• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bi. Du Mei, mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China anayejitahidi kuhifadhi tamaduni za makabila madogomadogo

    (GMT+08:00) 2016-03-23 15:14:28

    "Nilizaliwa miaka ya 60, wakati huo hali ya maskani yangu haikuwa nzuri, umeme ulikuwa unakatika mara kwa mara, na mama alizima mishumaa mapema sana, sasa ili kututuliza, alikuwa anatusimulia hadithi kila usiku."

    Uliyemsikia ni Bi. Du Mei alivyoelezea maisha yake ya utotoni. Yeye ni mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China na pia ni mfanyakazi wa kuhifadhi utamaduni wa kabila lake la wa-Ewenki. Bi. Du Mei amesisitiza kuwa, utamaduni wa kikabila uko kwenye damu ya kila mtu wa kabila fulani, tangu anazaliwa hadi kifo chake.

    Kuanzia miaka ya 80 ya karne iliyopita Bi. Du Mei aliyekua huku akisimuliwa hadithi za jadi za kabila lake, ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya kichina kuhusiana na maisha ya ufugaji na uwindaji ya kabila lake, ambavyo vilipewa tuzo kadhaa za fasihi za kitaifa na za mkoa wa Mongolia ya Ndani. Pia alitumia miaka 9 kutembelea maeneo ya milimani kuwatafuta wazee wa kabila la waEwenki, ili kukusanya mashairi ya hadithi za kabila hilo yanayokaribia kutoweka. Mashairi ya jadi ya kabila ya waEwenki huonesha moyo mkubwa na maisha ya kawaida ya watu wa kabila hilo wanaoishi maeneo ya misitu na mbuga za majani zilizoko kaskazini mashariki mwa China. Kutokana na uzoefu huo maalumu, Bi. Du Mei amehisi kwa kina dharura na umuhimu wa kuhifadhi utamaduni wa kabila lake.

    "Katika miaka ya 80, mimi na mama yangu tulitembelea sehemu kadhaa, kwa kuwa mama yangu anawafahamu zaidi, hata sasa kila nikikumbuka uzoefu huo bado nasikia huzuni. Wakati huo tulimhoji mzee mmoja mwenye miaka zaidi ya 80, nakumbuka tulimnunulia dawa nyingi za maumivu, mzee alikuwa anafurahi sana kutuona, na tulikaa huko tukimsikiliza anavyosimulia hadithi za jadi kutwa mzima. Baada ya mwaka mmoja au miwili tu, mzee huyo alifariki dunia. Maisha ni kama hivyo, kama hufanyi haraka, mambo ya kiutamaduni yanapotea tu pamoja nao."

    Bi. Du Mei ametambua kuwa, kwa kabila la waEwenki lenye lugha ya kienyeji isiyo na maandishi, ambalo halina watu wengi na wamesambaa kwenye maeneo makubwa, utamaduni muhimu wa kabila hilo kama vile mashairi ya hadithi, unaweza tu kurithiwa kwa njia ya masimulizi. Lakini watu wanaofahamu mashairi ya hadithi ya kabila hilo ni wachache sana, na wengi wao wamezeeka, hali ambayo inampa Bi. Du Mei wasiwasi mkubwa. Bi. Du Mei amesema, kupungua kwa mazingira ya kiutamaduni yanayotokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea kwenye mazingira ya kijamii na njia za maisha, kumewafanya vijana wa kabila la waEwenki kutofahamu utamaduni na mila za kabila lao.

    Mwaka 2003, Bi. Du Mei alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la awamu ya 10 la mashauriano ya kisiasa la China. Kuanzia hapo alijitahidi bila kusita kwa ajili ya uhifadhi na urithi wa utamaduni wa kabila la waEwenki. Bi. Du Mei amerekodi na kuandika mashairi ya hadithi za kabila hilo kwa njia ya matamshi yake.

    "Tukiwa ni kabila lenye idadi ndogo ya watu, nahisi nawajibika zaidi na inanibidi kujitahidi kuhifadhi utamaduni wa kabila letu, lakini sina uhakika, kwa kuwa tayari unakaribia kutoweka. Huu ni wasiwasi wangu mkubwa, tunachoweza kufanya kwa kizazi chetu ni kujitahidi kukusanya na kurekodi mashairi haya ya hadithi kwa njia ya sauti na video, kwa kufanya hivyo vizazi vya baadaye vitaweza kusikiliza na kutazama, ili yaweze kuenziwa, naona huu ni wajibu wetu."

    Akiwa mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa, ili kuinua mwamko wa umma kuhusu hatari ya kutoweka inayokabili lugha na tamaduni za makabila madogomadogo, Bi. Du Mei aliwasilisha mapendekezo mengi kuhusu uhifadhi na urithi wa utamaduni wa makabila madogo madogo, na baadhi kati yao yametekelezwa au kufuatiliwa sana na jamii, jambo lililomfurahisha sana Bi. Du Mei.

    Katika ripoti yake kwenye mkutano wa Baraza la awamu ya 12 la mashauriano ya kisiasa la China, mwenyekiti wa baraza hilo Bw. Yu Zhengsheng amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika uhifadhi wa urithi wa kiutamaduni katika mwaka 2015, na kuweka malengo ya mwaka huu. Akizungumzia ripoti hiyo, Bi. Du Mei amesema, China, yenye makabila 56, kila kabila lina umaalum wake, na namna ya kuonesha umaalum huo na kuyafanya makabila hayo yafundishane na kusaidiana ni moja ya masuala yanayokabili sekta ya utamaduni nchini China. Bi. Du Mei anasema,

    "Nchi yetu ina mazingira yenye mchanganiko wa tamaduni za makabila mbalimbali, ni lazima tustawishe utamaduni wa kila kabila, ili zisije tamaduni za makabila yote zikafanana. Nguvu bora ya nchi yetu ni kwamba, kila kabila lina uhodari wake wa kipekee, suala ni namna ya kuzienzi na kuzifanya zifundishane, ili kuwafahamisha watu wengi zaidi kuhusu utamaduni na umaalumu wa makabila tofauti."

    Bi. Du Mei anaona, kushikilia yanayohitajika na umma, na kueneza yanayopendelewa na wananchi ni mbinu mwafaka ya kustawisha sekta ya utamaduni nchini China.

    Mwaka huu, Bi. Du Mei ametekeleza majukumu yake kama mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa kwa awamu tatu mfululizo. Kila anapofikiria hivi, anaona furaha na pia wasiwasi. Bi. Du Mei amesema, hivi sasa kazi ya kuhifadhi na kurithi tamaduni za makabila madogomadogo imepata mafanikio makubwa, na katika siku za baadaye anatumai kwamba kazi hiyo itaweza kushirikisha watu wengi zaidi, na kuungwa mkono zaidi kisera na kifedha. Bi. Du Mei pia ameeleza imani yake kwamba kwa njia hiyo, juhudi za kizazi baada ya kizazi hakika zitahimiza ustawi endelevu wa sekta ya utamaduni nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako