• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yapaswa kutoa kipaumbele katika kuhifadhi tamaduni za makabila madogomadogo

    (GMT+08:00) 2016-03-16 20:28:41

    China ni nchi yenye makabila 56, na kila kabila lina utamaduni na mila zake maalum. Lakini kutokana na maendeleo ya uchumi na mchakato wa uendelezaji wa miji, tamaduni na mila za baadhi ya makabila madogo madogo zinakaribia kutoweka. Kwenye mkutano wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China uliomalizika jumatatu wiki hii, wajumbe wengi waliona kuwa tamaduni zilizostawi za makabila madogomadogo hazipaswi kutoweka kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe ili kurithi na kuenzi tamaduni hizo maalum.

    Mwanamuziki Tenger ambaye ni mjumbe wa baraza hilo anatoka mkoa wa Mongolia ya Ndani. Ingawa amefanya kazi na kuishi mjini Beijing kwa miaka kadhaa, lakini bado anakumbuka sana na kufuatilia maendeleo ya maskani yake. Bw. Tenger anaona, ingawa maskani yake imepiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, lakini pamoja na hayo, baadhi ya mila za jadi zilizoenziwa kizazi baada ya kizazi zimeanza kubadilika.

    "Kwa mfano, nyumba za kuhamahama za wafugaji wa Mongolia ya Ndani, wote tunajua nyumba hizo zinavyokuwa, lakini sasa kutokana na maendeleo ya jamii, kwenye sehemu nyingi za mkoa huo, haswa kwenye sehemu za utalii, nyumba hizo zinajengwa kwa kutumia saruji. Baadhi ya wakati nilipowatembeza marafiki zangu, wakaniuliza hizi ni nyumba za kimongolia? Sikujua niwajibu vipi, hata mimi nilikuwa najiuliza kama kweli hizi ni nyumba za jadi za kimongolia? Zimepambwa vizuri sana ndani kama hoteli, kuna televisheni, viyoyozi, maji moto ya kuoga, na pia kuna vyoo. Nyumba za jadi za kimongolia hazijengwi kwa kutumia tofali wala msumari hata moja. Lakini kwa mtizamo wa kikabila, hizi si nyumba za jadi za kimongolia, mila za kikabila zimeanza kupotea na kutoweka kutokana na maendeleo ya kijamii, hii kweli inasitikisha sana."

    Kwenye mkutano wa Baraza la mashauriano ya kisiasa, mjumbe Tenger aliwasilisha pendekezo kuhusu uhifadhi na urithi wa utamaduni na mila za jadi kwenye maeneo ya ufugaji mkoani Mongolia ya Ndani. Anaona kuwa, utamaduni na mila ni alama muhimu ya kabila moja, na kwa kiasi fulani vinawasilisha chimbuko la kabila hilo.

    Bw. Tenger anasema, uhifadhi na urithi wa utamaduni na mila za kabila fulani vinategemea zaidi watoto, lakini baada ya kufanya uchunguzi, amegundua kuwa watoto wa sasa pia wamekuwa tofauti na wale wa enzi yake.

    "Zamani, tulipokuwa watoto, shule za msingi tulizosoma zilitoa likizo wakati kulipokuwa na pilikapilika za ufugaji, watoto walirudi nyumbani na kuwasaidia wazazi kukata manyoya ya kondoo, hii pia ni mila yetu ya jadi. Hivi sasa shule hizo zote zimehamishwa mijini, kwa hiyo watoto hukaa mijini tu wakati wote. Angalia hali ilivyokuwa sasa, hata wafugaji halisi hawawezi kutofautisha mbuzi mdogo na kondoo mdogo."

    Si mjumbe Tenger pekee aliyekuwa na maoni kama hayo, mjumbe wa kabila la Wapumi kutoka wilaya inayojiendesha ya kabila la Walisu mkoani Yunan Bi. Rongba Xina amesema, jambo linalompa wasiwasi kwa muda mrefu ni miundombinu hafifu ya mawasiliano katika maskani yake iliyoko kwenye maeneo maskini ya milimani kwenye mpaka. Amesema mpaka sasa wakazi wapatao laki 1.7 wa maeneo hayo bado wanatengwa na dunia ya nje na kukabiliwa na umaskini. Kwa upande mwingine, ujenzi wa barabara kuu ya kwanza inayounganisha maskani yake unatarajiwa kumalizika mwaka kesho, na ujenzi wa uwanja wa ndege pia umeanza.

    "Ina maana kuwa, bonde la mto Nujiang ambalo halijulikani na watu wengi pia litaanza kuendelezwa, watu wengi wataenda huko, nguvukazi, vifaa pamoja na mitaji vitaingia kwenye maskani yetu, na hapo ndipo ninakuwa na wasiwasi zaidi. Kwa kuwa uhifadhi wa utamaduni wa kikabila hugongana na maendeleo ya kiuchumi, lakini kuhimiza maendeleo ni hatua ya lazima, kiwango cha maisha ya watu wa huko kinapaswa kuinuliwa, lakini wakati huohuo utamaduni na mila za jadi zilizoenziwa kizazi baada ya kizazi huenda vitaathiriwa sana."

    Basi ni kwa njia gani maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa utamaduni vitaweza kufikia uwiano? Bi. Rongba Xinna amesema, kabila lake la Wapumi lina watu elfu 40 tu, wana lugha ya kienyeji isiyo na maandishi, kwa hiyo ni rahisi sana kwa utamaduni wa kabila hilo kuathiriwa kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Bi. Rongba Xinna ametoa mfano ufuatao,

    "Mtizamo wa watu wa makabila madogomadogo kuhusu utamaduni wao wa jadi ni tofauti na maoni ya wataalamu au wasomi wa nje, ni kama vile watu wanaotoka vijijini huenda wanapendelea zaidi mazingira ya kisasa mijini, na huona walivyo navyo ni vya kishamba sana. Kwa hiyo kwenye mchakato wa kuhimiza maendeleo ni rahisi sana kwa makabila madogomadogo kupoteza utamaduni wao."

    Bi. Rongba Xinna anatumai kwamba, serikali kuu inapaswa kutoa kipaumbele katika kuhifadhi na kurithi utamaduni wa makabila madogo madogo wakati inapoendeleza uchumi wa maeneo ya mto Nujiang, ili utamaduni maalumu wa makabila hayo uendelee kuenziwa kizazi baada ya kizazi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako