• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Shughuli za kutangaza tiba ya jadi ya kichina zafanyika mjini Prague, Czech

    (GMT+08:00) 2016-04-06 15:29:13

    Kwenye ziara ya rais Xi Jinping wa China nchini Jamhuri ya Czech wiki iliyopita, miji ya Beijing na Prague ilisaini makubaliano ya kuwa miji rafiki. Pamoja na kusainiwa kwa makubaliano hayo, shughuli za kutangaza tiba ya jadi ya kichina zilifanyika kuanzia Jumapili hadi Jumanne wiki iliyopita mjini Prague.

    Kwenye shughuli hizo, wataalamu 8 wa tiba ya jadi ya kichina wametoa ushauri wa kitabibu bila malipo kwa wagonjwa wa huko, na wataalamu wa kampuni ya dawa za jadi za kichina ya Tong Ren Tang pia wamefanya mihadhara kuhusu tiba ya jadi ya kichina na namna ya kutunza afya kwa mujibu wa nadharia za matibabu hayo. Aidha, mamlaka za usimamizi wa dawa za China na Czech, wajumbe wa mashirikisho ya dawa na wataalamu husika kutoka nchi hizo mbili wamefanya mkutano wa Baraza la kitaaluma kuhusu dawa na tiba ya jadi ya kichina.

    Shughuli hizo zilizoandaliwa kwa pamoja na serikali ya miji ya Beijing na Prague, zinalenga kuzidisha mawasiliano ya kiutamaduni kati ya watu wa China na Czech, na kuwafahamisha zaidi watu wa Czech kuhusu utamaduni wa China, haswa utamaduni wa tiba ya jadi ya kichina. Kwenye duka la dawa la Tong Ren Tang mjini Prague, shughuli za kutoa matibabu ya jadi zimevutia wenyeji wengi na wachina wanaoishi nchini Czech.

    Naibu meneja mkuu wa kampuni ya dawa za jadi za kichina ya Tong Ren Tang Bi. Ding Yongling amesema, shughuli hizo zina maana kubwa. Amesema, wakiwa ni waenezaji wa tiba ya jadi ya kichina, ni jukumu lao kutoa huduma kamili za kutunza afya kwa watu wa Czech.

    "Kwanza, ni lazima tuzingatie mila na desturi za kienyeji, tunapaswa kuwafahamisha wenyeji kuhusu dawa na matibabu yetu, na kuwafanya wachague matibabu yetu, kwa hiyo naona kuna ulazima wa kufanya shughuli hizi kama vile mihadhara ya kitabibu na mafunzo kuhusu njia za kutunza afya. Ziara ya rais Xi nchini Czech imetoa fursa kubwa, na haswa kwa Beijing na Prague kusaini makubaliano ya miji ya urafiki, matibabu ya jadi ya kichina yamechukuliwa kama balozi, naona ni muhimu sana. Tunapaswa kutumia vizuri fursa hii, kuandaa na kupanga vizuri shughuli mbalimbali husika, ambazo pia zitasaidia watu wa Czech kufahamu zaidi tiba ya jadi ya kichina na kuichagua kama mbinu za kutunza afya katika siku za baadaye."

    Kampuni ya Tong Ren Tang ilifungua duka lake la kwanza mjini Prague mwaka jana, ambalo ni la nne barani Ulaya. Mkurugenzi wa bodi ya kampuni ya Tong Ren Tang, Bw. Shang Guosheng amesema, matibabu ya jadi ya kichina yanapendwa na wenyeji wengi, na yana mustakabali mkubwa kwenye soko la Czech.

    "Watu wengi wa Czech wamevutiwa sana na dawa na tiba ya jadi ya kichina, tunaona matibabu haya ni zawadi kubwa ya wachina kwa dunia, kwa hiyo tunatumai kuileta tiba hii nchini Czech, ili watu wengi zaidi wa nchi hiyo waweze kunufaika na rasilimali kubwa ya kiutamaduni ya taifa letu la China."

    Katika miezi kadhaa baada ya kufunguliwa kwa duka hilo mjini Prague, wagonjwa wengi walikwenda kutafuta matibabu. Lucy ni mmojawapo, na alipata habari kuhusu kampuni ya Tong Ren Tang kutoka kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook. Lucy alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kichwa na mgongo na tatizo la kukosa usingizi, na baada ya kutumia dawa za jadi za kichina pamoja na matibabu ya usingaji kwa muda kadhaa, amepona matatizo hayo. Anasema,

    "Naona, waczech wengi wanapenda tiba ya jadi ya kichina, lakini wanajaribu kupewa matibabu mara moja mbili tu, lakini kwa kweli usingaji au dawa za jadi za kichina zinapaswa kutumiwa mfululizo kwa muda mrefu ili kuonesha ufanisi wake."

    Meneja mkuu wa kampuni ya Tong Ren Tang, Bi. Ding Yongling anasema, Czech ni nchi mpya ambayo kampuni yake inatoa huduma za dawa na matibabu, na watu wa nchi hiyo hawana ufahamu kuhusu dawa na tiba ya jadi ya kichina, kwa hiyo kampuni yake itatoa huduma kamili na za asili, ili kuwasaidia watu wa nchi hiyo katika kujenga afya na kuwa na njia bora za maisha.

    "Naona kutokana na kuongezeka kwa juhudi za kutangaza tiba ya jadi ya kichina, wenyeji wengi zaidi wataifahamu zaidi, halafu kiwango cha faida pia kitainuka zaidi. Muhimu zaidi ni ushawishi wa kijamii, hali inayolingana na mkakati wa kampuni yetu kwa kuzingatia manufaa ya kiuchumi na vile vile ushawishi wa kiutamaduni. Naona lengo letu si kuchuma pesa tu, pia tunapaswa kutoa matibabu bora ya jadi ya kichina na njia bora za kutunza afya vitakavyoinufaisha jamii ya hapa."

    Naye Bw. Wang Guowei ni mmoja wa wataalamu mashuhuri wa matibabu ya jadi ya kichina walioshiriki kwenye shughuli hizo, amesema anafurahi kuweza kutangaza tiba ya kichina katika nchi za nje.

    "Wataalamu wetu, kwa upande mmoja wamekuja kuwafahamisha kuhusu tiba ya jadi ya kichina, kwa upande mwingine, wanaonesha kwamba, tiba hiyo pia ni aina ya utamaduni, kwa hiyo, kueneza tiba hiyo na utamaduni wake kutawaletea watu wa nchi mbalimbali duniani furaha zinazotokana na huduma za kimatibabu na vilevile utamaduni. Naona tiba ya kichina na utamaduni wake vinakubaliwa zaidi duniani."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako