengi pia wakifanya kazi katika wizara mbalimbali baada ya kuimarishwa kwa idara za afya na huduma za elimu. Rais Paul Kagame wa Rwanda alipozungumzia haki za wanawake barani Afrika akisema:

    "Wakati tulianza kushughulikia swala la wanawake hapa Rwanda, tulikuwa na mambo mawili la kwanza likiwa ni haki za wanawake na la pili ni kutumia tu akili. Katika hali yetu, ikiwa tungependa kuwa na maendeleo nchini Rwanda hatungeweza kuacha nje asilimia 52 ya wananchi, na asilimia hiyo ni wanawake. Lakini pia kwa sababu za kihistoria ambapo ushirikishwaji na haki za wanawake hazijazingatiwa, mara nyingi wanawake wanabaki nyuma sio tu Rwanda lakini pia kote duniani. Kwa hivyo tulitafuta njia zuri ya kuanza kushirikisha wanawake kwa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu kama vile elimu."

    Pamoja na mafanikio hayo ya Rwanda, Mwakilishi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Simone Ellis Oluoch-Olunya amesema kuwa, nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na tatizo la usawa wa kijinsia, jambo linaloleta athari kubwa kwa maendeleo ya kijamii na kisiasa barani humo. Pamoja na hayo, Somone anasema Afrika imepata maendeleo makubwa, kwani sasa kuna wakuu watatu wa nchi ambao ni wanawake, na idadi kubwa ya wanawake na wasichana wamejiingiza zaidi katika masuala ya kisiasa.

    Olunya anasema, sera endelevu na idara za kisheria, uwekezaji katika miradi ya kijamii, na utayari wa kisiasa ni muhimu sana kwa kuwawezesha wanawake na wasichana. Amesema katika baadhi ya nchi, kuna sheria kali ambazo zinakabiliana na vipingamizi vya maendeleo ya wanawake, na ana matumaini kuwa maendeleo ya kasi ya uchumi katika bara hilo yatasaidia kuinua hadhi ya wanawake. Daktari Pindi Chana aliyekuwa naibu waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto wa Tanzania ameeleza:

    "Kupitia kwa bunge Tanzania ilipitisha protokali ya usawa wa jinsia na maendeleo ambayo ilisainiwa mwaka 2008. Utekelezaji wa usawa wa kijinsia nchini Tanzania umekuwa na mafanikio kadhaa, kwa mfano kuna ongezeko la ufahamu huku usawa kwenye jamii na haki za wanawake dhidi ya dhuluma ukiongezeka na tulizindua kampeni ya kitaifa ya kupinga dhuluma kwa wanawake mwaka 2008. Tumeshuhudia ongezeko la wanawake kwenye nafasi mbalimbali za utoaji wa maamuzi kama vile wanawake mawaziri wameongezeka kutoka asilimia 15% mwaka 2004 hadi 27% mwaka 2009 kutokana na sheria ya kuwatengea wanawake asilimia 30% ya viti bungeni."

    Katika tathmini yake ya mara kwa mara, Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa limesema kuwa serikali za nchi za Afrika zinashikilia ahadi ya kutimiza usawa wa kijinsia, lakini mila zilizopitwa na wakati, umasikini uliokithiri, na sera zisizofungamana zimekuwa kipingamizi kikubwa kufikia lengo hilo. Olunya ameeleza kusikitishwa kwake na ukiukwaji wa haki za wanawake, ambao bado unafanyika katika baadhi ya nchi za jamii barani Afrika, wakati ushiriki wao kwenye majukumu ya kitaifa ukipuuzwa. Amesema katika baadhi ya jamii, tohara kwa wanawake ni kitendo cha lazima ambacho sio rahisi kukiondoa. Ni njia ya kujikimu kiuchumi kwa mangariba. Inge Zaamwani ni mkurungezi wa shirika la uchimbaji madini la Namdeb, nchini Namibia. Bw. Inge anatuambia:

    "Inatia moyo kuona kwamba Namibia iko kwenye nafasi ya 32 katika maswala ya usawa wa kijinsia, lakini pia kwa upande wa sekta ya kibinafsi, kiwango cha wanawake wanaotoa maamuzi na kushiriki uongozi bado ni cha chini. Serikali imeweka mikakati kadhaa ya kukuza usawa wa kijinsia lakini bado kuna mengi ya kufanya na tunapaswa kuongeza juhudi zetu kuhakikisha kwamba wanawake wanawakilishwa vilivyo. Hiyo ni haki ya kikatiba. Kuna utafiti mpana unaoonyesha kwamba ukuaji wa kiuchumi unahusiana na usawa wa kijinsia na kwa hivyo kutowashirikisha wanawake ni ishara kwamba nchi hazitumii kikamilifu uwezo wake."

    Ukuaji wa uchumi wa Afrika katika miaka ya karibuni haujabadili kidhahiri hali ya wanawake na wasichana kwenye bara hilo. Olunya amesema kuwa wanawake barani Afrika bado wameendelea kuwa chini katika piramidi la kijamii, licha ya mchango wao mkubwa katika ukuaji wa uchumi. Amesisitiza kuwa ubora wa elimu na matumizi ya teknolojia mpya zitawasaidia wanawake barani Afrika kuwa na uwezo wa ushindani katika soko la ajira. Amesema nchi lazima zihakikishe kuwa wanawake wanapata elimu, ufundi staid, ardhi, na fedha, ili kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi na kujenga upya jamii.

    Amesema kuwa, hasara ya takriban dola za kimarekani bilioni 255 inapatikana kila mwaka duniani kutokana na pengo kubwa la kijinsia katika sehemu za kazi. Amesema mvutano katika sehemu za kazi kwenye baadhi ya nchi za Afrika umekuwa na athari mbaya kwa kuwawezesha wanawake. Pia amesema, wanawake katika nchi zinazokabiliwa na vurugu wanakumbana na unyanyasaji wa kijinsia. Amesema Umoja wa Mataifa na wenzi wake wameanzisha miradi kadhaa kuwasaidia wanawake wanaoathirika na mapigano katika kanda ya Maziwa Makuu, Sudan Kusini, na Somalia kukabiliana na athari za machafuko hayo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako